Mwalimu: Kila Mbunge kwenye uongozi wangu lazma awe na msaidizi mtafiti, amkumbuka Sitta

Tabora. Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amesema endapo atachaguliwa kuwa Rais, kila mbunge atahakikisha anakuwa na msaidizi mtafiti atakayemsaidia kuandaa na kujenga hoja zenye mashiko bungeni.

Akizungumza leo, Jumatano Oktoba 22, 2025, katika muendelezo wa kampeni zake mkoani Tabora, Mwalimu alifanya mikutano katika majimbo ya Urambo, Kaliua na Tabora Mjini, ambapo alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuboresha ubora wa mijadala bungeni.

Mwalimu amesema Bunge la sasa limepoteza uzito wake na kugeuka kama sehemu ya vichekesho, kutokana na baadhi ya wabunge kushindwa kuibua hoja makini zinazowakilisha changamoto halisi za wananchi na kusababisha matatizo mengi kukosa ufumbuzi wa msingi.

“Nadhani mnakumbuka Bunge la enzi za marehemu Spika Samuel Sitta; wakati huo wabunge walikuwa na hoja zenye uzito na zenye kuleta tija kwa taifa. Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi.

“Aidha, Bunge la sasa limepoteza mwelekeo, limegeuka kuwa jukwaa la vichekesho. Wabunge wanatetea hoja zisizo na mashiko wala faida kwa wananchi.

“Cha kusikitisha zaidi, wengi wao wamegeuka kuwa wapambe wa kusifia tu uongozi wa juu, jambo ambalo halifai kwa kuwa kutekeleza majukumu ya uongozi si hisani bali ni wajibu,” amesema.

Pia, mgombea huyo wa urais amewataka vijana siku ya Oktoba 29 2025 wanapokwenda kupiga kura wasiende tu kwa kuwa siku imefika, bali waende wakifikiria hatma yao katika upatikanaji wa ajira na hali ya maisha magumu wanayopitia kwa sasa.

“Hatuendi kupiga kura sababu tarehe imefika bali tunataka kuingia mkataba wa miaka mitano na wananchi ya nini tutakachoenda kuwafanyia kwa yule ambaye tutamkabidhi uongozi kwenye kata yetu, kwenye jimbo letu kwenye nchi yetu.

“Msiende kupiga kura kwa mazoe halafu baada ya miezi michache mnaanza kulalamika bei ya tumbaku, unakwenda kumchagua mtu ambaye miaka yote ameshindwa kuwaletea stendi, halafu baada ya miezi michache mnalalamika hakuna ajira, nitawashangaa,” ameeleza mgombea huyo.

Naye mgombea ubunge wa Urambo kupitia Chaumma, Joyce Katobasho amesema, wananchi wa jimbo hilo wamekuwa wakisumbuliwa na mikopo iliyopewa jina la ‘mikopo mwemdakasi’ na ‘shikilia dera’ ambapo sasa imeingia hadi kwa kina baba kwani zamani ilikiwa ni kwa ajili ya  kina mama tu.

“Mikopo hii hapa kwetu imechangja kupunguza nguvu za wanaume, hawana amani na kujikuta nyumbani wanalala vyumba tofauti na wenza wao,” amedai.

Pia, ameeleza kuwa changamoto ya maji bado ni kubwa, licha ya ahadi zilizotolewa tangu mwaka 2020 kuwa maji yangesambazwa kutoka Ziwa Victoria.

Amesema hadi leo wananchi hawajafaidika na mradi huo, hali inayowalazimu baadhi ya wakazi kutafuta maji kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa tatu usiku bila mafanikio ya uhakika.