Mbeya. Viongozi wa dini Nyanda za Juu Kusini wameviomba vyombo vya ulinzi na usalama kutumia diplomasia kuhamasisha wananchi kupiga kura badala ya kukimbiza magari mengi barabarani, hali inayoweza kuathiri watu kushiriki katika kupiga kura.
Pia, wamewaomba viongozi wa dini, kila mmoja kwa nafasi yake, kutumia siku za Ijumaa, Jumamosi na Jumapili katika nyumba za ibada kuelimisha wananchi kujitokeza kupiga kura Oktoba 29, 2025.
Hayo yamebainishwa leo Oktoba 23, 2025 jijini Mbeya na Mwenyekiti Jumuiya ya Maridhiano Mkoa wa Mbeya, Askofu Oscar Ongere wakati wa kongamano la viongozi wa dini lililojumuisha mikoa ya Mbeya, Iringa, Songwe, Njombe na Rukwa, iliyoandaliwa na jumuiya hiyo.
Askofu huyo amesema zikiwa zimebaki siku chache kuelekea kwenye uchaguzi huo, kila mmoja ahamasishe waumini kujitokeza kupiga kura kwa mujibu wa katiba, akiwaomba kutimiza haki yao kuwachagua viongozi.
Amesema wakati viongozi wa dini wakifanya hivyo, vyombo vya ulinzi na usalama vinapaswa kutumia diplomasia nzuri kuhamasisha wananchi badala ya kutumia magari mengi, hali inayoweza kuchochea watu kutojitokeza kupiga kura.
“Tayari mkuu wa nchi ameweka utaratibu, sisi viongozi tujihamasishe na kuwahamasisha waumini kujitokeza kupiga kura, lakini vyombo vya ulinzi na usalama kuanzia Oktoba 27 na 28 vitumie diplomasia nzuri kwa kuwa wakikimbiza magari mengi, kesho yake watu hawataenda kupiga kura.
“Kubomoa nyumba ni rahisi sana kuliko kuijenga, tumeona na kushuhudia yanayowatokea mataifa ya jirani, hivyo ili tupate maendeleo na kila mmoja afanye shughuli zake, lazima tuilinde amani yetu ya nchi,” amesema Ongere.

Viongozi wa dini kutoka Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini wakiwa katika kongamano la kuliombea Taifa amani na utulivu kuelekea uchaguzi mkuu, lililoandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na amani nchini (JMAT) Mkoa wa Mbeya na Kamati za amani Nyanda za Juu Kusini.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dayosisi ya Nyanda za Juu Kusini, Jacob Kahemele amesema hofu iliyopo kwa sasa nchini ni ya kawaida kwa kuwa miaka yote ya uchaguzi, hali hiyo hujitokeza.
Amesema kinachotokea kwa sasa ni sawa na mataifa mengine hasa inapofika kipindi kama hiki, akieleza kuwa baada ya kumaliza uchaguzi nchi itaendelea na mambo mengine akiwaomba wananchi kuondoa hofu na kujitokeza kupiga kura.
“Tatizo letu ni namna ya kujibu hizo taharuki zinazotokea, hali hii si ya mwaka huu tu bali hata uchaguzi uliopita ilitokea ni sawa na familia wanandoa kutofautiana kauli lakini mwisho ni kutumia busara,” amesema Kahemele.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Ayas Njalambaha amesema dini zote zinahimiza amani ikiwa ndio msingi wa maisha akieleza kuwa hakuna uchaguzi bora na maendeleo bila amani akiwaomba wananchi kushikamana hasa kipindi hiki cha uchaguzi mkuu.
“Sisi Watanzania tunazo mamlaka na hata Uislamu unatambua mamlaka ukiashiria wanaosimamia sheria lazima kuwatii, hivyo tunaongozwa na kutii mamlaka zinazotuongoza, tulinde amani na kujitokeza kupiga kura,” amesema Sheikh huyo.
Akitoa tamko la jumuiya hiyo kwa ujumla, Profesa Anord Mwanjoka amesema kuelekea uchaguzi mkuu ni kudumisha amani na mshikamano na kushiriki kikamilifu katika kuchagua viongozi Oktoba 29, 2025.
“Tunawakumbusha wananchi wote nchini kujitokeza kushiriki uchaguzi ni haki kikatiba, viongozi wa kisiasa waonyeshe mifano, Tume Huru ya Taifa ya uchaguzi (INEC) isimamie uchaguzi uwe huru, haki na wa kuaminika, vyombo vya usalama kuzingatia utu, sheria na haki za binadamu.
“Sisi viongozi wa dini Nyanda za Juu Kusini, tuendelee kuiombea nchi yetu iwe yenye utulivu, amani, upendo na mshikamano na kukemea uchochezi na vurugu ya aina yoyote, tuilinde amani ya nchi,” amesema.