Dodoma. Zaidi ya watu 400,000 kutoka kaya maskini nchini wamenufaika na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf) wamehitimu rasmi na kuanza kujitegemea kiuchumi, hatua inayotajwa kuwa ni mafanikio makubwa ya mpango huo wa kijamii.
Akizungumza wakati wa ziara ya kutembelea baadhi ya walengwa wa mpango huo mkoani Dodoma leo Oktoba 22, 2025, Mkuu wa Chuo cha Shirikisho la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika nchi za Afrika Mashariki na Kati (ECASSA), Emmanuel Magoti, amesema mafanikio hayo yametokana na juhudi za Tasaf kuwajengea uwezo walengwa kwa kuwapatia elimu ya matumizi bora ya fedha, na mafunzo ya ujasiriamali.
“Nawashukuru sana Tasaf kwa kazi nzuri wanayoifanya kuhakikisha walengwa wanapiga hatua na kuanza kujitegemea kupitia ujasiriamali wa aina mbalimbali,” amesema Magoti.
Magoti amebainisha kuwa kutokana na mafanikio hayo, mpango huo utaendelea kwa awamu ya tatu ili kuwafikia walengwa zaidi na kuwawezesha kuinuka kiuchumi pamoja na familia zao katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, amesisitiza kuwa kuna mabadiliko chanya kwa walengwa pamoja na ufanisi katika utekelezaji wa mpango huo, hivyo Tasaf inastahili pongezi kwa juhudi zake za kuleta mabadiliko ya kweli kwa jamii.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Tasaf, Melikzedek Nduye, ameushukuru uongozi wa taasisi ya ECASSA kwa ushirikiano wake na kutoa wito kwa walengwa kuendelea kuwa wabunifu na kutumia maarifa waliyopata ili kujikwamua kabisa na hali ya maisha duni.
“Tunaamini walengwa wetu wakiwa na bidii na ubunifu, wataweza kujiimarisha kiuchumi na hatimaye kujitegemea kikamilifu,” amesema Nduye.
‘’Mradi umeanza nikiwa na watoto wawili wakiwa shule ya msingi ambao wamefanikiwa kumaliza elimu sekondari na wanaelekea kujiunga na chuo kikuu mwaka huu,’’ amesema Hellena John.
Licha ya mafanikio hayo wanufaika hao pia wameomba kujengewa kisima kikubwa na kuwekewa miundombinu ya umeme ili iwasaidie kuendesha shughuli za kilimo ndani ya kipindi chote cha mwaka.
Evalina Wami amesema ujenzi wa kisima hicho utainua kiwango cha uzalishaji na kuwapa fursa ya kuanzisha miradi mingine mikubwa kwa kutumia faida wanayoipata kwenye mradi huo.