Samia aahidi neema ya makazi kwa Watanzania

Dar es Salaam. Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, ameeleza pamoja na kuendeleza mambo manne ikiwemo uwezeshaji wananchi kiuchumi ambayo Serikali yake imejikita kufanya, nguvu kubwa itawekwa katika kuboresha makazi ya watu.

Akielezea jitihada za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) la kuendeleza miradi ya ujenzi wa makazi ya kudumu katika miji mbalimbali nchini, Samia amesema ajenda kuu katika eneo hilo ni kuhakikisha kwamba wananchi  wanapata makazi ya kudumu.

Samia ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ameyasema hayo leo Jumatano Oktoba 22,2025 wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika uwanja wa Kecha, Kinyerezi wilayani Ilala.

Samia amesema Tanzania ina uhitaji wa nyumba milioni tatu kila mwaka na kuwa Serikali yake itajenga nyumba 5,000 katika miji mbalimbali nchini.

“Kwenye makazi tunajitahidi Tanzania tuna uhitaji wa nyumba milioni tatu kwa mwaka na kwa sababu hatukuwa tukipunguza hiyo kadhia kwa hiyo sasa tunajielekeza kwa nguvu zote kwenye makazi,” amesema na kuongeza;

“Kitaifa NHC limejipanga kutekeleza mipango kadhaa ya makazi lakini wana mradi wa ujenzi wa nyumba (Samia housing scheme) wanajipanga kujenga nyumba 5,000,”amesema Samia.

Rais Samia amesema katika hizo nyumba 560 zimeshakamilika eneo la Kawe, nyumba 400 zinaendelea kujengwa eneo la Mtoni (Dar) na nyumba 1,000 ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni ambapo nyumba 200 zitajengwa eneo la Urafiki Dar es Salaam na nyumba 800 mkoani Dodoma.

Kwa upande wa Ilala ambayo ndiyo wilaya inayobeba jiji la Dar es Salaam, Samia amesema miradi ya ujenzi wa nyumba za makazi na biashara ikiwemo eneo la Kariakoo utafanyika kutokana na kamati aliyounda  kubaini matatizo makubwa Kariakoo.

“Sasa NHC linajielekeza Kariakoo ambapo kuna miradi 16 ya ubia baina ya wafanyabiashara na Serikali na kazi ya kujenga inaendelea. Hizi ni jitihada ambazo zinaendana na mkakati wetu wa kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara katika soko hilo,” amesema.

Akizungumzia mikakati mingine ambayo Serikali yake imeifanya na itaenda kuifanya iwapo itapewa ridhaa, Samia amesisitiza uboreshaji wa miundombinu ya usafiri na usafirishaji ikiwemo bandari, reli, anga na miundombinu ya barabara na madaraja huku kwa wilaya ya Ilala akiahidi uboreshaji wa barabara zikiwemo za ndani.

Katika bandari kiongozi huyo ametolea mfano Bandari ya Dar es Salaam na kuwa tayari wameiboresha na wanaendelea kuboresha bandari ya Mtwara, Tanga na bandari zingine kwa upande wa Tanzania Bara ili Tanzania ifanye biashara na nchi za Malawi na Msumbiji.

Katika usafiri wa anga, Samia amesema mbali ya uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Serikali yake imeendelea kujenga na kuboresha viwanja vingi ndani ya Tanzania na kuwa ilani watakayoenda kuitekeleza wamejipanga kununua ndege nane ili Shirika la Ndege (ATCL) itanue safari zake.

Mgombea huyo akizungumzia ujenzi wa reli ametolea mfano reli ya SGR kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo tayari inafanya kazi vizuri, ameeleza kuwa tayari mikakati ya kuendeleza vipande vya Dodoma hadi Uvinza, Kigoma tayari makandarasi wanaendelea.

Akizungumzia kuhusu ujenzi wa masoko, Samia ameahidi wakipewa ridhaa eneo la Jangwani ambapo ujenzi wa daraja utafanyika, watajenga soko kubwa la kisasa kwa ajili ya wamachinga ambalo litakuwa na uwezo wa kubeba wafanyabiashara wengi kwa wakati mmoja.

“Tumefanya maboresho kwenye mazingira ya kufanya biashara na tumeunda Tume ya kuangalia kodi kitaifa nchi nzima, tutaenda kuangalia kodi mpaka kwa wafanyabiashara wadogo ili mambo yawe mazuri. Tumekaa na umoja wa wafanyabiashara Kariakoo, uongozi wa machinga na makundi mengi tumewasikiliza shida zao,” amesema.

