NYOTA wa kimataifa na nahodha wa timu ya taifa, Mbwana Samatta jana Jumapili alitimiza jumla ya dakika 519 kupitia mechi nane za Ligi Kuu ya Ufaransa bila ya kufunga bao.
Samatta aliyetua katika Ligue 1 msimu huu, akijiunga na Le Harve akitokea PAOK ya Ugiriki aliyokuwa amemaliza nao mkataba, amekosa mechi moja ya ligi hiyo dhidi ya Rennes iliyoisha kwa sare ya 2-2 kutokana na kuwa majeruhi.
Katika mechi nane alizocheza Samatta ametumika kwa dakika 519 bila kufunga bao, lakini akipata kadi mbili za njano, huku timu hiyo ikivuna jumla ya pointi nane, Le Harve ikishinda mechi mbili na kuambulia pia sare mbili dhidi ya Metz na Lorient.
Rekodi zinaonyesha Samatta alianza kuitumikia Le Harve katika mechi ya kwanza dhidi ya Monaco kwa dakika 33 wakati timu hiyo ikipasuka kwa mabao 3-1.
Mechi ya pili ilikuwa dhidi ya Lens ambapo Chama la Samatta lililala mabao 2-1 huku nyota huyo wa Tanzania akilimwa kadi ya kwanza ya njano kabla ya kutumika kwa dakika 85 dhidi ya Nice iliyokubali kichapo cha mabao 3-1.
Samatta alitumika kwa dakika 90 kwa mara ya kwanza katika mechi ya kipigo cha bao 1-0 dhidi ya Strasbourg kisha akatumika kwa dakika 77 dhidi ya Lorient akipewa pia kadi ya njano wakati timu zikotoka sare ya 1-1.
Mechi nyingine tatu alizotumika na dakika zake katika mabano ni dhidi ya Metz (dk 61) ikiisha pia kwa sululu, Marseille (dk 38′) Le Harve ikipoteza kwa mabao 6-1 kabla ya jana usiku kucheza kwa dakika 62 dhidi ya Auxerre kumpisha Younes Namli, huku timu hiyo ya kina Samatta ikishinda bao 1-0 lililofungwa dakika 47 na Abdoulay Toure.
Kwa sasa Le Harve inashika nafasi ya 14 ikicheza mechi tisa za Ligue 1 ikishinda mbili, kutoka sare tatu na kupoteza nne, ikifunga mabao 11 na kufungwa 16 na kuvuna pointi tisa wakati PSG ikiongoza msimamo kwa kuwa na pointi 20 kupitia mechi tisa.
