Wanawake wahamasishwa kupiga kura | Mwananchi

Dar es Salaam. Muunganiko wa asasi za wanawake umewahimiza wanawake nchini kujitokeza kupigakura Oktoba 29 mwaka huu, kwa kuwa ni wajibu wa Kikatiba unaotoa fursa ya kuchagua viongozi watakaosimamia masilahi yao.

Kupitia tamko kwa vyombo vya habari asasi hizo zimeitaka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na vyama vya siasa kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanabaki salama, huru na jumuishi, bila vitisho, ukatili au udhalilishaji wa kijinsia.

Kwa mujibu wa INEC, Watanzania 37,647,235 watapiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani kati yao wanawake ni 18,950,801, sawa na asilimia 50.34.

Akiwasilisha tamko hilo leo Alhamisi Oktoba 23, 2025 mwanahabari mkongwe na mwanachama wa Chama cha Wanahabari Wanawake (Tamwa),  Rose Mwalimu amesema ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi ni moja ya nguzo muhimu za maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Rose amesema uwepo wa viongozi wanawake unasaidia kuibua sera zinazogusa maisha ya wanawake na familia kwa jumla, hivyo kundi hilo lina kila sababu la kuhakikisha linashiriki kwenye mchakato wa upatikanaji wa viongozi.

“Tunapokwenda kuwachagua viongozi wetu, tuwatwike mzigo wa mambo ya msingi yanayowahusu wanawake, watoto na makundi maalumu.Tanzania ni yetu sote, wanawake na wanaume tunapaswa kushiriki kwa usawa katika kuijenga,” amesema Rose.

Rose amesema uchaguzi wa mwaka huu unaendelea kuiweka Tanzania kwenye nchi za Bara la Afrika zilizopiga hatua kubwa katika ushiriki wa wanawake katika siasa, wanawake watatu wanagombea urais na wengine wanane wakigombea wenza.

Wagombea hao ni Samia Suluhu Hassan kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Saumu Rashid (The United Democratic Part- UDP) na Mwajuma Mirambo ( Chama cha Union Multiparty Democracy -UMD) katika nafasi ya urais huku Eveline Wilbard Munis (NCCR – Magueuzi), Husna Mohamed Abdallah, Chama cha Wananchi (CUF) na Devotha Minja (Chama cha Ukombozi wa Umma -Chaumma) wakiwa wagombea wenza.

“Hatua hii ni ishara ya ukuaji wa demokrasia jumuishi na uthibitisho kuwa uongozi wa mwanamke si tishio, bali ni fursa ya maendeleo ya Taifa.Tunaamini kuwa, pale wanawake wanapopewa nafasi ya kuongoza, jamii hunufaika zaidi kupitia sera za elimu, afya na usawa wa kiuchumi,” amesema

Mkurugenzi wa Taasisi ya Wajiki, Janet Mawinza ameeleza kuwa ni vyema jamii ikajiweka mbali na matumizi ya lugha za kudhalilisha au kejeli dhidi ya wagombea wanawake badala yake zisikilizwe hoja na sera zao.

Janeth ameeleza kuwa, uongozi bora hauna jinsia, bali unaongozwa na maadili, dira na dhamira ya dhati ya kuwatumikia wananchi.

“Wanawake wanaowania nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya udiwani hadi urais wasibezwe. Tunakemea vikali lugha dhalili zinazotweza utu wao, tuzingatie hoja, sera na dira za maendeleo badala ya mashambulizi ya kijinsia.”

Amesema kupatikana kwa Rais mwanamke kumechangia mageuzi makubwa, ikiwamo kubadilishwa kwa sheria za kisiasa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika sekta ya afya na elimu, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG 5) kuhusu usawa wa kijinsia.