Kocha Mreno atua Yanga na mifumo mitatu

YANGA inarudi kambini leo haraka na wachezaji wa timu hiyo wakifika tu AVIC Town watakutana na kocha wao mpya, Pedro Goncalves, akiwa anawasubiri tayari kwa kuanza kazi.

Yanga itakuwa kwenye mazoezi ya kwanza tangu ifuzu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mazoezi hayo yatakuwa pia ya kwanza chini ya kocha wao huyo Mreno aliyetua na wasaidizi wawili.

Pedro ametua na kocha atakayekuwa msaidizi wake wa kwanza Philipe Pedro na kocha wa makipa Fernando Pereira.

Wakati Goncalves akianza kazi Yanga amewaambia mabosi wa timu hiyo kuwa kuna kazi ya kufanya kubadilisha mambo lakini kwa haraka anataka kuwashusha presha wachezaji wake.

YAN 01

Bosi mmoja wa juu ndani ya Yanga amesema hakufurahishwa na namna wachezaji wake walivyokuwa wanacheza wakiwa na presha kubwa hatua ambayo iliwasababishia kupoteza utulivu wa kushinda vizuri.

Kwenye mchezo huo dhidi ya Silver Strikers, licha ya Yanga kushinda kwa mabao 2-0, ingeweza kushinda kwa ushindi mkubwa zaidi kama ingetumia nafasi ilizotengeneza.

Mshambuliaji Prince Dube ndiye aliyeshushiwa lawama nyingi na mashabiki baada ya kupoteza nafasi nyingi za wazi kwenye mchezo huo.

YAN 02

“Kocha hana shida na ubora wa wachezaji, lakini ameuliza kwanini wachezaji wanacheza kama wana presha kubwa sana ambayo imewapunguzia utulivu” amesema bosi huyo.

“Tumemwambia labda ni kwa kuwa tulitaka sana kufuzu makundi, amesema haitakiwi kuwa hivyo kwani kama ingekuwa wanacheza dhidi ya timu bora zaidi mambo yangekuwa mabaya.

“Ila amekiri wana kazi ya kufanya kwani ubora wa timu uko chini na kesho (leo) ataanza kazi rasmi kule Avic, tuna imani kwamba mambo yatabadilika.”

YAN 03

Yanga chini ya Pedro inaweza kuja kutumia mifumo mitatu tofauti ambayo kocha huyo alikuwa akiitumia akiwa na Angola 4-4-2, 3-5-2 na pia 4-2-3-1.

Falsafa ya kocha huyo ni kuona timu yake inacheza soka la nidhamu la kuvutia, ikiwa na mipango sahihi ya kuzuia na kushambulia.

Kwenye mifumo hiyo, mfumo wa 4-2-3-1 ndio umekuwa maarufu ndani ya Yanga ukianza kutumiwa na makocha wanne tofauti kuanzia Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead Ramovic na Hamdi Miloud.

YAN 04

Pedro akiwa Yanga ataanza historia mpya kwa kuwa kocha mkuu wa klabu ambapo kwenye historia ya wasifu wake kama kocha, hakuwahi kufundisha klabu na kuwa kocha mkuu, akibahatika kuwa kocha msaidizi mara mbili akizifundisha Amora na Cova da Piedade za kwao Ureno.

Akiwa na timu ya taifa ya Angola, Pedro alishinda Kombe la Cosafa mwaka jana.

YAN 05

Kama kuna mchezaji amelaumiwa kwenye mchezo wa juzi alikuwa ni mshambuliaji Prince Dube ambaye alionekana kukosa utulivu akipoteza nafasi nyingi za kufunga tena za wazi.

Hata hivyo, baada ya hali hiyo Dube mwenyewe aligundua kuna kitu hakipo sawa na kuomba kutolewa kisha kwenda kukaa kwa majonzi kufuatia yale aliyokutana nayo ndani ya uwanja.

Wengi wamekuwa wakimlaumu Dube, lakini usahihi ni benchi la ufundi la Yanga na hata viongozi, kumsaidia mshambuliaji wao huyu kisaikolojia badala ya kushambulia kama ambavyo baadhi wanafanya.

Kocha Mabedi alionekana akiongea na mshambuliaji huyo kwa muda mrefu na ulikuwa uamizi mzuri kutuliza presha yake kutokana na yale yaliyotokea kwenye mchezo huo.

Kocha mpya Pedro aliyetambulishwa kuchukua nafasi ya Romain Folz, ana kibarua kikubwa Yanga katika kufuata nyayo ama kupita mafanikio ya watangulizi wake.

Nabi aliifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo yenye miaka 90 tangu ilipoanzishwa mwaka 1935 na mbali na kuipa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara mbili, Ngao ya Jamii na rekodi ya taifa ya kucheza mechi 49 za ligi mfululizo bila ya kupoteza, Gamondi na Hamdi na wenzake pia waliweka rekodi za kibabe Jangwani. Hata Folz aliyedumu kwa muda mfupi sana, alishinda Ngao ya Jamii tena kwa kumfunga mtani Simba.

Hii ni ishara kwamba Pedro ana kazi ya kufanya ili kuirejesha katika makali Yanga ambayo msimu huu licha ya kushinda imekuwa ikicheza soka ambalo linaacha miguno kwa mashabiki wake.