Arusha. Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude ameutaka Umoja wa Mafundi wa Magari Krokon eneo la Suye Kata ya Kimandolu kuendelea na shughuli zao bila ya kuwa na wasiwasi wa kuondolewa.
Amesema wasiondolewe kwenye eneo hilo ambalo walikabidhiwa na aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Samweli Ndomba.
Akizungumza na mafundi hao leo Jumatano, Oktoba 22,2025 katika mkutano ulioitwa na umoja huo kumwomba afute uamuzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kutaka kulichukua eneo hilo kwa ajili ya kulipangia matumizi mengine.
Mkude amesema upo utaratibu wa kawaida wa Halmashauri ya Jiji kupanga maeneo yake kulingana na mahitaji yaliyopo, lakini amewahakikishia kuwa wataendelea kufanya shughuli zao eneo hilo bila kubughudhiwa.
Wakazi wa Kata ya Kimandolu pamoja na Umoja wa Mafundi Magari Krokon eneo la Suye wakimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Arusha, Joseph Mkude leo. Picha na Filbert Rweyemamu
“Serikali inatambua mchango unaotolewa na sekta binafsi hasa nyie mafundi wa magari ambao mnatumia ujuzi wenu kutatua changamoto za wateja wenu kupitia kazi halali zinazotambuliwa rasmi,Serikali imeweka mazingira mazuri ya ninyi kufanya kazi zenu,”amesema Mkude.
Katibu wa umoja huo, Joram Tarimo amesema walihamia eneo hilo mwaka 2006 kutoka Krokon katikati ya jiji kufuatia uamuzi wa Serikali uliowataka kuhama mara moja.
“Mkuu wa mkoa wa wakati huo, Luteni Jenerali mstaafu, Samwel Ndomba alisema hili eneo tumepewa kwaajili ya kufungua gereji kubwa ambayo itaweza kukidhi mahitaji na kuwaondoa mafundi wote katikati ya mji, tunasikitishwa na uamuzi wa halmashauri ya jiji kutwambia hili eneo ni mali yao na wanataka tuhamie eneo la Oljoro na Nyahiri,”amesema Tarimo.
Amesema wakati wanahamia eneo hilo walikua mafundi 600 lakini kulingana na masharti waliyopewa ya namna ya kujenga kwa ajili ya kuliweka eneo hilo katika mazingira mazuri, wengi walishindwa na sasa wapo 200.
Tarimo ameongeza kuwa wanaamini ni Serikali hiyohiyo iliyowapa hilo eneo hivyo hawapaswi kuondolewa kwa sababu wametumia muda mrefu na rasilimali zao kupaendeleza, na wasingependa kuwapoteza wateja wao na uwekezaji walioufanya.
Amesema kuwa mbali na kuomba kubaki eneo hilo, lina changamoto ya kupitika wakati wa msimu wa mvua na kumwomba Mkude kutumia mamlaka yake ili barabara hiyo ipitike muda wote na kuwawezesha kutimiza malengo yao.
Pia wapate mikopo rafiki ya kuwawezesha kuboresha mazingira ya kazi zao kwa kununua mashine za kisasa na kuongeza nafasi za vijana wenzao.
Akijibu hoja hizo, Mkude amewataka kuunganisha nguvu zao kupitia umoja waliouanzisha ili wapate mikopo kupitia benki, na kuahidi kuwatuma wataalamu wa mikopo ambao watapitia Katiba ya umoja wao ili kufikia malengo yao