Maswa. Mgombea urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Salum Mwalimu amewasili katika Jimbo la Maswa Magharibi analogombea John Shibuda, mbunge wa zamani wa CCM na Chadema na kueleza kwa nini anapaswa kuchaguliwa tena kuwa mbunge.
Mwalimu ameyasema hayo leo Ijumaa, Oktoba 24,2025, katika mkutano wake wa kampeni zake za lala salama alioufanya katika Kata za Wigelekelo, Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu.
Shibuda aliwahi kuwa Mbunge wa Maswa Chama cha Mapinduzi (CCM) mwaka 2005 hadi 2010, Mbunge wa Maswa Magharibi mwaka 2015 hadi 2020 kupitia Chadema.
Akimwelezea mwanasiasa huyo, Mwalimu amesema Shibuda ni mwalimu wake, mlezi na baba yake kisiasa, hivyo watakapomchagua ndiye atakayekuwa pia mshauri mkuu wakati wa kuiongoza nchi kwa kuwa ni mtu aliyelelewa kwenye misingi ya baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
“Kwa hiyo huku kwa mzee wangu Shibuda leo sijafika kwa bahati mbaya licha ya kuja mwishoni. Nimekuja kwa mambo mawili, moja kumuombea kura mzee wangu huyu Shibuda na pili kupata baraka zake.
“Huyu mzee ni nguli wa siasa, akiniambia nikae nakaa, akiniambia nenda mbele naenda, kiukweli wazee wa aina yake wamebaki wachache, wenye kuishi kwenye misingi ya utaifa,” amesema Mwalimu.
Akijiombea kura ya urais kwa wananchi hao, Mwalimu amesema yupo tayari kwenda kuiongoza nchi ikawe ni nchi yenye amani na haki.
Katika hilo alinukuu kauli ya baba wa taifa aliyeitoa mwaka 1962 ambayo amedai kuwa inaiishi hadi leo ya kuwa ‘hatuwezi kutatua matatizo yetu tukijidanganya kuwa hayapo.
“Tunaona leo hospitali hazina dawa, tatizo la ajira kwa vijana, migogoro ya ardhi. Wanatudanganya kila siku kuwa nchi ipo sawa wakati ni uongo.
“Ona Mungu amewajalia madini, mifugo na Tanzania ni nchi ya pili kwa mifugo lakini angalieni hali zenu zilivyo, kulikuwa na zao la pamba hapa ambalo Mwalimu Nyerere alilitumia kusomesha wazee wetu leo lipo wapo wameliua,’ amesema.
Mwalimu amesema katika ilani ya Chaumma, mojawapo ya mambo watakayoyatekeleza ni kurejesha heshima ya zao la pamba katika Kanda ya Ziwa.
Ameeleza kuwa katika juhudi za kukuza kilimo kwa ujumla, Chaumma imepanga kufuta mfumo kandamizi wa vyama vya ushirika ambao umekuwa ukiwanyanyasa na kuwalangua wakulima kwa kuhodhi soko na kudhibiti bei za mazao.
Badala yake, amesema chama hicho kitaanzisha mfumo wa ushirika wa hisa utakaomfanya kila mkulima awe na sauti katika uendeshaji wa ushirika na kunufaika moja kwa moja na mapato ya mazao yao.
Kuhusu sekta ya mifugo, Mwalimu amesema Chaumma itaanzisha kiwanda cha ngozi katika Kanda ya Ziwa, kwa kuwa licha ya mikoa hiyo kuwa na mifugo mingi, bado haina kiwanda kama hicho, wakati duniani matajiri wengi wanavaa bidhaa zinazotokana na ngozi asilia kutoka Afrika.
Awali akimkaribisha mgombea urais huyo, Shibuda amesema Oktoba 29, 2025 ni siku ya maamuzi magumu, akiwataka wananchi wasitishwe kwenda kupiga kura.
“Nawaomba hiyo siku mkajitokeze kwenda kupiga kura, na Mwalimu ndiye chaguo sahihi kwenu. Ndiye mkuki wa mashujaa wa kuwatungua wale wenye midomo ya kutoa ahadi zisizotekelezeka,” amesema Shibuda.
Alisisitiza kuwa wananchi wasione aibu kwenda kupiga kura, iwe kuna jua au mvua, kwani kufanya hivyo “ni kama kufanya udobi wa kuondoa uchakavu wa uongozi uliopo.”
Ameongeza kuwa moja ya mambo ambayo Mwalimu atayatekeleza ni kutengua uongo na kuleta uhalisia katika uongozi wa nchi. Shibuda amesema ilani ya uchaguzi ni mpango wa utekelezaji wa ahadi, lakini kwa muda mrefu baadhi ya viongozi wamekuwa wakiiahidi bila kuitimiza.
“Kupitia Mwalimu, wafugaji watapata maeneo rasmi ya malisho, wakulima watasimamiwa kupata bei nzuri za pembejeo, hivyo kumchagua ni sawa na kupata bima ya furaha kwa makundi yote ya wananchi,” ameongeza Shibuda.
Naye Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano wa Chaumma, John Mrema, amesema wamemsimamisha Shibuda kugombea ubunge katika jimbo hilo kwa sababu “kijiji hakiwezi kukamilika bila mzee.”
“Mwalimu akiwa kwenye kufanya maamuzi, lazima kuwe na mzee wa kumshauri. Hivyo naombeni sana mkampe kura Shibuda kwa kuwa ana uzoefu na hekima ya uongozi,” amesema Mrema.
