BAADA ya kupoteza dhidi ya Tanzania Prisons, Kocha wa Mbeya City, Malale Hamsin amesema ameshajua shida iliko na amejipanga kuiondoa mapema tu.
Mbeya City ambayo Juzi ilichezea KMC Complex kama uwanja wake wa nyumbani, hadi sasa imecheza mechi tano, ikishika nafasi ya kwanza kwenye msimamo na ndiyo timu iliyocheza mechi nyingi zaidi.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Mlale amesema Licha ya timu hiyo kuongoza kwa pointi lakini bado hali siyo nzuri kwani alama saba kwenye mechi tano siyo kiwango kizuri.
Amesema wachezaji wanatakiwa kujiuliza kama timu zingine zingecheza mechi kama wao, Je? wangekuwa nafasi ya ngapi kulingana na pointi.
“Nimewaambia wachezaji kutobweteka kwa matokeo ambayo wamepata kwani safari ya kutimiza malengo yao bado mbichi, kwani timu za sasa hivi zinaviwango vikubwa sio rahisi kupata matokeo.
“Baada ya matokeo haya, nimejua wapi natakiwa kupakazania zaidi na si pengine ni eneo la ushambuliaji, naona bado wamekuwa wazito kutengeneza na kutumia nafasi.”
Aliongeza; “Licha ya kupoteza kwa mara ya pili ila nawaamini wachezaji wangu na mara zote wamekuwa na kiwango bora ila maboresho hayakosekani ili kuhakikisha malengo ya timu yanatimia.”
Mbeya City kwa sasa imeshinda na kupoteza mechi mbili na sare moja, ikifikisha jumla ya pointi saba, ikifuatiwa na Singida Black Stars na Simba ambazo zimecheza michezo miwili na kuvuna alama sita.
