Dar es Salaam. Jarida la African Business limeiorodhesha Benki ya NMB Plc miongoni mwa benki 40 bora barani Afrika kutokana na msingi wake imara wa mtaji, faida thabiti na ukubwa wa mali.
Kwa mujibu wa orodha ya benki bora zilizotolewa na jarida hilo 2025, NMB ni miongoni mwa benki tano bora ukanda wa Afrika Mashariki, jambo linaloonesha ukuaji wake wa kudumu na uimara katika sekta ya fedha.
Katika taarifa iliyotolewa leo Alhamisi, Oktoba 23, 2025, benki hiyo inaeleza, utambuzi huo ni ushahidi kama moja ya taasisi za kifedha zenye nguvu na uthabiti zaidi Afrika.
Hatua hiyo imetokana na kujengwa kwa benki hiyo katika misingi imara, utawala bora na utekelezaji wenye nidhamu na mkakati wa muda mrefu wa ukuaji.
Kufikia Juni 2025, jumla ya mali za NMB zilikuwa zimevuka Sh14 trilioni, zikichangiwa na msingi imara wa mtaji, ukwasi wa kutosha na wastani wa ukuaji wa kila mwaka wa zaidi ya asilimia 30 kwenye faida halisi ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Pia, benki hiyo imeendelea kudumisha hadhi yake kama benki yenye faida kubwa zaidi nchini Tanzania, baada ya kurekodi faida halisi ya Sh358.57 bilioni katika nusu ya kwanza ya mwaka 2025, ongezeko la asilimia 14 kutoka Sh314.17 bilioni Juni 2024.
Kiwango cha faida kwa mtaji kwa NMB (return on equity) kimeendelea kuwa juu zaidi katika ukanda huu, kikiashiria usimamizi bora wa mtaji na uendeshaji makini wa shughuli zake.
NMB inahusisha mafanikio yake na utekelezaji bora wa mpango wake wa kati wa miaka mitano (2021–2025), unaolenga ujumuishaji wa kifedha, mageuzi ya kidijitali, ufanisi wa kiutendaji na maendeleo endelevu.
Kwa sasa, zaidi ya asilimia 96 ya miamala yote ya wateja inafanyika nje ya matawi ya benki, jambo linaloonesha mafanikio ya mkakati wake wa kidijitali.
Zaidi ya mafanikio ya kifedha, NMB inaendelea kuwa kinara katika benki yenye uwajibikaji na inayojali ustawi wa jamii na mazingira.
Mwaka 2021, NMB ilikuwa benki ya kwanza barani Afrika kuzindua Hati Fungani ya Kijinsia (Gender Bond), mpango uliodhihirisha dhamira yake ya kukuza ujumuishaji wa kifedha na kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Ubunifu uliipatia NMB utambuzi wa kimataifa, ikiwamo Tuzo ya Platinum ya Hati Fungani Endelevu Bora ya Mwaka kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC) na Jukwaa la Kimataifa la Fedha kwa Biashara Ndogo na za Kati (Global SME Finance Forum).
Benki hiyo pia imepokea tuzo za kimataifa, zikiwamo Tuzo ya Euromoney kwa Benki Bora Barani Afrika katika Uendelevu, Cheti cha Top Employer kwa ubora wa mazingira ya kazi na Cheti cha EDGE kwa usawa wa kijinsia, ikiifanya kuwa benki ya kwanza barani Afrika kufikia mafanikio hayo.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Mkurugenzi Mtendaji na Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, amesema, “utambuzi huu ni kielelezo cha uimara wa mkakati wetu, ustahimilivu wa watu wetu na imani ambayo wateja wanaendelea kuwa nayo kwetu.
“Huu ni wakati wa kujivunia kama Watanzania na sasa ni wajibu wetu kuendelea kujenga taasisi ya kifedha kwa kiwango cha kimataifa.”
Zaipuna amesema NMB itaendelea kuzingatia uendelevu, teknolojia na ubora wa huduma kama nguzo kuu za ukuaji wake wa baadaye.
Amesema NMB katika kusherehekea utambuzi huo Afrika, inatoa shukrani kwa wadau, wateja, wafanyakazi, wanahisa, washirika na wadhibiti kwa imani na ushirikiano wao.
“Tunayaweka mafanikio haya kwa kila mdau ambaye amesafiri nasi katika safari hii, hatujengi benki pekee, bali tunabadilisha maisha na kujenga mustakabali thabiti zaidi wa kifedha kwa Tanzania na ukanda mzima,” taarifa ya benki hiyo imeeleza.
