KOCHA Mkuu wa Dodoma Jiji, Amani Josiah amesema bado anaamini ubora wa wachezaji wake lakini akaitaja ratiba ya mechi ya Ligi Kuu Bara ni kikwazo kwake kubadili mambo huku akizitaja siku 21 ndani ya klabu hiyo.
Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah amesema baada ya kutua Dodoma Jiji, bado hajapata muda mwafaka wa kuingiza falsafa zake kutokana na mechi kuwa karibu na ndani ya siku 10 wamekuwa na mechi tatu.
Josiah amesema ukaribu wa michezo hiyo umekwamisha kufanyia kazi changamoto nyingi zikiwemo mbinu za ufungaji ambazo ndio zinazowatatiza.
Dodoma Jiji kwenye mechi zake mbili za mwisho haijafunga bao lolote ikiwa imeshacheza mechi tano ikishinda moja, ikitoa sare mbili na kupoteza michezo miwili.
“Hatujapata muda sahihi sana wa kubadilisha mambo, ratiba ya ligi inanibana sana, hapa tunachofanya ni kujaribu kufanya mambo kwa taratibu ili tusiharibikiwe, unaona sasa ndani ya siku 10 tumecheza mechi tatu,” amesema Josiah.
“Ukiangalia kwa sasa tuna changamoto kubwa ya kufunga mabao timu inatengeneza nafasi lakini haifungi na siyo kwamba tuna wachezaji wasiofaa nina imani sana na wachezaji wangu kitu muhimu hapa ni muda wa kuwaunganisha.
Aidha Josiah aliongeza baada ya mchezo wa leo dhidi ya Pamba Jiji, wanaweza kupata wiki tatu ambazo atazitumia kubadili mambo katika kikosi chake.
“Hapa karibuni baada ya mchezo wa Pamba tutapata muda wa kutosha kama wiki tatu hadi nne na kwa muda huo tutajipanga kufanya mambo baadhi ambayo yatatuongezea ubora kwenye mechi zetu.”
