Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeikataa ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa picha mjongeo (video clip) ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, anayekabiliwa na kesi ya uhaini, yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini.
Upande wa mashtaka katika kesi hiyo jana Jumatano, Oktoba 22, 2025 kupitia shahidi wake wa tatu iliiomba mahakama iipokee ripoti hiyo kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Hata hivyo, Lissu ambaye anajitetea mwenyewe, aliweka pingamizi dhidi ya ripoti hiyo akitaka isipokelewe kwa kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kisheria kuiandaa wala kuiwasilisha mahakamani ripoti hiyo, kwa kuwa si mtaalamu wa uhalifu wa kimtandao.
Licha ya upande wa mashtaka kupinga hoja za Lissu kuwa hazina mashiko kisheria, mahakama katika uamuzi wake leo Alhamisi Oktoba 23, imekubaliana na pingamizi hilo baada ya kuridhika na hoja za mshtakiwa, hivyo ikakataa kuipokea ripoti hiyo.
Hili ni pingamizi la pili la Lissu kukubaliwa na mahakama hiyo, baada ya jana mshtakiwa huyo kufanikiwa kuzuia flash na memory card zenye video inayodaiwa kumuonyesha akitamka maneno ya uchochezi, kwa sababu shahidi wa Jamhuri, Samweli Eribariki Kaaya, aliyeomba kuviwasilisha, hana mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
Lissu alipinga vielelezo hivyo visipokewe kwa hoja kwamba shahidi huyo si mtaalamu aliyeteuliwa na mamlaka husika na kutangazwa katika Gazeti la Serikali, kama inavyotakiwa chini ya kifungu cha 216(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Toleo la Marejeo la mwaka 2023.
Aidha, alieleza kuwa shahidi huyo ameteuliwa kama mtaalamu wa picha za mnato pekee, na si mtaalamu wa picha jongefu (video). Kwa kuwa vielelezo vinavyokusudiwa kuwasilishwa ni picha jongefu, basi hana mamlaka ya kisheria kuviwasilisha mahakamani.
Katika kesi hiyo namba 19605 ya mwaka 2025, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonyesha nia hiyo kwa kuchapisha meneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inayosikilizwa na na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde iko katika hatua ya ushahidi wa mashtaka, Kaaya akiwa shahidi wa tatu.
Shahidi huyo, mtaalamu wa picha, kutoka Kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake wa msingi, Kaaya alieleza kuwa Aprili 8, 2025 alipokea ‘flash disk’ na ‘memory card’ zenye video ya Lissu, yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Dar es Salaam kuchunguza uhalisia wake.
Shahidi huyo aliieleza Mahakama kuwa katika uchunguzi wake alibaini kuwa video hiyo ni halisi na haina pandikizi, kisha akaandaa ripoti ya uchunguzi huo.
Oktoba 17, 2025 aliiomba mahakama hiyo ivipokee vihifadhi data hivyo (flash disk na memory card zenye video ya Lissu, lakini Lissu aliviwekea pingamizi na mahakama katika uamuzi wake jana Jumatano ilikubaliana naye.
Baada ya uamuzi huo upande wa Jamhuri uliendelea na shahidi hiyo na ukaomba ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa video hiyo, alioufanya shahidi huyo ipokelewe na mahakama na kuwa kielelezo cha ushahidi wa Jamhuri, lakini pia Lissu akaiponga.
Lissu alidai shahidi huyo kwa ushahidi wake mwenyewe aliieleza mahakama kuwa ni mtaalamu wa picha za mnato chini ya kifungu cha 202(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA) Marejeo ya mwaka 2022.
Lissu alidai kuwa kifungu hicho ambacho kwa sasa baada ya marejeo ya mwaka 2023, ya Sheria hiyo ni kifungu cha 216(1), kinahusu mchunguzi kuandaa hati zinazowasilishwa mahakamani na watalaamu wa picha mnato na si ripoti.
Alifafanua kuwa ripoti inaandaliwa na kutolewa na mtaalamu wa uchunguzi wa uhalifu wa kimtandao na kufafanua kwamba picha jongefu ni tofauti na picha mnato.
“Waheshimiwa majaji, wino haujakauka tangu mmetoa uamuzi kuhusiana na vielelezo vilivyokataliwa, na mkaeleza kuwa huyu shahidi ni shahidi wa picha mnato na sio mtaalamu wa picha mjongeo video.
“Kwenye kielelezo hiki, huyu shahidi amesema kwamba aliteuliwa na kuthibitishwa na kutangazwa katika Tangazo la Serikali Namba 799 la mwaka 2020 na tangazo la Serikali hilo lilitolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali( AG) na sio Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) kama sheria inavyotaka” alidai Lissu.
Alidai kuwa kutokana na kuteuliwa na AG badala ya DPP, uteuzi wa shahidi haukuwa halali na hivyo hafai kutoa ripoti hiyo mahakamani.
“Kimoja kikikataliwa kingine hakiwezi kusimama chenyewe na kusimama kwake kunategenea kusimama, akimaanisha kuwa baada ya mahakama kukataa ‘flash disk’ na memory card, ripoti ya uchunguzi wake haiwezi kusimama.
Hivyo alisisitiza kuwa taarifa hiyo ya uchunguzi haijazingatia masharti ya kifungu 216 na hivyo haiwezi kuwasilishwa na kupokewa mahakamani.
Baada ya Lissu kueleza hayo, Wakili wa Serikali Mkuu, Job Mrema iliiomba mahamama hiyo itupilie mbali pingamizi la Lissu na mahakama ipokee taarifa hiyo ya shahidi ambaye ni mtaalamu wa picha.
Mrema alidai kuwa ripoti ya uchunguzi ni tofauti na vielelezo vilivyokataliwa na mahakama – flash disk na memory card, hivyo aliomba mahakama ipokee ripoti hiyo kwani shahidi ana sifa za kuiwasilisha mahakamani hapo.
Mahakama katika uamuzi wake uliosomwa na Jaji Karayemaha imekubaliana na pingamizi la Lissu kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kuandaa ripoti ya uchunguzi huo wala kuiwasilisha mahakamani, kwa kuwa ni mtaalamu wa picha za mnato na si wa video.
Jaji Karayemaha amesema kuwa kuwa shahidi huyo kwa kuwa ni mtaalamu wa picha za mnato, basi alipaswa kuaanda hati (certificate) na si ripoti.
“Ni wazi yeye shahidi aliteuliwa kushughulikia picha za mnato na mwishoni anapaswa kuandaa (hati) certificate,” amesema Jaji Karayemaha.
Amesema kwa kuwa sheria iko wazi na wao hawatakubali kuingia kwenye mtego wa kukiuka sheria na kwamba hata kama hiyo ripoti ingekuwa imeandaliwa kwa mujibu wa sheria (kuambatanishwa na hati), kwa kuwa flash na memory card zenye video iliyofanyiwa uchunguzi vimekataliwa, basi hata ripoti yenyewe isingekuwa na maana.
“Kwa hiyo tunakubali huyu shahidi hana uwezo wa kutoa hiyo ripoti isipokuwa certificate chini ya kifungu cha 216(1) cha CPA. Tunaona pingamizi la mshtakiwa lina mashiko na sisi hatutaipokea hiyo taarifa aliyotaka kuitoa shahidi,” amesema Jaji Karayemaha.
Baada ya hatua hiyo, upande wa Jamhuri umefunga ushahidi wa Kaaya na Lissu akaendelea kumuuliza maswali ya dodoso kuhusu ushahidi wake wa msingi.