Kuhusu utawala amesema ili kuhakikisha nchi inaongozwa vizuri ni lazima kuangalia masuala ya watu na kuwashirikisha ili kutafutia ufumbuzi wa masuala yanayowakabil,i ambapo ametaja baadhi ya tume alizounda ili kuangalia masuala mbalimbali ikiwemo tume ya kuangalia haki jinai, tume ya kuangalia uhusiano wa mambo ya nje.

“Tume zingine ni ile ya kodi pamoja na kuangalia mgogoro wa Ngorongoro. Tume hizi zimemaliza kazi wakati tunaingia kipindi cha kampeni kwa hiyo wataleta taarifa na mkitupa ridhaa na baada ya Serikali kuundwa tutaleta taarifa na tutaboresha kodi zetu Tanzania na tutachukua hatua stahiki.

“Hakuna anayejua kila kitu ukitaka kuendesha nchi kwa amani lazima uwashirikishe wenye nchi na ndiyo demokrasia tunafanya jazi kwa ajali ya watu maana na hao watu ndiyo wenye mpini katika kuendesha nchi hii na si watawala wenye mpini wa kuendesha nchi hii,” amesema.

Awali mgombea ubunge wa Jimbo la Ilala, Mussa Zungu na mgombea Ubunge jimbo la Arusha mjini, Paul Makonda walieleza maamuzi ya Samia ya kuhusisha sekta binafsi katika uboreshaji wa bandari ambavyo yamesaidia kuongezeka kwa mapato yanayokusanywa na kuipa Serikali uwezo wa kutoa huduma za kijamii.

Zungu amesema  kuwa kabla ya maamuzi ya kuwekeza katika bandari ya Dar es Salaam, makontena yaliokuwa yakiingia katika bandari hiyo yalikuwa kati ya 600,000 hadi 700,000 na hivi sasa yameongezeka hadi kufikia zaidi ya milioni 1.8, na kueleza kuwa uchumi wa nchi umeendelea kuimarika kutoka anguko la Uviko-19.

“Kabla ya uwekezaji huu, TRA ilikuwa inakusanya mapato ya uchumi wa forodha Sh10 trilioni kwa mwaka 2022/23 na kuongezeka hadi Sh12 trilioni mwaka  2024/25,” amesema na kuongeza kuwa maamuzi ya kushirikisha sekta binafsi sio ya kuogopwa bali ya kuthaminiwa ili kuwezesha taifa kukua zaidi kiuchumi.

“Maamuzi yako ya kuboresha na kuleta wawekezaji kwenye bandari yalipingwa sana na baadhi ya watu. Lakini nikupongeze kwa juhudi, uhodari na ushupavu wako wa kusimamia jambo hili ukijua litaleta manufaa kwa taifa na tayari matokeo yapo wazi. Lazima Watanzania wakurudishe uendelee kuyafanya haya,” amesema.

Naye Makonda ambaye aliwahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alieleza takwimu mbalimbali za faida iliotokana na uwekezaji katika bandari akisema kuwa uamuzi huo umeboresha utendaji na utosji huduma katika bandari za nchini.

Alisema kabla ya uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam, ilikuwa na uwezo wa kupokea mzigo tani milioni 18, bandari ya Mtwara ilikuwa na uwezo wa kupokea mzigo tani 590,000 na uwezo wa bandari ya Tanga ulikuwa kupokea mzigo tani 890,000.

“Takwimu zinaonyesha kuwa uwekezaji wake umepelekea bandari ya Dar es Salaam kuwa na uwezo wa kupokea mzigo tani milioni 27  kutoka tani milioni 18. Bandari ya Mtwara imeweza kupokea tani milioni 2.5 kutoka tani 590, 000 na bandari ya Tanga  kutoka tani 890,000 hadi tani milioni 1.3,” amesema.

Aliongeza: “Kwa upande wa mapato, tumetoka kwenye Sh800 bilioni kwa mwaka hadi Sh2 trilioni kwa mwaka. Nawashangaa wanaokosoa bila kupiga mahesabu na kuona mapinduzi yanayoendelea,” amesema.

Amesema meli zilikuwa zinakaa kwa siku 15 ikisubiri kwenda kupakia mzigo. “Hili nalo limebadilika. Sasa Meli inakaa kwa siku tano tu na kupakia mzigo, hatua ambayo inawapa Watanzania ujasiri wa kukuchagua ili uendeleze haya makubwa unayoyafanya.”