Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku tano kabla ya Watanzania kupiga kura tarehe 29 Oktoba 2025, baadhi vyama vya siasa vimekuwa na malalamiko juu ya uapishaji wa mawakala, hatua inayosababisha kukosa watu wa kusimamia kura zao kwenye vituo mbalimbali.
Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Jacobs Mwambegele amesema hawezi kutolea taarifa madai hayo kwa kuwa hajayapata kwa njia rasmi, akisema la kuongeza muda wa kuapisha mawakala, ni lenye misingi ya kisheria.
“Kuhusu kuongeza muda wa kuteua na kuapisha mawakala suala lipo kisheria, sheria imetoa muda wa siku saba kabla ya uchaguzi kwa mawakala kuapishwa,” amesema Jaji Mwambegele, akisisitiza kuwa madai ya ACT- Wazalendo yatatolewa ufafanuzi baada ya kupokelewa rasmi na kupitiwa hoja zake.
“Kwa sasa bado sijapewa taarifa ya kupokewa kwa barua hiyo, hivyo siwezi kutolea ufafanuzi wowote,” amesema.
Chama cha ACT Wazalendo ni miongoni mwa vyama vilivyoibua malalamiko hayo, kikidai kukosa mawakala katika maeneo mbalimbali kutokana na dosari kwenye uapisho na hivyo kuomba INEC iongeze muda hadi Oktoba 27, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa ya chama hicho iliyotolewa kwa umma jana Alhamisi, Oktoba 23, 2025, ACT imesema mawakala wake katika maeneo mbalimbali wameshindwa kuapishwa kutokana na vikwazo tofauti tofauti.
Taarifa hiyo iliyosainiwa na Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, Mbarala Maharagande imeeleza kuwa maombi ya kuongezwa muda yametolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 40(2) na Kanuni ya 40(6) ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani, inayoruhusu Tume kuongeza muda kwa vyama kuwasilisha au kuwaapisha mawakala.
“Maombi haya yapo kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi ambapo Tume imepewa mamlaka ya kuratibu zoezi hilo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.
ACT Wazalendo imesema zoezi la uapisho limekumbwa na ukiukwaji wa sheria, ikidai baadhi ya mawakala wamekuwa wakipewa taarifa zisizo sahihi kuhusu muda na mahali pa kufika kuapishwa, huku baadhi ya wasimamizi wakikataa kuwaapisha mawakala wa ACT kwa madai hawajafikishaumri wa miaka 18 bila ushahidi wa kisheria.
Aidha, chama hicho kimedai kumekuwa na wasimamizi wanaowataka mawakala kuwa na vitambulisho vya kupigia kura na picha mbili, kinyume na mwongozo wa kanuni za uchaguzi, jambo lililokwamisha chama hicho kuapisha mawakala katika maeneo mbalimbali.
Kutokana na changamoto hizo, ACT Wazalendo imeiomba Tume kuongeza muda wa zoezi hilo hadi Oktoba 27, 2025, ikiwa ni siku mbili kabla ya uchaguzi, ili kutoa nafasi sawa kwa vyama vyote kuwa na mawakala waliotambulika kisheria.
Kwa mujibu wa chama hicho, hatua hiyo ni muhimu katika kulinda uhalali wa uchaguzi na kuimarisha imani ya umma kwa Tume.
ACT imeonya kuwa endapo hatua stahiki hazitachukuliwa, kukosekana kwa mawakala kunaweza kuathiri haki ya vyama na matokeo ya uchaguzi kwa ujumla.
Mbali na ACT-Wazalendo, mgombea urais wa Chama cha Wananchi (CUF), Gombo Samandito naye amedai mawakala wengi wa chama hicho wameshindwa kuapa kwa sababu mbalimbali, hivyo kukosa sifa za kisheria kusimamia vituo walivyopangiwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Morogoro, Jumatano Oktoba 22, 2025 Gombo amesema kwenye baadhi ya majimbo nchini mawakala wa chama hicho hawajajitokeza kuapa kwa sababu tofauti.
“Kuna jimbo moja zaidi ya mawakala wetu 300 kati ya 500 tuliowateua wameshindwa kwenda kuapa, hali hii inaharibu uchaguzi huru na wa haki” amesema akitaja uhaba wa fedha na hujuma kuwa sababu kuu za tatizo hilo.
