SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limewatangaza waamuzi kutoka Benin ndiyo watachezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya Yanga dhidi ya Silver Strikers itakayochezwa Jumamosi Oktoba 25, 2025.
Mechi hiyo ya marudiano kuwania kufuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo, itachezwa kuanzia saa 11:00 jioni kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Yanga inayoingia uwanjani ikiwa imetoka kufungwa bao 1-0 ugenini nchini Malawi, inahitaji ushindi wa angalau tofauti ya mabao 2-0 ili kufuzu hatua ya makundi kwa msimu wa nne mfululizo kwenye mashindano ya CAF baada ya 2022-2023 kufanya hivyo upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, kisha 2023-2024 na 2024-2025 upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi hiyo, mwamuzi wa kati atakuwa Adissa Abdul Raphiou Ligali kutoka Benin kama ilivyo kwa msaidizi wake namba moja, Lucien Todégnon Hontonnou. Lamien Dofinte Adolphe anayetokea Burkina Faso ni msaidizi namba mbili.
Mwamuzi wa akiba (Fourth Official) atakuwa Dedjinnanchi Tanisla Ahomlanto Dedjinnand wa Benin, wakati kamishna wa mechi ni Ahmad Nazeer Hossen Bowud (Mauritius) na mtathimini waamuzi ni Andriamparany Lova Rakotoarimanana (Madagascar).
Rekodi zinaonyesha, Adissa Ligali alichezesha mechi moja pekee ya Kundi A katika michuano ya CHAN 2024 iliyofanyika nchi za Tanzania, Kenya na Uganda mwaka 2025, iliyochezwa Agosti 10, 2025 kwenye Uwanja wa Nyayo nchini Kenya, Angola ikiichapa Zambia mabao 2-1.
Katika msimu wa mashindano 2023-2024, mwamuzi huyo alichezesha jumla ya mechi 11 zikiwamo za kufuzu Kombe la Dunia, CHAN, AFCON na Kombe la Shirikisho Afrika. Jumla ya kadi 41 za njano alitoa katika mechi hizo ikiwa ni wastani wa 3.7. Kadi nyekundu ni moja pekee.