Siri, makosa upigaji wa chafya

Kupiga chafya ni tendo la kawaida la kibinadamu ambalo huchukuliwa kama jambo la kawaida kiasi kwamba watu wengi hawalipi uzito. 

Hata hivyo, nyuma ya tendo hili dogo la kiafya kuna mchakato wa ajabu wa mwili unaotimiza majukumu muhimu ya kinga.

Kupitia vyanzo mbalimbali vya kimtandao, makala haya, itaangazia kwa undani siri iliyofichika nyuma ya chafya, maana yake kiafya, na makosa ya kawaida ambayo watu hufanya wanapopiga chafya.

Kupiga chafya ni mchakato wa kiasili unaosaidia mwili kuondoa vitu visivyotakiwa katika njia ya pua. Mara nyingi, tunapopumua, hewa huingia pamoja na chembechembe kama vumbi, poleni, vijidudu, na moshi. 

Pua ina nywele na ute  unaosaidia kuchuja uchafu huu, lakini wakati mwingine vitu hivyo hufika ndani zaidi. Mwili hupokea taarifa hiyo kupitia neva maalum zilizoko katika pua na koo na kuamsha mchakato wa chafya.

Kwa kifupi, chafya ni njia ya mwili ya “kujisafisha” haraka, kwa nguvu, na kwa ufanisi. Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa kupiga chafya ni jibu la kinga ya mwili linalotokea kwa kasi ya ajabu. Wakati mwingine kasi ya hewa inayotoka wakati wa chafya hufikia hadi kilomita 160 kwa saa (km/h), ikimaanisha ni kama mlipuko mdogo wa ndani unaosukuma nje kitu kisichotakiwa.

Daktari bingwa wa afya ya masikio, koo na pua kutoka Hospitali ya Kanda ya Rufaa Bugando, Dk Masumbuko Madebele anasema faida kuu za kupiga chafya ni kusafisha njia ya pua na hewa.

“Chafya huondoa uchafu na vijidudu vilivyoko kwenye utando wa pua kabla havijafika mapafuni. Ni kinga ya mwili ya asili inayosaidia kuzuia magonjwa ya njia ya hewa kama mafua, ‘sinusitis’, na hata nimonia,”anasema Dk Madebele na kuongeza:

“Lakini pia, husaidia kupunguza mzio kwa kuondoa vichocheo kabla havijasababisha athari kubwa kama madoa ya ngozi au kushindwa kupumua na hupunguza msongamano wa pua (nasal congestion) kwakuwa huweza kufungua mirija ya pua iliyoziba na kusaidia upumuaji kuwa mwepesi.”

Mwaka wa 2021, timu ya watafiti katika Chuo Kikuu cha Washington, St. Louis walifanya utafiti wa kuvutia juu ya jinsi panya wanavyopiga chafya. Panya wakiwa ni wanyama wanaofanana kwa sehemu nyingi za mfumo wa neva na ubongo na binadamu.

Watafiti waligundua kuwa kupiga chafya si jambo la nasibu, bali ni jibu la kinga la mwili linalosimamiwa na ubongo. Jibu hilo linahusisha sehemu kadhaa za ubongo.

Sehemu muhimu ni trigeminal nucleus, ambayo ni kiini cha ubongo kinachopokea taarifa za hisia kutoka kwenye pua na uso.

Wakati kitu kinachochochea, kama vumbi au poleni, kinagusa pua, neva za pua zinatuma ishara kwenda trigeminal nucleus, na sehemu hii ya ubongo inachochea mwili kuanza kupiga chafya.

Utafiti huo pia ulionyesha kuwa protini maalumu inayosaidia usafirishaji wa ishara za neva ndani ya ubongo na neva za hisia (neuromodulin B),  ina jukumu muhimu katika kupeleka ishara hizi za kupiga chafya.

Moja, mzio:Watu wenye mzio hupiga chafya mara kwa mara hasa wanapokutana na vichochezi kama vumbi, poleni, manyoya ya wanyama au manukato makali.

Mbili, mabadiliko ya halijoto:Kuwapo kwenye mazingira ya baridi ghafla au kuingia sehemu yenye hewa kali kunaweza kuchochea chafya.

Tatu, magonjwa ya viroboto: Mafua, homa ya kawaida, na mafua ya mzio husababisha chafya kwa sababu virusi huathiri njia ya hewa ya juu.

