Polisi: Mchungaji Mtaita hakutekwa, tunamshikilia kwa uchochezi

Babati. Jeshi la Polisi mkoani Manyara, linamshikilia mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Boay wilayani Babati, Eleth Mtaita akidaiwa kufanya uchochezi.

Akizungumza kwa njia ya simu na Mwananchi leo Kumamosi Oktoba 25 mwaka 2025, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, Ahmed Makarani amesema mchungaji huyo hakutekwa, bali alikamatwa jana Oktoba 24 mwaka 2025 na wanamshikilia kwa mahojiano kuhusu tuhuma za uchochezi.

“Huyo mchungaji hajatekwa, Polisi tunamshikilia tunamuhoji kwani anafanya uchochezi kwenye kanisa lake kuhusiana na watu wasiende kupiga kura,” amesema Kamanda Makarani.

Amesema pia wanamtafuta mmoja kati ya masheikhe wa msikiti uliopo eneo hilo la Boay, Juma Silima pia kwa kuwataka watu wasiende kupiga kura Oktoba 29 mwaka 2025.

Amesema viongozi wa dini wanapaswa kuendelea kuzungumza juu ya masuala ya kumuabudu Mungu na si kujihusisha na mambo ya siasa.

“Kanisani na msikitini si mahali pa kufanya siasa, hivyo tunamshikilia mchungaji huyo na pia huyo sheikh tunaendelea kumtafuta kwa kufanya uchochezi,” amesema Makarani.

Tangu usiku na alfajiri ya leo Oktoba 25 mwaka 2025 kwenye mitandao ya kijamii kulizuka taharuki juu ya kutekwa kwa mchungaji huo.

Taharuki hiyo ilizuka baada ya mchungaji huyo kuelezwa ametekwa nyumbani kwake na watu wasiojulikana waliovamia wakiwa na silaha.

Imeelezwa kwamba watu hao walitumia silaha kuwatishia wanafamilia wa mchungaji Mtaita, kabla ya kumpakia kwenye gari na kuondoka naye kwa kasi, wakitumia gari aina ya Toyota Land Cruiser lisilo na namba za usajili.

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga hivi karibuni akizungumza na waandishi wa habari alisema Serikali itawachukulia hatua kali wote watakaochochea watu wasijitokeze kupiga kura.

Sendiga alieleza kwamba kitendo cha baadhi ya watu kuieleza jamii kuwa isijitokeze kushiriki uchaguzi mkuu kwa kupiga kura, watakuwa wanafanya makosa hivyo watawachukulia hatua kali za kisheria.