Nitaendelea Kuimarisha Udhamini Na Miundombinu Ya Michezo – Global Publishers


Mgombea wa nafasi ya Rais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali itaendelea kufanya kila juhudi kuhakikisha wadhamini katika sekta ya michezo wanapatikana, ili kukuza vipaji na kuinua ustawi wa michezo nchini.

Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 26 Oktoba 2025, baada ya kuongoza matembezi ya wanamichezo kutoka vikundi vya mazoezi ya viungo, vilivyoanzia Hoteli ya Bwawani, kupitia Darajani–Michenzani hadi Viwanja vya Michezo vya Maisara, Mkoa wa Mjini Magharibi.

Amesema kuwa upatikanaji wa wadhamini utasaidia kukuza vipaji vya vijana, jambo litakaloiwezesha Zanzibar kupata wanamichezo bora watakaoiwakilisha nchi ndani na nje ya mipaka yake.

Dkt.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kushirikiana na taasisi na wadau mbalimbali kuhakikisha michezo inapata udhamini wa kutosha, ili kukuza vipaji na kutoa ajira kwa vijana wetu.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali itashirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kupata wakufunzi bora watakaowajengea uwezo walimu wa michezo wa ndani ya nchi, ili kuimarisha taaluma na ushindani wa michezo.

Matembezi hayo ni sehemu ya kampeni zake zinazoendelea visiwani Zanzibar, ambazo zinahusisha mikutano na vikao na makundi mbalimbali ya kijamii, kwa lengo la kuomba ridhaa ya wananchi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.

Ameeleza kuwa Ilani ya CCM imetekelezwa kikamilifu katika sekta ya michezo kupitia ujenzi wa viwanja vya kisasa kama New Amaan Complex, Mao Tse Tung, na Gombani Pemba, huku Serikali ikiendelea na ujenzi wa viwanja 17 vya wilaya, viwili kati yake vikiwa na akademi za michezo.

Halikadhalika, Dkt.Mwinyi amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha vyama vyote vya michezo vinaendeshwa kwa mfumo wa kisasa, sambamba na kuweka mazingira bora kwa uendeshaji wa shughuli zao, ikiwemo upatikanaji wa ofisi rasmi.

Kuhusu ukosefu wa gym kwa wanamichezo, Dkt. Mwinyi ameahidi Serikali kulifanyia kazi suala hilo, pamoja na kuanzisha bwawa la kuogelea lenye viwango vya Olimpiki katika eneo la Fumba.