SIMBA imeweka rekodi mpya baada ya kufuzu hatua ya makundi kwa mara ya saba katika miaka minane, lakini kama taifa kukiwa na rekodi nyingine kali ya kufanikiwa kuingiza timu nne kwenye michuano ya CAF kwa mara ya kwanza.
Kuanzia mwaka 2018 Simba ilianza utawala wa soka la Tanzania kwenye michuano ya CAF na leo iliweka rekodi nyingine baada ya kutoka suluhu na Nsingizini Hotspurs ya eSwatini katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Simba imefuzu kwenye hatua hiyo muhimu kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-0 baada ya mchezo wa kwanza ikiwa ugenini kupata ushindi wa mabao 3-0.
Hii imekuwa timu ya nne kwa Tanzania kufuzu hatua ya makundi kwenye michuano ya CAF, ikiwa ni rekodi ya kwanza tangu timu za nchi hii zianze kushiriki michuano hiyo, lakini ndiyo nchi pekee Afrika Mashariki ambayo imefanikiwa kufanya hivyo kwa miaka yote.
Yanga na Simba zimefuzu kwenye hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa huku Azam na Singida juzi zikipata nafasi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushinda michezo yao na sasa zinasubiri droo ya makundi itakayopangwa siku saba mbele.
Kikosi cha Simba leo kilianza bila mshambuliaji asilia kwa mara ya kwanza msimu huu, lakini mwanzoni mwa kipindi cha pili kocha huyo akawaigiza kwa pamoja Steven Mukwala na Jonathan Sowah ambapo walitoka Morice Abraham na Jean Charles Ahoua, lakini bado mastaa hao walishindwa kuipenya ngome ya Nsingizini ambao walionekana kucheza kwa tahadhari kubwa tofauti na mchezo wa kwanza wakiwa nyumbani kwao.
Hii ina maana sasa kuna uhakika kwa timu zote kuchuma fedha za kutosha kwenye michuano hiyo msimu huu, timu zote zinazoingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika zina uhakika wa kuchukua kuanzia kitita cha dola 700,000 (sawa na Sh1.7 bilioni) huku timu inayotinga hatua hiyo kwenye Kombe la Shirikisho ikizoa dola 400,000 (sawa na Sh 1 bilioni).
Kipindi cha kwanza kilikuwa na mvutano mkubwa katikati ya uwanja kuliko eneo la mwisho la umaliziaji kwa timu zote kupambana kumiliki mpira huku mashambulizi yakikosa utulivu.
Shambulizi zuri lilikuwa dakika ya 27 ambapo wageni Nsingizini walitengeneza shambulizi zuri lakini kipa Yakub Seleman aliruka imara na kupangua na kuwa Kona.
Shambulizi hilo ndio pekee lililotengeneza shuti lililolenga lango kwenye dakika 45 za kwanza, ingawa Simba ndio iliyomiliki mpira vizuri kwenye kipindi hicho cha kwanza kushinda wapinzani wao.
Hali hiyo ya timu zote kushambuliana kwa zamu ikiendelea kipindi cha pili ambapo Simba ndio walikuwa wa kwanza kutengeneza shambulizi zuri dakika ya 55 kupitia Elie Mpanzu lakini kipa Dlamini Thabo alisimama imara na kupangua.
Simba ilifanya mabadiliko matano dakika ya 57 wakiwatoa Morrice Abraham, Elie Mpanzu, Jean Charles Ahoua na Yusuf Kagoma nafasi zao zikichukuliwa na Alassane Kante, Neo Maema, Steven Mukwala na Jonathan Sowah.
Mabadiliko hayo yalikwenda kuwaimarisha wekundu hao katika eneo la kiungo cha ukabaji na kile cha kushambulia huku pia ikiifanya Simba kucheza na washambuliaji wawili mbele.
Nsingizini ilifanya shambulizi lingine zuri dakika ya 64 kupitia adhabu ndogo shuti la Joel Madondo likagonga mwamba na kurudi uwanjani.
Wageni wakafika tena vizuri lango la Simba kwa shambulizi kali dakika 67 mashuti ya Dlamini Sinenkosi na Mavuso Thubelihle yaiishia kwenye miili ya mabeki wa Simba, Nsingizini ikitengeneza presha kubwa kwenye lango la wenyeji.
