MGOMBEA UBUNGE CHATO KUSINI AOMBA KURA MLANGO KWA MLANGO

Kulia ni mgombea Ubunge Jimbo la Chato kusini,Paschal Lutandula,akiomba kura.

………….

CHATO 

SIKU Moja baada ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, kuhitimisha kampeni za jukwaani za Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Chato kusini, mgombea wa Ubunge wa Jimbo hilo, Paschal Lutandula, ameendelea na kampeni za nyumba kwa nyumba ili kuomba kura za Rais, Mbunge na diwani.

Akiwa katika kata ya Buziku wilayani Chato mkoani Geita, amezungumza na baadhi ya wakazi wa kata hiyo kwa lengo la kuwaomba kuwapigia kura wagombea wa Chama hicho.

Lutandula amewataka wamuamini kutokana na kuwa na dhamira  ya kweli ya kuwatumikia wananchi hao na kwamba anazitambua shida za kata hiyo.

Mbali na hilo, ameendelea kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi hao ili kuepuka kuharibika kwa kura za Rais, Mbunge na diwani wa kata hiyo, Salama Mgasa.

Akiwa ameongozana na kamati ya ushindi ya Jimbo la Chato kusini, Lutandula amesema ni busara na heshima kubwa kuwatembelea wapiga kura kwenye kaya zao badala ya kuwasubiria kwenye mikutano ya kampeni pekee.

Amesema wananchi ndiyo wenye mamlaka ya kuweka viongozi katika utawala wa kidemokrasia, na kwamba ni muhimu kuwaomba wajitokeze kupiga kura ili kutimiza azma yao ya kikatiba.

Baadhi ya wananchi waliozungumza na Torch Media, Sifael Enock na Ester Komanya, wamesema wanayo Imani kubwa na Chama Cha Mapinduzi kuwa ndiyo Chama pekee kinachoweza kutoa viongozi wanaofaa kuongoza taifa.

“Tunayo Imani kubwa na CCM kwa maana ndiyo Chama pekee ambacho kimekuwa kikidumisha amani na maendeleo ya nchi hii” amesema Komanya.

Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani unatarajiwa kufanyika nchi nzima Oktoba 29 mwaka huu.

                           Mwisho.