Wananchi Ngara kunufaika na msaada wa gari la zima moto

Ngara. Serikali imekabidhiwa gari la kuzimia moto kwa ajili ya kusaidia shughuli za kudhibiti majanga ya moto katika Wilaya ya Ngara mkoani Kagera.

Kwa miaka mingi, wakazi wa Ngara wamekuwa wakishuhudia moto ukiteketeza nyumba, mali na hata maisha bila msaada wa haraka.

Hali hiyo inatarajiwa kubadilika kufuatia msaada wa gari hilo la zima moto lililotolewa na kampuni ya uzalishaji umeme wa Rusumo (RPCL).

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Maduhu Kazi baada ya kupokea Gari hilo na kueleza mikakati ya Serikali kuhusu jeshi la Zimamoto na Uokoaji Nchini.

Gari hilo lenye thamani ya zaidi ya Sh2.1 bilioni, limekabidhiwa kwa Wizara ya Mambo ya Ndani leo Ijumaa Oktoba 24, 2025 likiwa na vifaa vya kisasa vya kudhibiti moto na kuokoa maisha ya watu an mali zao.

“Tumepata mkombozi, msaada huu umefika wakati unaohitajika Zaidi,” amesema Yusuph Paulo, mkazi wa Ngara aliyeshuhudia magari matano ya mizigo yakiteketea kwa moto mwaka 2018 na tukio jingine la watu kuungua ndani ya nyumba mwaka 2024,” amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Kanali Mathias Kahabi amesema wilaya hiyo imekuwa ikikumbwa na majanga ya moto kwa muda mrefu na upatikanaji wa gari hilo ni hatua ya kihistoria.

“Tulikuwa tukipoteza mali na maisha kutokana na kukosa msaada wa haraka. Hii ni neema kwa wananchi wetu,” amesema.

Akizungumza wakati akipokea gari hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Dk Maduhu Kazi amesema msaada wa RPCL unaonyesha ushirikiano wa kweli kati ya Serikali na sekta binafsi katika kulinda maisha ya Watanzania.

“Huu ni mfano wa kuigwa, Serikali inaendelea kushughulikia changamoto za Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, lakini tunafarijika kuona wadau kama RPCL wakijitokeza kusaidia,” amesema Dk Maduhu.

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Happiness Shilima akieleza gari hilo litakavyotumika kuhimalisha huduma za uokoaji kwenye jamii.

Ameongeza kuwa kupitia mradi wa Adex, Serikali imepata mkopo wa Dola za Marekani 100 milioni kwa ajili ya kununua magari, boti na helikopta moja, hatua itakayoongeza ufanisi wa jeshi hilo nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa RPCL, Ntare Karitanyi amesema kampuni hiyo imekuwa ikitumia sehemu ya mapato yake kusaidia jamii zinazozunguka mradi wa umeme wa Rusumo, unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania, Rwanda na Burundi.

“Mradi wa Rusumo si wa nishati pekee, bali pia ni mradi wa maendeleo ya watu. Tunataka jamii iondokane na hofu ya majanga, ndiyo maana tumewekeza katika gari hili lenye vifaa vya kisasa,” amesema Karitanyi.

Wakati huohuo, askari 10 wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wamepatiwa mafunzo maalumu ya kutumia gari hilo kutoka kampuni ya Achelis, wauzaji rasmi wa vifaa hivyo.

Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Happiness Shirima amesema hadi sasa Tanzania Bara ina vituo 83 vya zimamoto, lakini bado inakabiliwa na upungufu wa zaidi ya vituo 200 vinavyohitajika kufikia huduma bora kwa wananchi.

 “Kupokea gari hili leo ni hatua kubwa. Tutaliweka katika matumizi mara moja, na litasaidia kusukuma huduma zetu mbele, hasa kwa wananchi wa Ngara,” amesema Shirima.