Mwameja: ‘Manula bab’kubwa, anastahili Tanzania One’

Makipa wa zamani waliowahi kutamba na jina la Tanzania One, Mohamed Mwameja na Idd Pazi ‘Father’ wamezungumzia sifa za jina hilo, huku wakimtaja kipa wa zamani wa Simba, Aishi Manula aliyetua Azam FC msimu huu.

Wakongwe hao wamemezungumzia kipi wafanye wachezaji kwa sasa katika nafasi hiyo ili walifufue jina hilo na lianze kusikika tena.

Aishi Manula kabla ya kuumia na kukaa nje kwa takriban msimu mzima uliopita akiwa na Simba, aliwahi kutamba na jina hilo kwa muda mrefu, lakini kwa sasa linaonekana kama halina mwenyewe.

Manula aliandika rekodi ya kuchukua tuzo ya kipa bora mara mbili akiwa Azam FC kisha Simba 2017/18 alimaliza na ‘clean sheet’ 19, ilhali 2018/19 alimaliza nazo 18, huku 2019/10 akiwa nazo 12 na 2020/21 zilikuwa 18.

Kipa wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Mohamed Mwameja aliyeweka rekodi ya kuitwa jina hilo kuanzia 1992 hadi 1997, alisema baadhi ya sifa za kipa anayepaswa kuwa na jina hilo ni pamoja na kuwa na mwendelezo wa muda mrefu wa ubora awapo golini.

MWAME 01

“Jambo la kwanza sifa ya Tanzania One ni kipa kuwa na mwendelezo wa kiwango angalau miaka mitatu na zaidi na siyo mechi moja inayofuata anapotea ama msimu mmoja unafuata anacheza vibaya,” amesema Mwameja na kuongeza:

“Japokuwa kwa sasa sijajua wanaangalia kitu gani, zamani anaangaliwa kipa bora kuanzia ligi za chini hadi Ligi Kuu ambaye anakuwa tegemeo kwa timu ya taifa, mfano mimi nilibahatika kuitwa jina hilo kuanzia mwaka 1992 hadi 1997 baadaye likahamia kwa Juma Kaseja niliyepishana naye, wakati anakuja Simba mimi nilienda nje.

MWAME 03

“Tanzania One niliipokea kutoka kwa Ally Bushiri alikuwa kipa namba moja wa Muungano na Idd Pazi alikuwa kipa namba moja wa Tanzania, viwango vyao vilikuwa vya juu.

“Siyo lazima Tanzania one atokee Simba ama Yanga anaweza akawa nje ya hizo timu, kitu kikubwa ni wao kujitambua na kujituma kwa bidii, ili kulinda viwango vyao, wajue soka linataka nini kutoka kwao na wao wanataka nini katika kazi hiyo.”

MWAME 02

Kipa na kocha wa zamani wa Simba,  Idd Pazi ‘Father’ amesema ili kipa aitwe Tanzania One lazima ategemewe na taifa, kiwango chake kisiwe cha kubahatisha, nidhamu na kujitambua.

“Mara nyingi nimekuwa nikitoa mfano wa Kaseja namna alivyokuwa ananifuata na kuniambia kocha umeionaje mechi niliyocheza na kipi nikifanyie kazi, aliipenda kazi yake na alifanya mazoezi binafsi kwa bidii, jambo linalowashinda wengi wanapopata majina wanajisahau na kutoka katika mstari.”