Maandalizi ya upigaji kura Kigoma Kusini yakamilika

Uvinza. Wananchi 259,617 wa jimbo la Kigoma Kusini wanatarajia kupiga kura katika uchaguzi mkuu unatarajia kufanyika Oktoba 29, 2025,  huku maandalizi yakiwa yamekamilika kwa asilimia mia ikiwa ni pamoja na uwepo wa vifaa vya kupigia kura.

Hayo yamesemwa leo Jumapili, Oktoba 26, 2025 na Msimamizi wa uchaguzi jimbo la Kigoma Kusini, Acland Kambili wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wasimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo  yaliyofanyika wilayani Uvinza, Kambili amesema idadi ya wananchi hao ndio waliojiandikisha katika daftari la kudumu la mpigakura.

Amesema kun vituo 660 katika kata 16 za jimbo la Kigoma Kusini na jumla ya wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi 1,980 wanatarajia kupata mafunzo hayo ya siku mbili. 

“ Nitoe rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura, vifaa vyetu vimewasili na vya kupigia kura na sasa tunavisambaza kwenye vituo husika lakini pia usalama upo wa kutosha kwa kila atakayetoka kwenda kupiga kura siku ya Oktoba 29,”amesema Kambili.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),  Jacobs Mwambegele amewataka wasimamizi  wa uchaguzi katika vituo vya kupiga kura kufuata sheria, kanuni na taratibu za INEC kwa muda wote watakaokuwa wanasimamia vituo hivyo,  ili kuepusha malalamiko kutoka kwa mawakala wa vyama vya siasa na wananchi kwa ujumla.

“Niwasihi kwa sasa msiache kusoma sheria, miongozo, kanuni na taratibu zilizotolewa na tume lakini pia mkasome Katiba yetu ya Tanzania na kama mtu atakuwa na swali lolote au kuna jambo halijaeleweka tafadhali usiogope kuuliza, lengo ni kujifunza na kutenda haki pamoja na kuwa na uelewa wa kutosha ili ikifika tarehe 29 usibabaike uwe unajua sheria zote na taratibu,”amesema Mwambegele 

Amesema wasimamizi hao wajiepushe kuwa chanzo cha malalamiko, wahakikishe vifaa vyote vya kupigia kura viko sawa na vimetimia, kila mmoja afike mapema katika kituo alichopangiwa na ikifika saa 1:00 asubuhi vituo vyote vitatakiwa kuwa wazi na kuanza kupokea wapiga kura. 

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema wapo tayari kwenda kutekeleza majukumu yao kama walivyoapa bila kuegemea upande wa chama chochote.

Benard Jacob amesema siku ya uchaguzi mkuu wataenda kutenda haki kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa hatua zote za upigaji kura hadi kumalizika.

Vumilia Ayoub amesema pamoja na mambo mengine katika mafunzo haya amejifunza kuwapa kipaumbele watu wa makundi maalumu wakiwemo   wajawazito, wazee na walemavu, na muhimu katika yote ni kutunza siri ili kuwezesha mchakato mzima wa uchaguzi kuanzia kupiga kura hadi kutangazwa kwa matokeo kumalizika salama.