KOCHA Mkuu wa Nsingizini Hotspurs, Mandla Qhogi, amesema licha ya kikosi hicho kupoteza kwa mabao 3-0, dhidi ya Simba katika mechi ya mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, ila wana nafasi ya kurekebisha kasoro zilizojitokeza.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mandla, amesema anatambua ugumu uliopo wa kushinda ugenini kwa zaidi ya mabao manne, ingawa katika mpira wa miguu kila kitu kinawezekana pia.
“Kabla ya mechi yetu ya kwanza hakuna aliyetarajia pia kama Simba ingeshinda ugenini kwa idadi kubwa ya mabao, hii ni mechi nyingine ngumu ila tutapambana kadri ya uwezo wetu.”
Aidha, Mandla amesema licha ya ugumu wa kupindua matokeo ya kwanza, ila watapambana kwa ajili ya Taifa lao na mashabiki wa Eswatini.
“Unapotaja miongoni mwa timu tano Barani Afrika huwezi kuiacha kuitaja Simba, tunatambua tunaenda kucheza kwenye uwanja wenye uwezo mkubwa wa kubeba mashabiki zaidi ya 60,000, hivyo, tuna kazi pia ngumu ya kufanya, ili tusonge hatua inayofuata.”
Kwa upande wa nyota wa timu hiyo, Khanyakwezwe Shabalala, amekiri deni kubwa wanalokabiliana nalo kama wachezaji, ingawa sio kigezo cha kucheza kwa presha zaidi wakiwa ugenini.
“Tumefanyia kazi mapungufu makubwa ambayo tulionyesha mechi yetu ya kwanza, hususani kuwaruhusu wapinzani wetu kutushambulia kwa kutushtukiza,” amesema Shabalala.

