Dar es Salaam. Mtandao wa WhatsApp uko mbioni kuanza kutumia jina la kipekee la mtumiaji (username) badala ya namba yake ya simu kama ilivyo sasa, ingawa matumizi ya namba ya simu, pia, yataendelea.
Mtandao huo maarufu duniani wenye zaidi watumiaji bilioni tatu katika zaidi ya nchi 180, unatumika kuwasiliana na marafiki na familia, wakati wowote na mahali popote. WhatsApp inatoa huduma kama kupiga simu na kutuma ujumbe kote ulimwenguni.
Kwa tafsiri hiyo, kipengele hicho kipya kitawawezesha watumiaji kuwasiliana bila kuwa na namba za simu, bali kutafuta jina la kipekee ambapo kwa mujibu wa tovuti za teknolojia, matumizi hayo yataanza mapema mwaka 2026.
Kwa mujibu wa mtandao maarufu wa taarifa za WhatsApp wa WABetaInfo, kwa sasa WhatsApp imeanza kufanya kazi kwenye kipengele kipya kinachoitwa ‘Username Reservation’ yaani, mfumo wa kuhifadhi jina la mtumiaji mapema kabla ya kipengele hicho kuzinduliwa rasmi kwa watumiaji wote.
Lengo kuu ni kurahisisha mchakato wa kuandika jina la kipekee kabla halijachukuliwa na mtu mwingine.
Pia, matumizi ya namba hayatasitishwa, bali imetajwa kama njia ya kuongeza faragha na kupanua mawasiliano zaidi. Kwa sasa kampuni hiyo iko katika majaribio ya Android na iOS.
Imeelezwa kipengele cha ‘username’ kimekuwa kikisubiriwa kwa muda mrefu na watumiaji wanaolinganisha na mitandao mingine inayotumia kipengele hicho kama Telegram.
Ikumbukwe kwa sasa watumiaji wa WhatsApp mtandao unaomilikiwa na kampuni ya Meta bado unahitaji mtumiaji kuingia kwa kutumia namba ya simu, badala ya jina la mtumiaji na nywila lakini hilo litabadilika hivi karibuni.
Kwa mujibu wa WABetaInfo ambayo hufuatilia vipengele vipya vya majaribio vya WhatsApp, toleo la majaribio la WhatsApp (version 25.17.10.70) linaonyesha kampuni hiyo inafanya kazi ya kuongeza uwezo wa kutumia majina ya watumiaji, ingawa bado halijaanza kupatikana kwa watumiaji wote.
Watumiaji watapata sehemu ya ‘Username’ kwenye ukurasa wa wasifu wao mara kipengele kitakapopatikana. Watatengeneza jina la mtumiaji kulingana na mapendekezo yao, lakini majina hayataruhusiwa kuwa na viambishi vya tovuti kama “.com” na lazima yawe na angalau herufi moja.
Watumiaji watapewa nafasi ya kuandika jina lenye mchanganyiko wa herufi na namba. Hata hivyo, haitaruhusiwa kutumia alama (isipokuwa nukta “.” na mstari wa chini “_”).
Kwa sababu za kiusalama, majina ya watumiaji hayataruhusiwa kuanza na “www.” au kumalizika na viambishi kama “.com”, ili kuepuka udanganyifu wa watumiaji wanaoweza kujifanya kuwa tovuti fulani. Pia, majina ambayo tayari yametumika hayatapatikana tena.
Wakati mtumiaji atabadilisha jina lake, marafiki au watu aliokuwa akizungumza nao watapokea ujumbe wa mfumo (system message), ukionyesha kuwa jina hilo limebadilishwa.
Kwa kifupi, kipengele hiki kipya kitawawezesha watumiaji kuficha namba zao za simu na kuwasiliana kwa kutumia majina hatua kubwa katika kulinda faragha kwenye WhatsApp.
Ili kuongeza usalama, WhatsApp pia inapanga kuanzisha ‘username key’ ambayo itakuwa neno la siri au msimbo mfupi.
Kwa kutumia mfumo huu, mtu asiyejulikana hataweza kukutumia ujumbe hadi awe na msimbo sahihi unaohusiana na jina lako la mtumiaji.
Hii inamaanisha watumiaji wataweza kudhibiti zaidi nani anaweza kuwasiliana nao, na hivyo kupunguza uwezekano wa ulaghai (scams) na ujumbe wa kiholela (spam) kutoka kwa watu wasiojulikana.
Kwa ujumla, WhatsApp inajitayarisha kuingia katika enzi mpya ya mawasiliano salama zaidi, ambapo namba ya simu haitakuwa muhimu tena hatua ambayo inaweza kubadilisha kabisa jinsi watu wanavyotumia programu hiyo duniani kote.
Kuhusu faida; kwanza ni kuongeza faragha ya mtumiaji. Mfumo wa usernames utakuwezesha kushiriki taarifa zako za mawasiliano na watu au biashara bila kufichua namba yako ya simu. Wale ambao hawana namba yako watahifadhiwa wataona jina lako la mtumiaji tu.
Vilevile namba yako ya simu bado itatumiwa kwa usajili na uthibitisho wa akaunti. Jina la mtumiaji litatumika kama kitambulisho cha ziada, kinachozingatia faragha. Watumiaji watakuwa na chaguo la kuficha namba yao ya simu kwa wengine kabisa ama la.