Mgombea huyo ameeleza masikitiko hayo akitoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) na kutekeleza wajibu wake kwa haki na bila upendeleo, hasa kwa vyama ambavyo vimekosa mawakala kwenye baadhi ya maeneo.
“Nawaomba INEC watende haki kwa wote hasa kwa vyama ambavyo vimekosa mawakala,” amesema Gombo.
Kwa upande mwingine, Msemaji wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), John Mrema amesema Tume ya Uchaguzi imeonyesha ushirikiano wa kuridhisha katika utekelezaji wa majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni.
Hata hivyo, awali alitilia shaka mchakato wa upatikanaji na uapishwaji wa mawakala, akidai baadhi ya mawakala wamekuwa wakiombwa vielelezo vingi tofauti na vinavyotakiwa na kanuuni za uchaguzi.
“Kanuni zinasema wakala anatakiwa kuwa na barua ya utambulisho kutoka chama chake, picha mbili na kitambulisho chochote, lakini wapo wasimamizi wanaandika barua wakitaka vielelezo vingi zaidi kama hati ya kusafiria, leseni au Nida, jambo ambalo haliko kwenye kanuni,” alisema na kuongeza:
“Kuhusu hatua zilizobaki za kupiga kura, kuhesabu na kutangaza matokeo, ni imani yetu kuwa watasimamia zoezi hilo kwa mujibu wa sheria na kanuni. Wanatakiwa kutenda haki kwa wagombea wote,” amesema.
Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani za mwaka 2024, kifungu cha 40.(1), msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi, ndani ya siku 14 kabla ya siku ya uchaguzi au kipindi kingine chochote kitakachoelekezwa na Tume, atawapa wagombea au vyama vya siasa majina na anuani za vituo vya kupigia kura.
Kifungu kidogo cha cha (2) cha kanuni hiyo kinasema kwa kuzingatia masharti ya sheria, chama cha siasa kinachoshiriki katika uchaguzi, kitawasilisha kwa msimamizi wa uchaguzi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi taarifa yenye orodha na barua za utambulisho za mawakala walioteuliwa katika kila kituo cha kupigia kura si chini ya siku saba kabla ya siku ya uchaguzi au ndani ya muda mfupi zaidi kadiri Tume itakavyoruhusu.
“Taarifa ya mawakala itaambatishwa na nyaraka zifuatazo kuhusiana na kila wakala (a) picha mbili za rangi zenye ukubwa sawa na picha inayotumika katika pasi ya kusafiria; (b) nakala ya kitambulisho cha taifa; (c) nakala ya kadi ya mpiga kura; au (d) nakala ya pasi ya kusafiria: Isipokuwa kwamba, kituo cha kupigia kura kitakuwa na wakala mmoja kutoka chama cha siasa kinachoshiriki uchaguzi ambaye atakuwa ni wakala kwa wagombea wa chama hicho katika uchaguzi wa Rais, mbunge na diwani,” kifungu kidogo cha 4) cha sheria hiyo kinasema.
Aidha kifungu kidogo cha (7) kinaweka msingi kuwa wakala wa upigaji kura hataruhusiwa kuingia katika kituo cha kupigia kura bila kuapa kiapo cha kutunza siri.
Kauli hizo kutoka za vyama zimeibua mjadala mpana kuhusu uwazi na maandalizi ya uchaguzi wa mwaka 2025, ambapo wadau wa siasa wanaona kuna haja ya Tume kuchukua hatua za haraka kuhakikisha haki inatendeka kwa vyama vyote na kuondoa hofu ya upendeleo katika usimamizi wa uchaguzi.
Akizungumzia madai ya vyama hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Conrad Masabo amesema malalmiko hayo yanarejea madai ya muda mrefu ambayo yamekuwa yakijirudia kila uchaguzi nchini, hivyo akiona umuhimu wa kuangaliwa mfumo mzima wa uchaguzi ili kuyakomesha.
“Hata uchaguzi wa serikali za mitaa 2024 yalitokea madai kama hayo yote, hivyo malamiko hayo si jambo jipya. Bila mabadiliko ya kweli chaguzi zetu haziwezi kuwa huru, ukishakosa wakala kituoni huna uhakika wa matokeo yako,” amesema.
Ameongeza kuwa sheria zimetoa mamlaka kila linalofanywa na Tume ya uchaguzi halihojiwi na mamlaka yoyote, hivyo hakuna cha kufanya bila kuwa na mabadiliko ya mfumo mzima wa uchaguzi,” amesema.
