OMO: Sihofii kura ya mapema, nitashinda tu

Pemba. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema hana wasiwasi na kura ya mapema, akisema ana uhakika wa kuibuka mshindi katika uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Kwa mujibu wa kifungu cha 82 cha sheria ya uchaguzi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), upigaji kura ya mapema utawahusisha watendaji wanaosimamia majukumu ya uchaguzi siku ya uchaguzi.

Kura ya mapema mwaka huu itapigwa Oktoba 28 ikihusisha pia vyombo vya ulinzi na usalama.

Ingawa kwa nyakati tofauti viongozi wakuu wa ACT Wazalendo, wamekuwa wakitoa kauli ya kutokukubaliana na kura ya mapema ikipigwa katika uchaguzi wa mwaka huu.

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema hana wasiwasi na kura ya mapema, akisema ana uhakika wa kuibuka mshindi katika uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Lakini leo Othman amewaambia wananchi wa Pemba “kura ya mapema haitushughulishi ACT, hata wakitaka tumgaie zote tutampa, achukue lakini naapa hashindi,” amesema Othman bila kufafanua mgombea yupi.

Othman ameeleza hayo leo Jumatano Oktoba 22,2025 alipokuwa  akihutubia mkutano wa hadhara wa kampeni zake za lala salama katika Uwanja wa Shumba ya Vyamboni Jimbo la Tumbe, kabla ya kuzifunga rasmi katika viwanja vya Tibirinzi Pemba na Kibanda Maiti Unguja.

Mgombea huyo, amesema ACT Wazalendo inajiamini na ina uhakika wa kushinda katika uchaguzi wa Oktoba 29 pasipo kutegemea matokeo ya kura za mapema.

“Hata akisema tumpe kura 10,000 au 20,000 tuna uhakika wa ushindi. Wazanzibari wameamka CCM, ACT na walioko katika sekta wapo tayari kusimama kuinusuru Zanzibar yao,” amesema Othman.

Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT, amesema akichaguliwa Oktoba 29, atahakikisha anaijenga upya Zanzibar ili kurudi katika misingi ya ustaarabu ikiwemo kuondoa vitendo vya kifisadi na rushwa.

“Watu wa Tumbe tuungane na tusimame pamoja, hawa jamaa wamekwisha tusimame na Wazanzibari twende tukainusuru Zanzibar ili tuondoe viburi vilivyopita mpaka,” amesema Othman.

Naibu Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Zanzibar Omar Ali Shehe amesema kesho Alhamisi Oktoba 23, Othman anamaliza mzunguko wa majimbo akifanya mkutano wa hadhara jimbo la Wete.

“Mgombea wetu (Othman), amefanya kampeni za kistaarabu, kimantiki na zilizoshiba maudhui na kujibu changamoto na hoja ambazo Wazanzibari wanatamani kuzisikia,” amesema Shehe.