Trump aanza ziara barani Asia, kukutana na rais wa China

Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Donald Trump leo Jumapili Oktoba 26, 2025 amewasili nchini Malaysia ikiwa ni kituo chake cha kwanza katika ziara yake barani Asia.

Ziara hiyo itahusisha mazungumzo muhimu ya biashara na Rais wa China, Xi Jinping nchini Korea Kusini katika siku ya mwisho, akilenga kufikia makubaliano ya kumaliza vita vya kibiashara.

Leo Jumapili Oktoba 26,2025 Rais Trump amesaini makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Thailand na Cambodia ambapo mkataba huo umesiniwa na Waziri Mkuu wa Thailand, Anutin Charnvirakul, na Waziri Mkuu wa Cambodia, Hun Manet, kwa kushirikiana na Trump na Waziri Mkuu wa Malaysia, Anwar Ibrahim.

Makubaliano hayo yanajumuisha kuachiwa kwa wafungwa wa kivita 18 wa Cambodia kwa misingi ya kibinadamu, kwa mujibu wa taarifa ya wizara ya mambo ya nje ya Cambodia ikinukuliwa na DW.

Thailand na Cambodia zilikubaliana kusitisha mapigano mwishoni mwa Julai hatua iliyosaidiwa na ushawishi wa Trump ingawa pande zote mbili zimekuwa zikilaumiana kwa uvunjaji wa makubaliano hayo.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutiwa saini, Trump amesema ni “hatua kubwa ya kihistoria” na akawapongeza Anutin na Hun kwa ujasiri wao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia, Mohamad Hasan, ambaye ameongoza mazungumzo kwa niaba ya Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN), amesema makubaliano hayo mapya yanalenga kuanzisha ujumbe wa waangalizi wa kikanda katika maeneo ya mpaka, kuondoa silaha nzito, na kusafisha mabomu ya ardhini yaliyosalia katika mpaka wa nchi hizo mbili.

Hata hivyo kwa mujibu wa DW akiwa njiani kutoka Washington, kuna tetesi Trump anaweza pia kukutana na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, kwa mara ya kwanza tangu 2019, kwa ajili ya mazungumzo.

Hii ni safari yake ya kwanza barani Asia tangu kurejea Ikulu Januari, akiwa na sera za ushuru na mikakati mipya ya biashara ya kimataifa.

Akiwa njiani kuelekea Malaysia, Trump alisema anatarajia kufikia “makubaliano ya kina” na China ili kuepusha ushuru wa ziada wa asilimia 100 unaotarajiwa kuanza kutumika Novemba 1.

Vilevile akiwa Malaysia, atahudhuria mkutano wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN), ambao aliukosa mara kadhaa katika muhula wake wa kwanza, na atasaini pia makubaliano ya biashara na serikali ya Malaysia.

Aidha Trump katika ziara hiyo anatarajiwa kusimama nchini Japan kukutana na kiongozi mpya wa kwanza mwanamke wa nchi hiyo, aliyechaguliwa hivi karibuni Sane Takaichi.