Wakati teknolojia ikizidi kubadilisha taswira ya maisha katika sekta mbalimbali, kilimo nacho hakijabaki nyuma. Simu za mkononi zimekuwa nyenzo muhimu katika kuinua wakulima wadogo na kuwapa fursa ya kupata taarifa, huduma na masoko kwa urahisi kuliko ilivyokuwa awali.
Kupitia simu, mkulima sasa anaweza kufanya malipo kwa njia za kidijitali, hatua ambayo imepunguza hatari ya kubeba fedha taslimu, lakini pia simu imerahisisha manunuzi ya pembejeo, mbegu bora na huduma za usafirishaji wa mazao.
Malipo haya yameongeza uwazi, usalama na ufuatiliaji wa miamala katika mnyororo wa thamani wa kilimo.
Aidha, simu zimekuwa darasa jipya la wakulima. Kupitia programu mbalimbali, wakulima hupata elimu ya kitaalamu kuhusu kilimo cha zao fulani kutoka hatua ya maandalizi ya shamba, upandaji, matumizi ya mbolea hadi uvunaji na uhifadhi bora wa mazao. Teknolojia hizi zinawawezesha kufanya maamuzi sahihi kulingana na mazingira yao.
Taarifa za hali ya hewa pia zinapatikana kirahisi kupitia simu. Kwa kutumia majukwaa ya taarifa za hali hewa wakulima hupata taarifa sahihi za mvua au ukame, jambo linalosaidia kupanga ratiba ya kilimo na kuepuka hasara kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Huduma za bima nazo zimeingia vijijini kupitia simu. Huduma hizo zinawawezesha wakulima kulipa michango na kupata fidia pale mazao yao yanapoharibiwa na ukame au mafuriko lakini pia bima za afya kwa ajili ya matibabu pale inapotokea. Hatua hii imeongeza uthabiti wa kipato na kuondoa hofu kwa wakulima wadogo.
Faida kubwa zaidi ni upatikanaji wa taarifa za masoko. Kupitia applikesheni na vikundi vya mitandao ya kijamii, wakulima sasa wanajua bei za mazao kwa wakati halisi katika masoko ya ndani na nje ya nchi, hivyo kuepuka unyonyaji wa madalali.
Takwimu za mawasiliano za Mamlaka ya mawasiliano nchini (TCRA) zinaonyesha kuwa idadi ya laini za simu hai zilizopo ilifikia milioni 99.3 kati ya hizo 111,169 zilikuwa zikitumika katika mashine (IOT).
Wakati huo watumiaji wa huduma za miamala ya fedha nao wamekuwa wakiongezeka hadi Septemba mwaka huu akaunti za miamala zilifikia milioni 71.7. Vilevile watumiaji wa huduma za mtandao walifikia milioni 54.1.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas ambayo umiliki wake wa soko la huduma za miamala ya simu nchini ni takriban ya asilimia 30, Angelica Pesha, anasema kupitia mtandao wao wenye kasi ya (4G/5G) huduma za malipo kidijitali na upatikanaji wa taarifa kwa wakulima vijijini zimerahisishwa.
Mixx imekuwa ikifanya uwezeshaji wa wakulima kwa kushirikiana na wadau wengine katika mnyororo wa thamani zikiwemo taasisi za Serikali, vyama vya ushirika, watoa huduma za bima na taasisi za maendeleo kwa kutoa mafunzo ili kuhakikisha wakulima wanatumia huduma hizi ipasavyo.
Anasema akili unde (AI) inaweza kusaidia katika uchambuzi wa data za mavuno, taarifa za hali ya hewa, na upangaji wa rasilimali, na hivyo kuboresha maamuzi ya kilimo huku vifaa vitumiavyo intaneti vikisaidia kufuatilia hali joto, unyevu wa udongo au mifumo ya umwagiliaji kwa ufanisi zaidi.
“Licha ya kuwa Mixx imeleta suluhu za kifedha na afya (kupitia Kilimo Pesa na Afya Mkulima) bado tunaona fursa kubwa ya kuunganishwa kwa teknolojia hizi katika hatua zinazofuata ili kuongeza tija kwa wakulima hivyo tunaendelea kubuni zaidi,” anasema Pesha .
