BALOZI MULAMULA AZUNGUMZA NA RAIS DK. NETUMBO, IKULU WINDHOEK NAMIBIA

:::::::

Mjumbe Maalum wa Umoja wa Afrika kuhusu Agenda ya Wanawake, Amani na Usalama, Balozi Liberata Mulamula, amefanya mazungumzo na Rais wa Namibia Dk.Netumbo Nandi -Ndaitwah, Ikulu Jijini Windhoek.

Katika mazungumzo hayo, Dk. Netumbo alimpongeza kwa kuteuliwa kuwa Mjumbe Maalum wa  Umoja wa Afrika na kwamba Namibia ilifurahishwa sana na uteuzi huo hususan Mtanzania kutokana na mahusiano mazuri ya kihistoria baina ya Namibia na Tanzania. 

Dk. Netumbo, alimhakikishia ushirikiano kutoka Serikali ya Namibia katika kutekeleza majukumu yake vizuri ya kiofisi.

Alieleza kuwa, Namibia kihistoria imekuwa mstari wa mbele katika kusukuma Agenda ya Wanawake Amani na Usalama wao wakiwa waanzilishi wa Azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ushiriki wa Wanawake katika masuala ya Amani na Usalama miaka 25 iliyopita. 

Aidha, alisema katika Serikali yake, amehakikisha wanawake na vijana  wanashika nafasi za uongozi maeneo muhimu akiamini kwamba nchi haiwezi kupata maendeleo endelevu kama sio shirikishi. 

Serikali yake kwa sasa inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya Wanawake katika nafasi kuu za uongozi ikiwemo Makamu wa Rais, Spika, Katibu Mkuu  wa Chama, Katibu Mkuu Kiongozi na asilimia 57 ya Mawaziri wakiwa Wanawake na Vijana akiwemo, Waziri wa Mambo ya Nje na Biashara ya Kimataifa, Elimu.