Nne, mwanga mkali: Watu wengine hupiga chafya wanapokutana na mwanga mkali wa jua; hali hii huitwa “photic sneeze reflex”, ambayo huwa ya kurithiwa kijenetiki.

Ingawa chafya ni jambo la kawaida, watu wengi hufanya makosa yanayoweza kuhatarisha afya yao wenyewe au wengine. 

Baadhi ya makosa haya yanaweza kuepukwa kirahisi ikiwa kutakuwepo na uelewa sahihi.

Watu wengi hujaribu “kumeza” chafya au kuizuia kwa kuziba pua na mdomo. Hili ni kosa kubwa. Kuzuia chafya kwa nguvu kunaweza kusababisha madhara makubwa kama vile kuvunjika kwa mishipa midogo ya damu kwenye macho au uso, kuumiza ngoma ya sikio.

Dk Madebele anasema iwapo mtu ataziba pua na mdomo wakati wa kupiga chafya shinikizo la ndani la kichwa linaweza kuongezeka na kusababisha kupasuka kwa mishipa midogo ya damu kwenye macho, masikio au ubongo, kuvimba kwa uso au sikio (barotrauma), ngoma ya sikio inaweza kupasuka au kupata maumivu makali.

Anasema iwapo mtu akijisikia kupiga chafya akaizuia anaweza kupata madhara ya kwakuwa uchafu hubaki kwenye njia ya hewa na kuongeza hatari ya maambukizi ya sinus (sinusitis), kupumua kwa shida pamoja na maambukizi ya mapafu.

Ni muhimu kuiruhusu chafya itoke kwa njia salama bila kuizuia.

Pili, kupiga chafya bila kufunika pua na mdomo.Hili ni kosa kubwa sana hasa wakati wa msimu wa magonjwa ya kuambukiza kama mafua. Kupiga chafya bila kufunika mdomo au pua hueneza vijidudu hewani na kuwaweka wengine katika hatari.

Wataalamu wa afya wanashauri kutumia tishu safi kufunika mdomo na pua, au kupiga chafya kwenye kiwiko cha mkono ikiwa hakuna tishu karibu.

“Mtu akitaka kupiga chafya atumie tishu safi au kiganja kufunika mdomo na pua unapopiga chafya kisha atupe tishu na kuosha mikono,”anasema.

Tatu, kutonawa mikono baada ya chafya.Chafya hutawanya chembechembe ndogo za mate au ute wa pua. 

Ikiwa mikono itagusa maeneo ya uso au vitu vingine baada ya kupiga chafya, kuna uwezekano mkubwa wa kusambaza vijidudu. 

Ni muhimu kunawa mikono kwa maji na sabuni au kutumia vitakasa mikono mara baada ya kupiga chafya.

Nne, kutojali dalili zinazofuatana na chafya.Watu wengi huchukulia chafya kama jambo la kawaida, lakini wakati mwingine chafya inaweza kuwa dalili ya tatizo kubwa zaidi kama mzio mkali, maambukizi ya ‘sinus’ pumu, Uviko-19 au mafua makali.

Ikiwa mtu anapiga chafya mara nyingi kwa siku kadhaa, hasa akifuatana na dalili kama homa, kikohozi, au maumivu ya kichwa, ni vyema kumuona daktari.

Tano, kushika pua kwa nguvu wakati wa chafya. Baadhi ya watu hushika pua kwa nguvu wakidhani wanazuia chafya kutoka kwa sauti. Hii ni hatari kwa sababu hewa iliyozuiliwa hutafuta njia nyingine ya kutokea, hivyo inaweza kusababisha kuvimba kwa pua au maeneo ya uso,  kuumiza sikio la ndani na kuvuja damu puani.

Kupiga chafya si tu tendo la kiasili la mwili bali pia ni njia muhimu ya kujilinda dhidi ya vimelea na uchafu. 

Hata hivyo, namna tunavyoshughulikia chafya huweza kuwa na athari kubwa kwa afya binafsi na afya ya jamii.

Ni muhimu kufahamu kuwa kuizuia chafya, kupiga chafya ovyo bila kufunika mdomo, na kutozingatia usafi wa mikono ni makosa yanayoweza kuepukwa kwa elimu sahihi.

Makala inahimiza afya bora kwa jamii nzima. Kupiga chafya kwa heshima, kwa usafi, na kwa usahihi ni ishara ya uzalendo na uwajibikaji wa kiafya kwa kila mtu.  Katika dunia ya leo iliyojaa maambukizi kila chafya ni jukumu la kijamii.