Anaongeza kuwa wakulima wanapopokea malipo kwa njia ya simu, jambo hili huwatengenezea rekodi ya kifedha ambayo inasaidia kwenye tathimini ya uwezo wao kukopesheka na kulipa (credit score) hivyo wanaweza kupata huduma nyingi zaidi kutoka kwa watoa huduma za kifedha.
“Kupitia huduma za Mixx wakulima hupokea malipo yao haraka na kwa usalama bila hitaji la nyaraka nyingi. Upekee ni katika namna tunavyowaleta wakulima karibu na suluhu za kifedha, zinazozingatia na kukidhi mahitaji yao halisi,” anasema.
Anaongeza kuwa huduma zao hutoa mikopo ya kifedha kupitia Kilimo Pesa ili wakulima wawe na mtiririko wa fedha wa kufanya kazi bila wasiwasi sambamba na kuratibu programu za bima ya afya kupitia huduma ya Afya Mkulima ili kulinda ustawi wa kaya za wakulima.
“Afya Mkulima inalenga kuondoa wasiwasi kwa kuwapa wakulima uwezo wa kukabiliana na gharama za tiba na hatari kwa njia iliyo ya kweli na matumizi ya taarifa za ufuatiliaji na taratibu za malipo zimerahisishwa, ili wakulima wapate msaada bila kuchelewa”
Hata hivyo Pesha anasisitiza kuwa Mixx ni mshirika wa kifedha sio tu kwa wakulima bali kwa watanzania kwani wanawasaidia kufikia malengo yao ya kifedha na kibiashara kwa urahisi na usalama.
Mhadhiri wa Uchumi katika Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), Dk Eliaza Mkuna anasema kwa miaka mingi, kilimo cha Tanzania kilitegemea mbinu za zamani na upatikanaji wa mvua. Lakini sasa, hali hiyo imepata mkombozi mkubwa kutoka kwenye vifaa vya kisasa teknolojia ya dijitali.
Dk Mkuna aliunga mkono hoja za Pesha akisema kupitia simu janja na mtandao, eneo la kilimo nchini limepata mabadiliko makubwa, yakiwapa wakulima silaha za kuongeza tija na kufanya maamuzi yenye msingi.
“Matumizi ya simu za mkononi yamemfanya mkulima kuwa na maarifa mkononi mwake. Kupitia programu maalum za kilimo na huduma za USSD, wakulima wanapata taarifa muhimu kwa wakati husika. Wanajua hali ya hewa halisi, bei za soko la mazao tofauti, na hata kupata maelekezo ya kupambana na magonjwa ya mimea,” anasema Dk Mkuna.
DK Mkuna ambaye ni mtaalamu wa kilimo uchumi anasema tekinolojia ya simu inawaokoa dhidi ya hasara za muda fupi na muda mrefu. Zaidi ya hayo, mfumo wa malipo kwa simu, umerahisisha biashara kwa kuwapa wakulima njia salama na ya haraka ya kupokea na kulipa deni, hata kwenye maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma za kibenki.
“Teknolojia pia inawapa wakulima nafasi ya kufikia soko lenye uwazi zaidi. Mitandao ya kijamii na maduka mtandaoni inawawezesha kuwasiliana moja kwa moja na wateja hivyo kupata bei nzuri zaidi kwa juhudi zao. Ushirikiano wa vikundi vya wakulima kupitia mitandao ya kijamii pia umeongeza nguvu yao ya ushindani,” anasema Dk Mkuna.
Anasisitiza kuwa teknolojia mfano simu na intaneti sio tena kitu cha anasa kwa wakulima, bali ni zana muhimu kama jembe na panga. Inawasaidia kufanya kilimo kisayansi, kuokoa wakati na gharama, na hatimaye kuwaongezea kipato.
“Ili kuendelea kukiuka changamoto za ukulima, ni muhimu zaidi serikali na wadau kuhakikisha kuwa huduma hizi za kidijitali zinafika kwa kila mkulima, hata katika vijijini vilivyo na mtandao dhaifu. Maendeleo ya taifa yanaanza shambani, na teknolojia ndio dereva wa maendeleo hayo,” anasema Dk. Mkuna.
