Iringa. Katika kuimarisha usalama wa wananchi na kudhibiti uhalifu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Iringa limekabidhiwa magari manane ya kisasa ili kuongeza ufanisi katika doria, kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya kiusalama na kuleta utulivu kwa wananchi.
Akikabidhi magari hayo leo Oktoba 23, 2025 katika Ofisi za Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Mkuu wa Mkoa huo, Kheri James amesema Serikali imeendelea kuwekeza kwenye usalama wa wananchi kwa kulikabidhi Jeshi la Polisi magari mapya kwa ajili ya kuimarisha utendaji kazi na kudhibiti uhalifu.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James akiwa nje ya ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoani humo akizungumza na Jeshi la Polisi mkoani humo katika hafla ya kukabidhi magari nane yatakayotumika kuimarisha ulinzi na usalama. Picha na Christina Thobias
James amesema magari hayo ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya serikali ya kuimarisha usalama wa nchi, hasa kuelekea uchaguzi.
Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa mkoa amewataka maofisa wa jeshi hilo kutumia magari hayo kwa uangalifu na kwa kazi zilizokusudiwa pekee.
Aidha, ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Iringa kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga vituo vya polisi ili kuimarisha huduma za ulinzi na usalama hasa katika maeneo ya vijijini na pembezoni.

Amesisitiza kuwa uwekezaji wowote wa Serikali hautakuwa na tija kama hakutakuwepo na usalama wa kutosha, hivyo ni wajibu wa vyombo vya usalama kushirikiana na jamii kulinda amani.
”Jeshi la Polisi limekuwa likiimarishwa kwa kutoa ajira mpya, kuongeza vitendea kazi na mafunzo ya mbinu mbalimbali ili kuhakikisha wanalinda maisha na mali za wananchi kwa ufanisi,” amesema.
Pia, ametoa wito kwa Jeshi la Polisi kushirikiana na wananchi kupitia dhana ya Polisi Jamii, akisisitiza kuwa usalama ni jukumu la kila mmoja.
Awali, akisoma taarifa ya magari hayo, ofisa wa polisi, Eustace Kinuno ameeleza kuwa magari yaliyotolewa ni Toyota Land Cruiser GXR 300, Toyota LX 5D Pick Up (2), Toyota LX 5D Hard top (2) na Toyota Hillux Double Cabin (3) huku akisema lengo ni kuleta mapinduzi katika kuimarisha doria na usalama wa raia.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Iringa, SACP Allan Bukumbi akizungumza na Jeshi la Polisi mkoani humo katika hafla ya kukabidhiwa magari nane yaliyotolewa na Serikali yatakayotumika kuimarisha ulinzi na usalama. Picha na Christina Thobias
Kamanda wa Polisi Mkoani Iringa, Allan Bukumbi, ametoa shukurani kwa Mkuu wa Mkoa na Serikali kwa kuongeza vitendea kazi na kusisitiza kuwa Jeshi la Polisi limejipanga kikamilifu kulinda amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
”Sisi kama Polisi tunaahidi tutafanya kazi, na tunawahakikishia kuwa kuelekea uchaguzi, Mkoa wa Iringa ni salama na mtu yeyote mwenye chokochoko atakutana na polisi na si wananchi,” amesema Kamanda Bukumbi.

Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Iringa, Glory Mtui ameeleza kuwa magari hayo yatasaidia pia kwenye uboreshaji wa doria na kupunguza ajali katika maeneo yenye changamoto kubwa za usalama barabarani.
Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Iringa, Peter Jackson ameeleza kuwa magari hayo yataleta utulivu na kusaidia wananchi kuendesha shughuli za kiuchumi bila hofu, jambo litakalosaidia ukusanyaji wa mapato ya Serikali kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Meneja wa Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) mkoani Iringa, Jackson Peter akizungumza na Jeshi la Polisi katika makabidhiano ya magari ya kuimarisha utendaji kazi. Picha na Christina Thobias
“Usalama ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi na tunashukuru Serikali kwa kuona umuhimu wa kuwapa Jeshi la Polisi vitendea kazi kama hivi.”