Timu ya Taifa ya soka ya Wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ethiopia kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam leo.
Matokeo hayo yanaifanya Twiga Stars ihitaji ushindi au sare ya aina yoyote katika mechi ya marudiano wiki ijayo ili itinge katika fainali hizo ambazo zitafanyika Morocco.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), mechi ya marudiano itachezwa jijini Addis Ababa, Ethiopia, Jumanne ijayo, Oktoba 28.

Mabao ya ushindi ya Twiga Stars katika mchezo wa leo yamefungwa na Aisha Mnunka na Jamila Rajab.
Ikifanikiwa kufuzu, itakuwa ni mara ya tatu kwa Twiga Stars kushiriki WAFCON baada ya kufanya hivyo mwaka 2010 na 2024 ambapo mara zote iliishia hatua ya makundi.
Fainali za WAFCON 2026 ndizo zitatumika kusaka timu nne ambazo zitaiwakilisha Afrika katika Fainali za Kombe la Dunia ambazo zitafanyika Brazil 2027.
Timu hizo ni ambazo zitamaliza katika nafasi nne za juu katika Fainali za WAFCON 2026 ambazo zimepangwa kufanyika kuanzia Machi 17 hadi Aprili Aprili 3, mwakani.