KIUNGO wa zamani wa Simba, Hamis Abdallah amewataka wachezaji wa Pamba Jiji kusikiliza na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ili kufanikisha malengo ya klabu hiyo msimu huu kumaliza katika nafasi tano za juu.
Baada ya msimu uliopita kunusurika na janga la kushuka daraja, Pamba Jiji msimu huu imejiwekea lengo la kumaliza katika nafasi tano za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ukiwa ni wa pili mfululizo kushiriki baada ya kurejea ikipita takribani miaka 22.
Abdallah aliyedumu Simba kwa mwaka mmoja (2023-2024), msimu huu anaitumikia Pamba Jiji ya Mwanza baada ya kujiunga nayo dirisha kubwa lililofungwa Septemba 2025.
Akizungumza jijini Mwanza, Abdallah amesema licha ya uwepo wa wachezaji wenye uzoefu na vipaji vipya una faida kwa klabu hiyo, lakini akatahadharisha kwamba hautaleta tija kama wachezaji hawatowasikiliza makocha wao.
“Sisi kama wachezaji wenye uzoefu pamoja na wengine hatuwezi kuwa na maana kama hatumsikilizi mwalimu. Malengo ya timu ni kumaliza tano bora, tunahitaji kumaliza hapo ndipo malengo binafsi ya sisi wachezaji yatafuata,” amesema Hamis.
Kuhusu matokeo ya timu hiyo, Abdallah amesema tayari kikosi chao kimeshapitia maumivu ya kufungwa, sare na raha ya ushindi, hivyo kinahitaji kuwa na mwendelezo na kuwapa furaha mashabiki wake katika mechi zijazo.
“Bila shaka pia uwepo wetu (wazoefu) unaweza kuwa chachu kwa wachezaji wachanga. Tumeshaonja ladha ya kufungwa, kutoa sare, kwahiyo hatuhitaji mambo mengi tunahitaji ushindi,” amesema kiungo huyo.
Licha ya uzoefu wake, nyota huyo aliyewahi kukipiga nje ya nchi katika klabu za Al-Sadd na Al-Duhail za Qatar, Hadiya Hossan FC (Ethiopia), Sony Sugar na Bandari FC za Kenya, bado hajapata nafasi ya kuaminiwa katika kikosi cha kwanza cha Pamba Jiji chini ya kocha Francis Baraza.
 
                         
                         
                         
                         
                         
			 
			 
			 
			