Utafiti uliofanywa na taasisi ya Kilimo Kwanza na kuchapishwa Desemba 2024, unaonyesha matumaini makubwa katika sekta ya kilimo kutokana na neema ya maendeleo ya teknolojia ya dijitali.
Kulingana na Ripoti ya Hali ya Kilimo Afrika 2023, teknolojia za kidijitali zitakuwa na nafasi muhimu katika kupambana na upungufu wa ufanisi, ubaguzi, na ukosefu wa endelevu katika sekta ya kilimo.
“Matumizi ya teknolojia za kidijitali yanatarajiwa kubadilisha kilimo na maisha ya wakulima wadogo. Simu za mkononi, redio, kompyuta, ndege zisizo na rubani (drones), satelaiti, akili unde, cloud computing, na data kubwa (big data) vinaingizwa zaidi katika mifumo ya kilimo barani Afrika,” ilieleza sehemu ya ripoti ya utafiti huo.
Teknolojia hizi zinaelekezwa katika kuunda huduma bunifu zinazoweza kuboresha nyanja mbalimbali za kilimo, kuanzia maandalizi ya shamba, usimamizi wa mazao, hadi uvunaji na uuzaji.
Ulimwengu wa kidijitali unatoa ubunifu na maendeleo mapya yanayomwezesha bara la Afrika kuwa mstari wa mbele na kufanikisha kwa ufanisi na kwa njia endelevu uwezo kamili wa wakulima wadogo na sekta ya biashara za kilimo.
Kupata simu za mkononi kwa wingi, hasa kwa wakulima wanawake, kunaweza kuwa na athari kubwa katika uzalishaji wa kilimo na usalama wa chakula. Kuondoa pengo la kijinsia katika umiliki wa simu na upatikanaji wa intaneti kunaweza kuongeza uzalishaji wa kilimo hadi asilimia 4 na kupunguza idadi ya watu wakumbwa na njaa barani Afrika kwa asilimia 17.
Ili kufanikisha uwezo kamili wa kilimo kidijitali, serikali, wafadhili, na mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kuunga mkono utafiti na maendeleo ya kilimo, kuhimiza utumaji wa teknolojia nafuu, na kupanua wigo wa huduma za TEHAMA katika maeneo ya vijijini.
Programu za kukuza ujuzi wa kidijitali pia ni muhimu kushughulikia kiwango kidogo cha uelewa wa kidijitali, hasa miongoni mwa wanawake, vijana, na jamii za vijijini.
Zaidi ya hayo, suluhisho za mafanikio katika kilimo kidijitali zinapaswa kuhusisha wakulima katika mchakato wa kubuni, zikizingatia mahitaji yao halisi, na kuhakikisha mtiririko wa taarifa unaenda pande zote mbili. Serikali pia zinapaswa kuunda na kutekeleza sera zinazounga mkono mahitaji yanayobadilika ya enzi ya kidijitali.
Kwa mujibu wa ripoti ya utafiti wa dijitali katika mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo nchini Tanzania ya mwaka 2025 ya Taasisi ya Utafiti wa Sera za Chakula (IFPRI), kidijitali sasa ni injini muhimu katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.
Mtafiti wa ripoti hiyo, Judith Valerian, Mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika kilimo biashara Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) anasema Tanzania inashuhudia mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo kupitia teknolojia za kidijitali, hatua inayochochea tija, uwazi wa biashara na ujumuishi wa kifedha kwa wakulima wadogo.
Ripoti yake inaonyesha mazao ya kahawa, korosho, mahindi, mpunga, na ufugaji wa kuku ndiyo yenye mafanikio makubwa katika matumizi ya teknolojia. Kupitia majukwaa kama Tanzania Mercantile Exchange (TMX), ATMIS, na M-Kilimo, wakulima wamepata fursa ya kufuatilia bei za mazao sokoni kwa muda halisi, kuimarisha uuzaji wa mazao, na kujua masoko yenye bei bora zaidi.
Kwa upande wa malipo, huduma za miamala ya simu zimebadilisha kabisa namna wakulima wanavyopokea mapato na kulipa gharama za uzalishaji. Wakulima sasa wanaweza kulipwa moja kwa moja kupitia simu zao, kujiwekea akiba, kupata mikopo midogomidogo, na kulipia bima ya kilimo bila kusafiri mbali.