MKE WA MGOMBEA UBUNGE CHATO KUSINI AMWOMBEA KURA MUMEWE

Kushoto ni mke wa mgombea Ubunge Jimbo la Chato kusini akiwaomba kura wananchi.

……………..

CHATO

MKE wa mgombea Ubunge Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula, amesimama jukwaani kuwaombea kura wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) akiwemo mumewe, Diwani wa kata hiyo pamoja na Samia Suluhu Hassan.

Mbali na hatua hiyo kuwavutia wananchi wengi waliojitokeza kumsikiliza mgombea Ubunge wa Jimbo hilo, pia ameahidi kumshauri vizuri mumewe ili awe mtumishi mwema kwa wananchi wake.

Akiwa amepiga magoti kama ishara ya heshima kwa wananchi, mama huyo ( jina limehifadhiwa) amesema atakuwa tayali kutoa ushauri wenye maslahi mapana kwa umma ili wananchi wa Jimbo la Chato kusini waweze kupata maendeleo ya haraka.

“Ndugu zangu naomba mumpigie kura nyingi mume wangu, kipenzi changu na Baba watoto wangu ili awe Mbunge wa Jimbo hili, ninawaahidi nitakuwa mshauri mwema sana kwa mume wangu ili atimize wajibu wake wa kuwatumikieni wananchi” amesema.

Alikuwa kwenye mkutano wa kampeni za CCM zilizofanyika kwenye Kijiji cha Bwanga kata ya Bwanga wilayani Chato mkoani Geita, huku mgombea huyo akidai kufurahishwa na mwitikio wa wananchi waliojitokeza kumsikiliza.

Kadhalika ameahidi kuupima mji mdogo wa Bwanga ili uwe wa kisasa na kuuongezea thamani kuliko ulivyo hivi sasa.

Amesema atahakikisha anazichonga barabara zote za mitaa kwa kiwango cha changarawe ili zipitike wakati wote baada ya kununua mitambo ya ujenzi wa miundombinu hiyo kupitia pesa za mfuko wa Jimbo.

Vilevile amewaahidi watumishi wa umma kushirikiana nao kwa kutetea maslahi yao ikiwa ni pamoja na kupigania upatikanaji wa watumishi wapya ikiwemo sekta ya afya na elimu kwa kuzingatia matakwa ya Ilani ya CCM ya mwaka 2025/30.

“Katika kipindi changu cha Ubunge nitawataka watumishi wa umma mfanye kazi kwa bidii na baada ya muda wa kazi kuisha mle Bata, nahitaji mfurahie kuwa katika Jimbo hili jipya” amesema Lutandula.

Hata hivyo, aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo na mgombea udiwani wa Kata ya Bwongera Jimbo la Chato Kaskazini, Christian Manunga, amemtaka Lutandula kwenda Bungeni kupigania upatikanaji wa halmashauri mpya ya Bwanga.

Amesema Mji mdogo wa Bwanga na Buseresere zinakidhi vigezo vya kuwa halmashauri mpya kutokana na akidi ya watu kwa kuzingatia sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Aidha amewasihi sana wananchi wa kata ya Bwanga kumpigia kura nyingi Dkt. Samia ili aweze kuwa rais wa Tanzania, kwa kuwa ndiye mwenye mamlaka ya kutoa fedha zote za maendeleo nchini.

                          Mwisho