TRC yasitisha safari za SGR kwa muda

Dodoma. Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema hakuna treni itakayoruhusiwa kuanza safari kwa sasa, mpaka pale watakapotoa taarifa mpya.

Hatua hiyo imefuata baada ya treni ya Electric Multiple Unit – EMU maarufu treni ya mchongoko iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Dodoma leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 kupata ajali katika kituo cha Ruvu mkoani Pwani.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Fredy Mwanjala amesema kwa sasa bado wanasubiriwa mafundi ili waweze kutoa taarifa mpya.

“Tupo eneo la tukio tunawasubiri mafundi ili waseme tatizo liko kwa kiasi gani, sababu hii ni ajali kama ajali zingine zinavyotokea.

“Hivyo mpaka sasa hakuna treni iliyoruhusiwa kuanza safari mpaka pale mafundi watakapotoa taarifa mpya. Muda rasmi wa kuanza safari hatujajua maana mafundi bado hawajatoa taarifa yoyote mpya,” amesema Mwanjala.

Awali taarifa iliyotolewa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa umma ilitaja chanzo cha awali cha ajali hiyo huku ikieleza jitihada zinazofanyika sasa kuhakikisha huduma zinarejea.

“Shirika la Reli Tanzania (TRC) linautaarifu umma kuhusu ajali ya treni ya EMU iliyokuwa ikisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma majira ya saa 2:00 asubuhi Oktoba 23, 2025 kutokana na hitilafu za kiuendeshaji, tukio hili limetokea kituo cha Ruvu na kwa taarifa za awali hakuna kifo.

“Timu ya wataalamu ikiongozwa na Katibu Mkuu Uchukuzi, Mkurugenzi Mkuu TRC, vyombo vya ulinzi na usalama na menejimenti ya TRC inaendelea na uchunguzi wa kina na juhudi za kuhakikisha kwamba huduma zetu zinarejea haraka,” ilieleza taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa.

Treni ya mchongoko, ambayo imekuwa ikifanya safari zake kutoka Dar es Salaam, Morogoro hadi Dodoma ilianza kutoa huduma Novemba Mosi, mwaka 2024.