Dar es Salaam. Watu wengi hivi sasa ni wapekuaji hodari wa mitandao ya kijamii ikiwamo WhatsApp, Instagram, Facebook, TikTok na mitandao mingine.
Mwaka 2023 kulikuwa na wastani wa watumiaji bilioni 4.9 wa mitandao ya kijamii ulimwenguni, ikikadiriwa mtu wa kawaida kutumia wastani wa dakika 145 kwenye mitandao hiyo kila siku.
Matumizi holela ya mitandao yanaweza kuathiri vibaya ustawi wa ujumla kwa kuchochea hali ya wasiwasi, huzuni, upweke, woga, hofu ya kukosea, uraibu, kutochangamana, kutojiamini na kujitenga.
Masuala haya yameenea hasa kwa wanaobalehe, vijana na watu wazima umri wa kati. Hali hizo zikidumu huteteresha afya ya akili hatimaye kuathiri umakini wa darasani na utendaji kazini.
Hali ya uraibu ya mitandao ya kijamii huwezesha kituo maalum katika ubongo kwa kutoa kichochezi cha dopamine ambacho kinatufanya kujisikia vizuri hasa katika shughuli za kupendeza na kufurahisha.
Tunapochapisha kitu, marafiki na familia zetu wanaweza kukipenda, na hivyo kutupa nguvu ya dopamine. Hata hivyo, kisipopendwa au kupata ukosoaji mbaya heleta huzuni, hasira na kujiona dhaifu.
Uraibu hukufanya kuwa mtumwa wa mitandao hivyo kuwa mbebaji wa athari mbaya iikiwamo mtetereko wa afya ya akili.
Simu janja na mitandao hiyo huwa vichujio kwa Kingereza filter kinachoupa mwonekano picha ya mwili kuvutia kuliko uhalisia.
Majukwaa mengi ya mitandao ya kijamii huwapa watumiaji chaguo la kutumia vichungi vyenye picha za kuvutia.
Vichungi vinaweza kuwa vizuri kwa kicheko, lakini uwezo wa kubadilisha sura ya mwili kwa urahisi na kuficha kasoro ambazo huunda udanganyifu wa kiwango cha juu.
Picha hizo zilizobadilishwa zinaweza kukufanya ujisikie na kutopenda jinsi unavyoonekana na pia huongeza hisia za hofu ya kukosa kwa watu wengi.
Kuangalia marafiki na familia yako kupitia mitandao ya kijamii kunaweza kukufanya uhisi kuwa wengine wanaburudika zaidi au wanaishi maisha bora kuliko wewe. Vile vile mitandao huonyesha sehemu bora za maisha ya mtumiaji.
Hili linaweza kuathiri kujistahi, kuzua wasiwasi na kuwafanya watu kutumia mitandao ya kijamii zaidi ili wasikose kile kinachoendelea.
Mwaka 2020, asilimia 44 ya watumiaji wote wa intaneti nchini Marekani walisema wamenyanyaswa mtandaoni.
Mitandao ya kijamii inaweza kuwa sehemu kuu za unyanyasaji wa mtandaoni na kueneza uvumi wenye kuumiza, uongo na matumizi mabaya ambayo yanaweza kuacha makovu ya kudumu ya kihisia
Kuelewa jinsi mitandao inavyoathiri afya yetu ya akili na ustawi wetu kwa ujumla ni muhimu ili kulinda jamii isiingie katika mgogoro mkubwa wa kiafya.
Njia nzuri ya kuboresha uhusiano wako na mitandao ya kijamii na kusaidia kupunguza athari mbaya, ni kupunguza muda wako wa kutumia simujanja au vifaa vingine vya kuperuzi kila siku.
Chagua saa maalum za matumizi ya mitandao ya kijamii; angalia orodha ya marafiki na wafuasi wako na usifanye urafiki na watu ambao akaunti zao hukufanya ujisikie vibaya.