Shambulizi lingine zuri kwa Simba likafanyika dakika ya 87 kupitia Sowah baada ya kumtoka vizuri kipa Dlamini Thabo lakini shuti lake likagonga mwamba chini.
Mpaka mwisho wa mchezo timu hizo zilimaliza dakika 90 bila kufungana huku wekundu hao wakinufaika na ushindi wa mchezo wa kwanza na kutinga makundi.
Simba katika safari ya kucheza hatua ya makundi michuano ya CAF mara sita kipindi cha miaka saba iliyopita, imekuwa mikononi mwa makocha sita tofauti walioweka rekodi hiyo, akiwamo mzawa mmoja Juma Mgunda.
Baada ya kupita miaka mingi, Simba ilianza kwa kufuzu makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2018-2019 ikiwa inafundishwa na kocha Patrick Aussems.
Katika mechi iliyoipeleka Simba hatua ya makundi, iliifunga Nkana jumla ya mabao 4-3, kufuatia mechi ya kwanza kupoteza ugenini kwa mabao 2–1, kisha nyumbani Simba ikashinda 3–1.
Baada ya hapo, 2019-2020, haikufika makundi, lakini kuanzia hapo, suala la Simba kucheza hatua ya makundi michuano ya CAF kwa maana ya Kombe la Shirikisho au Ligi ya Mabingwa, limekuwa ni jambo la kawaida.
Sven Vandenbroeck aliipeleka Simba hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2020–2021 baada ya kuiondosha FC Platinum kwa jumla ya mabao 4-1. Licha ya mechi ya kwanza ugenini kupoteza kwa bao 1–0, ikarudi nyumbani na kuiangushia mvua ya mabao 4–0.
Kidogo Simba iliteleza msimu wa 2021-2022 katika Ligi ya Mabingwa Afrika ikashindwa kufuzu makundi ikiwa chini ya Thierry Hitimana ambapo timu hiyo ilishinda ugenini 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy, nyumbani ikachapwa 3-1, ikatolewa kwa kanuni ya bao la ugenini matokeo ya jumla yakiwa 3-3.
Simba ikaangukia mtoano kucheza kuwania kufuzu makundi upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, ndipo kocha Pablo Franco Martin akakabidhiwa kikosi huku Hitimana akiwa msaidizi, timu ikafanya kweli kwa kufuzu makundi Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2021–2022 ikiiondosha Red Arrows kwa jumla ya mabao 4-1. Simba ilianzia nyumbani ikishinda 3–0, ugenini ikaenda kuchapwa 2–1.
Juma Mgunda anaingia kwenye rekodi ya kuipeleka Simba makundi upande wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ilikuwa msimu wa 2022–2023 ambapo alikabidhiwa kikosi kwa muda ikiwa ni baada ya kuondoka kwa Didier Gomes De Rosa.
Mgunda aliiongoza Simba kushinda ugenini mabao 1–3 dhidi ya 1º de Agosto, nyumbani Simba ikashinda tena 1–0, ikafuzu kwa jumla ya mabao 4-1.
Roberto Oliveira ‘Robertinho’ naye aliipeleka Simba makundi Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023–2024 kwa kuitoa Power Dynamos kwa bao la ugenini, mechi ya kwanza ugenini matokeo yalikuwa 2–2, nyumbani 1–1.
Fadlu Davids akaja kufunga kazi, msimu wa 2024-2025 akaipeleka Simba makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika akiifunga Al Ahli Tripoli jumla ya mabao 3–1. Ugenini matokeo yalikuwa 0-0, nyumbani Simba ikashinda 3–1.
Simba: Yakub Seleman, David Kameta,Antony Mligo, Rushine de Reuck, Chamou Karaboue, Yusuf Kagoma/Allasane Kante,Joshua Mutale/Aweso Aweso, Morice Abraham/Steven Mukwala,Kibu Denis, Jean Charles Ahoua/Neo Maema, Elie Mpanzu/Jonathan Sowah.
Nsingizini Hotspurs: Dlamini Thabo,Adeleke, Ade,Vuyo Macina/Ayanda Gadlela,Kwakhe Thwala, Kingsley Kwakyi, Dlamini Senzo, Mavuso Thubelihle/Sambulo Simelane,Khumalo Sizwe/Veemak Jordyn, Shongwe Nkosingphile, Joel Madondo/Mthethwa Mvuselelo, Dlamini Sinenkosi.
