Shinyanga. Taharuki yaibuka katika mtaa wa Viwandani kata ya Mjini Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga baada ya kichanga kukutwa katika mfuko wa takataka.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Oktoba 22, 2025 shuhuda wa kwanza wa tukio hilo Jeremia Evance ameeleza kuwa, huwa anapita kutafuta chakula cha kuku kwenye mifuko ya taka, wakati anafukua taka hizo ndio alipokutana na katoto kamewekwa kwenye mfuko,
“Huwa nina tenda ya kulisha kuku Nguzo nane, wakati na pitapita katika mifuko kutafuta chakula nikakuta mfuko ndani ya mfuko wa taka nilipoufungua nikakuta kichanga ndani, nilishtuka nikaenda kuwaita wote wanaokaa katika hosteli hii waje kushuhudia” amesema Evance.

Boski lenye kichanga. Picha na Hellen Mdinda.
Naye mkazi wa mtaa wa Viwandani Stamili Mohammed ameeleza kuwa aliitwa kuja kushuhudia alipofika akakuta kweli ni kichanga kikiwa bado na damu.
“Niliitwa na jirani kuja kushuhudia kichanga kimetupwa nilipofika nikakuta kweli, kwa makadirio kinaweza kuwa cha miezi saba au nane, maana viungo vyake tayari vimekamilika” amesema Stamili.
Aidha, Mwenyekiti wa mtaa wa Viwandani kata ya Mjini Ashrafu Majaliwa ameeleza kushuhudia kwa kichanga hicho ambacho tayari kilikuwa kimetolewa kwenye mfuko wa taka na kuwekwa kwenye boski,

Baadhi ya wananchi wakushuhudia kichanga kilichotupwa.
“Nilipigiwa simu na balozi kuhusu tukio hili maana sikuepo ofisini, nilipofika nimeshuhudia kweli kichanga kimetupwa kwenye mfuko wa taka ambacho hakijajulikana ni jinsia gani huyu ni malaika wa Mungu, nimewapigia polisi na utaratibu wa mtaa wet ugari la taka huwa linapita Jumatano, pengine aliyefanya tukio hili alikuwa amelenga siku ya kubeba taka” amesema Majaliwa.
Hata hivyo jeshi la polisi limefika eneo la tukio na kuchukua mwili wa kichanga kisha kuanza kuchunguzi wa awali kwa wanafunzi wa hosteli hiyo.
Kwa upande mwingine Mwananchi imejaribu kufanya mawasiliano na Kamanda wa Jeshi la polisi lakini hatukufanyikiwa kumpata kuzungumzia tukio hilo.