Dar es Salaam. Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imewataka Watanzania wote waliotimiza vigezo vya kikatiba kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Kwa mujibu wa tamko lililotolewa na Mwenyekiti wa THBUB, Jaji mstaafu, Mathew Mwaimu, limeeleza kuwa kupiga kura ni haki ya msingi inayomuwezesha kila raia kushiriki katika maamuzi ya nchi kwa kuchagua viongozi wanaowataka katika nafasi za urais, ubunge na udiwani.
“Tume inawakumbusha wananchi kuwa, kupiga kura ni haki ya kikatiba na wajibu wa kila Mtanzania mwenye umri kuanzia miaka 18 na aliyejiandikisha, kuhakikisha anaitumia haki hiyo ipasavyo,” amesema Jaji Mwaimu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, THBUB imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa kampeni zinazoendelea na kutoa mafunzo kwa askari polisi na waandishi wa habari katika mikoa mbalimbali, lengo likiwa ni kuhimiza utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia haki za binadamu na misingi ya utawala bora wakati wa uchaguzi.
Aidha, amewataka wadau wote wa uchaguzi kuhakikisha upigaji kura unafanyika katika mazingira ya amani na utulivu, ili kila mwananchi mwenye sifa aweze kutekeleza haki yake ya kikatiba bila hofu wala usumbufu.
Endelea kufuatilia Mwananchi
