Ameolewa ananilazimisha nitembee naye | Mwananchi

Nilikuwa na uhusiano wa mapenzi na binti mmoja kwa miaka kadhaa kabla ya kuachana na kila mmoja kushika njia yake.

Baadaye mimi nilioa na nimebahatika kupata watoto wawili, mwenzangu pia nilikuja kujua alishaolewa na ana mtoto mmoja.

Jambo la ajabu ambalo linaniweka njia panda ni huyu mwenzangu kuniganda kuendeleze uhusiano wetu akidai wakati huu tumekuwa kiakili ndiyo tutafurahia sana kuliko wakati ule maisha yalikuwa yakitusukuma huku na kule.

Licha ya ukweli kuwa huyu mwanamke nilimpenda sana, wazo lake hili linaniumiza kichwa ukizingatia ninajua mke wa mtu ni sumu nami ninaiheshimu ndoa yangu. Kwa kweli Anti ninashindwa nifanye nini au nimjibu vipi anielewe na asiniwekee nongwa/ Kwanza hongera sana kwa uamuzi wako wa kuheshimu ndoa yako na kutambua kwamba mke wa mtu ni sumu.

Huo ni ukomavu wa kipekee, hasa katika dunia ya leo ambapo maadili ya ndoa mara nyingi yanatetereka. Jambo unalopitia ni zito kihisia hasa ukizingatia huyu mwanamke aliwahi kuwa mpenzi wako na ulimpendana kama siyo kupendana.

Muhimu kutambua kuwa anachokifanya huyo mwanamke kukung’ang’ania ni jaribu kama majaribu mengine na unapaswa kulishinda.

Lakini niamini mimi hisia ulizokuwa nazo awali kama unampenda mkeo hazitakuwa na nafasi tena. Unaweza kuvutiwa naye lakini kwa muda tu.

Ndoa ni agano takatifu na jukumu la kimaadili na kiroho. Kwa hiyo, kuyalinda mapenzi yako ya sasa ni wajibu wako wa kwanza kitamaduni, kisheria na kidini.

Kama mwanamke huyo anaendelea kukulazimisha, jambo la kwanza hakikisha kunakuwa na mipaka baina yenu, usikubali kukaa naye faragha kwa namna yoyote ile.

Pia usiingie kwenye mkenge wa kujibu ujumbe wake wa mapenzi na epuka mawasiliano yasiyo ya lazima. Akikuuliza kuhusu masuala tofauti hasa yale muhimu kama ya kazi, kijamii na kiuchumi mjibu tofauti na hapo mkalie kimya.

 Unapokuwa thabiti kwenye msimamo wako, ataona kwamba huna udhaifu wa kihisia anaoweza kuutumia kutimiza azma yake hiyo mbaya.

Pia, kumbuka kuwa heshima ya ndoa yako ndiyo heshima yako binafsi. Wengi wameshuhudia maisha yao yakiharibika kwa kukubali tamaa ya muda mfupi.

Ukiruhusu mwanamke huyo kuingia tena kwenye maisha yako ya kimapenzi, hautakuwa tu unamsaliti mke wako bali pia unajiweka katika hatari ya aibu, migogoro, na majeraha makubwa ya kihisia kwa familia zote mbili.

Zingatia kumuomba Mungu akuepushe na vishawishi kama anavykuletea huyo mpenzi wako wa zamani asiyeheshimu ndoa yake. Maombi yana nguvu ya kukulinda na kukuimarisha. Kila unapotaka kudhoofika, jiulize: “Je, ni faida gani nitakayopata nikiharibu amani ya ndoa yangu kwa sababu ya kumbukumbu za zamani?”

Kwa hiyo, usiogope kusema hapana kwani huyo mwanamke siyo tu atakuvunjia heshima yake bali pia atakuweka kwenye migogoro na mumwe. Wahenga walisema: ‘penzi kikohozi kulificha huliwezi’, naamini hata mjifiche vipi mtabainika na mumewe hatokuelewa utajishushia heshima na kutengeneza adui wa kujitakia.

Umeonyesha msimamo na wasiwasi wa kujiuliza mara mbili na kutaka ushauri umefanya jambo jema, mwisho huyo mwanamke kaa naye mbali hakutakii mema na hana adabu kwani hajiheshimu hata yeye mwenyewe.

Mwanamke anayejiheshimu humheshimu mumewe na familia yake kwa ujumla anachotaka kukifanya si miongoni mwa tabia za wake wema. Ukiweza mweleze kinagaubaga kuwa huna mpango wa kuwa na uhusiano naye tena, atulie kwenye ndoa yake.