Droo ya makundi CAF kuchezeshwa Novemba 3

Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), limetangaza Novemba 3, 2025, itachezeshwa droo ya upangaji wa makundi kwa msimu wa 2025-2026 katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho.

Droo hiyo imepangwa kufanyika Johannesburg nchini Afrika Kusini ambapo ile ya Kombe la Shirikisho itaanza saa 8 mchana, wakati Ligi ya Mabingwa ikiwa saa 9 alasiri kwa saa za Afrika Mashariki.

Wakati ratiba ya droo hiyo ikipangwa, wikiendi hii kuna mechi za marudiano zinachezwa ambapo washindi wa jumla ndiyo watafuzu makundi wakisubiri wapinzani wao wapya.

Katika upangaji wa droo hiyo, CAF itaangalia Viwango vya Klabu vya CAF kwa mwaka 2025 ili kupanga timu kwenye vyungu (pots).
Kwa sasa, Al Ahly ya Misri inaongoza kwenye orodha ya viwango vya klabu vya CAF kwa mwaka 2025, ikiwa na alama 78, wakithibitisha hadhi yao kama klabu yenye mafanikio makubwa zaidi barani Afrika kihistoria na kimafanikio ya hivi karibuni, baada ya kutwaa taji la CAF Champions League mara nne katika misimu sita iliyopita.

CA 01

Katika viwango hivyo, Simba ni ya tano ikikusanya alama 48, ambayo ni timu yenye nafasi ya juu zaidi kutoka Afrika Mashariki, wakati Yanga ni ya 12 na alama 34 sawa na Al Hilal SC ya Sudan.

Timu nyingine ya Tanzania iliyopo kwenye listi hiyo ya viwango ni Namungo FC yenye alama 0.5 ikishika nafasi ya 77. Ingawa Namungo msimu huu haishiriki mashindano ya CAF, imefika hapo kufuatia kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2020–2021.

Azam na Singida Black Stars hazipo kwenye viwango hivi kutokana na kutokuwa na rekodi nzuri kwenye mashindano ya CAF, lakini zinaweza kuungana na Namungo endapo zitafuzu makundi msimu huu.

Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini yenye alama 62, inashika nafasi ya pili, kisha Espérance Sportive de Tunis iliyokusanya alama 57 ikishika nafasi ya tatu.

RS Berkane ya Morocco (alama 52) ambayo ni bingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, inakamata nafasi ya nne.

Nguvu ya Misri inaendelea kudhihirika kupitia Pyramids FC (nafasi ya 6, alama 47) na Zamalek SC (nafasi ya 7, alama 42), wakati Morocco inawakilishwa na Wydad AC (nafasi ya 8, alama 39) na Raja CA (nafasi ya 15, alama 30).

CA 02

Kutoka Algeria, USM Alger (nafasi ya 9, alama 37) na CR Belouizdad (nafasi ya 10, alama 36) wanaongoza kwa nchi yao.

Baadhi ya klabu zimeonyesha maendeleo makubwa katika miaka ya hivi karibuni. Stellenbosch ya Afrika Kusini inashika nafasi ya 21 kwa alama 15 licha ya historia fupi ya ushiriki wa kimataifa, huku Dreams FC ya Ghana ikipanda hadi nafasi ya 26 baada ya mafanikio mazuri msimu uliopita.

15 BORA VIWANGO VYA KLABU VYA CAF 2025
1️.Al Ahly FC (Misri) – alama 78
2️.Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini) – alama 62
3️.Espérance de Tunis (Tunisia) – alama 57
4️.RS Berkane (Morocco) – alama 52
5️.Simba SC (Tanzania) – alama 48
6️.Pyramids FC (Misri) – alama 47
7️.Zamalek SC (Misri) – alama 42
8️.Wydad AC (Morocco) – alama 39
9️.USM Alger (Algeria) – alama 37
10.CR Belouizdad (Algeria) – alama 36
11.Al Hilal SC (Sudan) – alama 34
12.Yanga (Tanzania) – alama 34
13️.ASEC Mimosas (Ivory Coast) – alama 33
14️.TP Mazembe (DR Congo) – alama 30.5
15️.Orlando Pirates (Afrika Kusini) – alama 30