Matola, Kapombe waitangazia vita Nsingizini Hotspurs 

KOCHA Msaidizi wa Simba, Selemani Matola na nahodha wa timu hiyo, Shomari Kapombe, wametamba kuendelea kufanya vizuri katika mechi ya mkondo wa pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika, dhidi ya Nsingizini Hotspurs.

Mechi hiyo ya marudiano itakayopigwa kesho Jumapili Oktoba 26, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, Simba inaingia ikiwa na morali baada ya pambano la kwanza lililopigwa Eswatini kushinda mabao 3-0, Oktoba 19, 2025.

Akizungumzia na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, Matola amesema licha ya ushindi mzuri katika mechi ya kwanza, ila hawatabweteka kwa sababu wanahitaji kufunga mabao mengi zaidi.

INS 01

“Ni kweli tuna uzoefu mkubwa katika hii michuano lakini hatutaki kurudia kile kilichowahi kutukuta misimu kadhaa nyuma, hii ni mechi nyingine yenye uhitaji mkubwa kama ilivyokuwa ile ya mwanzoni ugenini,” amesema.

Aidha Matola, amesema kitendo cha timu hiyo kuchaguliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kuwania tuzo ya klabu bora ya mwaka 2025, ni ishara ya kuwapa motisha ya kufanya vizuri.

“Sio kwa bahati mbaya sisi kupata hiyo nafasi kwa sababu ni kutokana na mafanikio ambayo tumekuwa nayo ya kimataifa, kwetu inatupa morali ya kuzidi kupambana katika michuano hii mikubwa Barani Afrika,” amesema.

INS 02

Akizungumzia hali ya wachezaji wa timu hiyo, Matola amesema beki wa kikosi hicho, Wilson Nangu aliyepata majeraha mechi ya kwanza yupo fiti kucheza, huku kiungo mshambuliaji, Mohamed Bajaber akiendelea vizuri baada ya kupewa programu maalumu.

Kwa upande wa nahodha wa timu hiyo, Shomari Kapombe, amesema licha ya ushindi katika mechi ya kwanza ila wao kama wachezaji wamejipanga vizuri kuendeleza kiwango bora zaidi.

“Niwaombe mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kwa sababu mechi za kwanza hawakupata hiyo nafasi, hii ni fursa nyingine nzuri ya kuendelea kuandika historia mpya kwa umoja wetu,” amesema na kuongeza;

INS 03

“Nina majukumu mazito kama nahodha ya kuipelekea Simba mbali zaidi ya hapa, naamini kwa umoja na ushirikiano wetu tutafikia malengo ambayo tumedhamiria kwa msimu huu.”

Simba inaingia katika mechi hiyo ikihitaji sare au ushindi wa aina yoyote ile ili itinge katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo droo yake itafanyika Novemba 3, 2025 huko jijini Johannesburg Afrika ya Kusini.