HALMASHAURI YA MERU YATOA MIL.385 KWA VIJANA NA WANAWAKE.

Na Ashura Mohamed -Arusha

Halmashauri ya wilaya ya Meru mkoani arusha imetoa mikopo ya asilimia kumi yenye Jumla ya shilingi milioni mia tatu themanini na tano na laki nane(385,800,000/=,) kwa vijana wanawake na watu wenye Ulemavu.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika katika halmashauri ya Meru  Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Mheshimiwa Mwinyi Ahmed Mwiyi  aliipongeza halmashauri hiyo kwa kuweza kutimiza takwa la serikali ya kuwawezesha watanzania kupitia mikopo hiyo.

Mh.Mwinyi alisema kuwa utoaji wa mikopo hiyo ya asilimia kumi ni adhma  ya Serikali kuyawezesha Makundi hayo ambapo wananchi wataweza kujiongezea kipato na kukua kiuchumi.

“Niwapomgeze sana halmashauri ya Meru hususani dada yangu Afisa Maendeleo  bi.Flora Msilu na  Mkurugenzi Mtendaji Mwl. Zainabu J. Makwinya kwa kuhakikisha fedha za asilimia 10 za mapato ya ndani zinatengwa kwa ajili ya Vikundi,mmetumiza Azma ya Serikali ya kuwezesha wananchi kiuchumi na pia vikundi vya vijana hamjaviacha nyuma niombe muendelee kuvilea vema msiwaache wenyewe mvifuatilie na muwasaidie wakue zaidi ya hapo.”Alisema Mh.Mwinyi

Pia aliongeza kuwa fedha hizo za serikali sio  mwiba kwa wananchi hivyo pindi ambapo watayumba kibiashara  halmashauri iangalie namna ya kuwasaidia badala ya kuwakomoa watakapokosa marejesho kwa kuwa hawana vyanzo vingine vya mapato zaidi ya biashara amabazo watafungua.

“Niwaombe sana hizi fedha zisiwe mwiba kwa hawa wananchi  tunafahamu fika biashara zina kuyumba na kusimama sasa zikiyumba msiwakomoe hawa wananchi bali wasaidieni hatua kwa hatua ili kuhakikisha wanafikia malengo wanakua kiuchumi na serialised inapata fedha hizi bila kuumizana”Alisisitiza Mkuu wa wilaya 

Kwa Upande wake  Mkurugenzi Mtendaji Mwl.Zainab  Makwinya alimtoa hofu mkuu wa wilaya kwa kueleza kuwa  Halmashauri ya Meru imekuwa kinara wa kuvilea vikundi hivyo na kuwapatia fursa ya kufanya biashara na halmashauri pindi zinapojitokeza fursa ili wasikose marejesho.

“Halmashauri yetu imekuwa ikihakikisha hivi vikundi vinavyopewa mikopo vinapewa kipaumbele katika  shughuli mbalimbali za Halmashauri ambazo zinaweza kufanywa au kuhudumiwa na vikundi hivyo,kama hapa huu mziki ni wa kikundi tukihitaji usafiri tunatafuta kikundi cheese usafiri lengo ni kuwawezesha kiuchumi ili wasikwame kurejesha na wamekuwa wakifanya vizuri sana na hata ambao wanafuga ikifikia ng’ombe au mbuzi anafaa kuingia sokoni wasisite hapa huwa tuna shughuli nyingi sana na hawa ni wananchi wetu waje tu”Alifafanua mwl.Makwinya

Alisisitiza kuwa vikundi vilivyopatiwa mikopo ni 26 ambapo vikundi 14 ni vijana na vikundi 12 ni wanawake ambapo milioni mia moja hazijakopeshwa kutokanaa na kundi la wenye ulemavu kutokupatikana ambao jitihada zinafanywa ili fedha hizo zitumike kama ambavyo serikali  imekuwa ikielekeza.

Mwenyekiti wa kikundi cha WALIALANGA , Ndg. Zawadi Emmanuel Chirimo kwa niaba ya Vikundi vyote ametoa shukrani kwa Serikali ya Awamu Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Meru kwa kuwawezesha kupata Mitaji ambapo alisema kuwa atajihushisha na shughuli za Ufugaji wa kuku wa kisasa na Nyama ili awezs kujikwamua kiuchumi.

Nae bi.Mary Mongi ambaye amewakilisha kundi la wanawake alisema kuwa mikopo hiyo itawawezesha kukua kiuchumi kutunza familia  na kujiletea maendeleo hivyo watakuwa waaminifu katika kurejesha fedha hizo huku akiwatoa hofu wanawake kutumia fursa hiyo kukua kiuchumi.

Jumla ya Vikundi 76 viliomba mikopo ambapo vikundi 26 ndio vikundi ambavyo vimeweza kupatiwa mikopo hiyo ya asilimia kumi huku zoezi hilo likitanguliwa na mafunzo maalum ya kuwawezesha wanavikundi kufanya biashara zao kwa ufanisi mkubwa ili kukua kiuchumi,kuweka akiba fedha katika taasisi mbalimbali za kibenki na kukataa rushwa.

Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo bi.Flora Msilu akizungumza na wanachi wakati wa zoezi hilo la utoaji mikopo.

Mkurugenzi wa halmashauri ya Meru mwl.Zainab Makwinya akizungumza na Wanavikundi ambao walijitokeza wakati wa zoezi la Utoaji Mikopo