KOCHA Msaidizi wa Malindi, Mohamed Salah ‘Richkard’ ameanza kujipa matumaini wakati kikosi hicho kikishikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar.
Malindi iliyocheza mechi tano, imeshinda tatu na sare mbili, haijapoteza huku ikifunga mabao manane na kuruhusu moja ikikusanya pointi 11.
Richkard amesema bado hawajafikia wanachohitaji kwani lengo lao ni kuwa juu ya msimamo wa ligi hiyo na ndiyo sababu ya kujipanga kila mechi kuvuna alama tatu.
Alieleza, mipango mingine kwake ni kuona kila mechi kipa wa timu hiyo anapata cleansheet.
“Nimerudi nyumbani kufunza na kutoa hamasa ya mpira, mashabiki na wadau wa soka wafike uwanjani kushuhudia burudani inayotolewa na Richkard,” amesema.

Oktoba 21, 2025, Malindi ilipata alama moja dakika za mwishoni katika sare ya 1-1 dhidi ya JKU.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja, James Ambros aliitangulizia JKU akifunga bao dakika ya 22, kabla ya Malindi kusawazisha dakika ya 90+3 kupitia Shafii Omar.
Bao hilo la kusawazisha liliibua shangwe uwanjani hapo kwa mashabiki, wachezaji na benchi la ufundi huku wakiweka vidole mdomoni wakimaanisha kuwafunga midomo wapinzani.
Kuhusu mfungaji wa bao hilo, Richkard amesema Shafii amefanya kazi kubwa kuhakikisha timu hiyo haitoki uwanjani na vilio huku akimpongeza kwa kutumia uwezo binafsi na kuikoa na kipigo.

Kabla ya mechi za jana Alhamisi, Malindi ni miongoni mwa timu nne ambazo hazijapoteza mechi katika Ligi Kuu Zanzibar msimu huu. Zingine ni Uhamiaji, KVZ, JKU na Mlandege.