Kauli za wadau na ripoti za waangalizi wa uchaguzi mkuu

Dar es Salaam. Wataalamu wa siasa na utawala bora wamezitaka mamlaka za uchaguzi nchini kuzingatia kwa umakini ripoti na mapendekezo yanayotolewa na waangalizi pamoja na watoa elimu ya uchaguzi, wakisisitiza kuwa wadau hao ni nguzo muhimu katika kujenga misingi ya chaguzi huru, haki na zenye amani.

Kauli hiyo imetolewa zikiwa zimesalia siku tisa kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu Jumatano Oktoba 29, 2025, taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi zinatarajiwa kushiriki kufuatilia mwenendo wa uchaguzi na kutoa ripoti zao.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeshatangaza orodha ya taasisi 252, zilizopata vibali rasmi kushiriki katika uchaguzi huo, kati ya hizo 164 zinatoa elimu kuhusiana na uchaguzi na 88 zitafuatilia mchakato wa uchaguzi.

Kati ya taasisi hizo, 76 ni za ndani na 12 ni za kimataifa kutoka mabara ya Ulaya na Amerika. Hatua hiyo imepongezwa na wadau wa demokrasia kama ishara ya uwazi na ushirikishwaji mpana wa wadau, ikionekana kuongeza uaminifu wa wananchi kwa mamlaka za umma.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, uwepo wa waangalizi wa uchaguzi, huthibitisha kuwa mchakato wa kidemokrasia unasimamiwa kwa uadilifu na kwa kuzingatia sheria.

Waangalizi hufuata hatua zote muhimu za uchaguzi kuanzia kampeni, upigaji kura, kuhesabu na kutangaza matokeo, kabla ya kutoa ripoti huru zenye mapendekezo ya maboresho.

Ripoti hizo zimeelezwa kuwa ni rejea muhimu kwa serikali, mamlaka zinazosimamia uchaguzi na wadau wengine, katika kuboresha mifumo ya kisiasa na kisheria kwa chaguzi zijazo. Wataalamu wanasema utekelezaji wa mapendekezo hayo unaweza kuimarisha uadilifu wa uchaguzi, kupunguza migogoro ya kisiasa na kuongeza imani ya wananchi kwa mamlaka za uchaguzi.

Uwepo wa waangalizi pia huondoa hofu ya udanganyifu au vurugu, kwa sababu wananchi wanaposhuhudia taasisi huru zikifuatilia mchakato mzima, hujenga imani kuwa uchaguzi unafanyika kwa uwazi na uwajibikaji.

Kwa upande mwingine, watoa elimu ya uchaguzi wanaelezwa kuwa na jukumu kubwa la kukuza uelewa wa wananchi kuhusu haki na wajibu wao wa kiraia. Kupitia elimu ya uraia, mijadala ya kijamii na kampeni za kitaifa, wananchi huelimishwa namna ya kupiga kura kwa usahihi, umuhimu wa kudumisha amani na madhara ya rushwa ya kisiasa.

Elimu hii husaidia kuondoa makosa kama kupiga kura mara mbili, kushawishiwa na hisia za vyama au kushiriki vurugu, sambamba na kuhamasisha ushiriki wa makundi yaliyokuwa pembezoni kama wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Paul Loisulie anasema taasisi hizi ni jicho la tatu katika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa misingi ya kisheria na kisiasa. “Waangalizi na watoa elimu ni sehemu muhimu ya mchakato mzima wa uchaguzi. Wanalinda uhalali wa uchaguzi kwa macho mawili; moja la kisheria na jingine la kisiasa,” anasema.

Hata hivyo, Dk Loisulie anabainisha changamoto kubwa barani Afrika kuwa ni kutotekelezwa kwa mapendekezo ya waangalizi, hali inayopunguza athari chanya za kazi yao.

“Bahati mbaya ripoti nyingi huishia makabatini bila utekelezaji. Hii inapunguza nguvu ya ushauri wao, ingawa nyaraka hizo hubaki kuwa rejea muhimu za kihistoria na kitaalamu,” anasema.

Kwa upande wake, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda anasema waangalizi na watoa elimu ni wadau muhimu wanaojenga imani ya jamii kuhusu usalama na uhalali wa uchaguzi.

“Wananchi wanaposhuhudia taasisi huru zikitoa elimu au kufuatilia uchaguzi, hupata matumaini kuwa uchaguzi utakuwa huru, wa haki na usio na upendeleo,” anasema Dk Mbunda.

Anaongeza kuwa ripoti zinazotolewa baada ya uchaguzi ni nyenzo muhimu za kitaalamu ambazo zikizingatiwa, zinaweza kusaidia kuboresha mifumo ya uchaguzi wa baadaye. “Ripoti hizo zina mchango mkubwa katika kuboresha mifumo ya uchaguzi nchini ikiwa mapendekezo yake yatafanyiwa kazi,” anasisitiza.

Dk Mbunda anaongeza kuwa mamlaka za uchaguzi zinapojua zinaangaliwa na taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi, hulazimika kufuata sheria na taratibu ili kuepuka kupewa ripoti zenye maoni hasi.

Wataalamu hao wanashauri serikali kuendelea kuweka mazingira huru kwa asasi za kiraia na waangalizi kufanya kazi bila hofu, pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa taarifa kwa wakati. Pia, wanapendekeza kuimarishwa kwa ushirikiano kati ya Tume ya Uchaguzi, asasi za kiraia na vyombo vya habari ili kuongeza uwazi na uwajibikaji katika mchakato mzima.

Wanasema demokrasia haiwezi kukua bila elimu na uangalizi makini. Kila kura, wanasema si tu inapaswa kuhesabiwa bali pia kueleweka. Elimu na ufuatiliaji wa kitaalamu hufanya kila raia atambue maana ya kura yake na wajibu wake katika kulinda amani.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, Tanzania inapaswa kuendelea kulinda nafasi yake kama mfano wa demokrasia barani Afrika kwa kuhakikisha chaguzi zake zinabaki huru, za haki na zenye uwazi.

Wanasisitiza kuwa uwepo wa waangalizi na watoa elimu unaleta uwajibikaji, huimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za umma na kujenga misingi imara ya amani na utulivu wakati wa uchaguzi.