Mtoto wa Mjini – 15

KATIKA mitoko yote waliyokuwa wakifanya, kuna kitu kilimshangaza sana Linnie, pamoja na starehe zote lakini Muddy hakuwa mnywaji wa pombe.
Hata pale mwanamke huyo alipojaribu kumshawishi alikutana na kipingamizi, Muddy hakuwa akinywa na mara zote alikuwa akitumia vinywaji laini visivyokuwa na kilevi cha aina yoyote.
Uhusiano wao ulizidi kuimarika na watu wengi walizidi kuwaonea wivu. Tangu Muddy akutane na Linnie maisha yake yalibadilika kwa kiasi kikubwa na kuwa mtu wa kutazamika mbele ya watu.
Maisha yalimkubali ngozi yake ilinawiri na kuwa na afya na mwonekano wa kupendeza sana mbele za macho ya watu.
Sio kiafya tu hata katika maisha kwa ujumla alikuwa ni tofauti na Muddy yule aliyekuwa akiishi mitaa ya Gerezani, Kariakoo jijini Dar es Salaam. 
Wanawake wengine waliokuwa wakimuona akitoka na Linnie wakaaanza kummezea mate, waliitamani nafasi ya mwanamke mwenzao. 
Wanawake hao wakaanza kumfanyia visa na kumpa ahadi za maisha mazuri zaidi ya yale aliyokuwa akipata kwa Linnie.
***
Baada ya kesi ya Muddy kuisha na mzee Mangushi kuwa huru, ingawaje ilitumika nguvu kubwa kuweza kuimaliza kutokana na maaskari wengi kutaka kuifufua mara kwa mara na kumtishia mzee Mangushi kwa nia ya kutaka kumtoa pesa, wazazi wa Muddy wakaanza kuumizwa na kitendo cha kutokujua alipokuwa mtoto wao.
Damu nzito kuliko maji, familia ikaanza kuteseka na kutamani kujua kama Muddy alikuwa hai au alikuwa amefariki dunia.
Walijaribu kufanya uchunguzi kwa marafiki zake wa mtaani kujua kama alikuwa akiwasiliana nao lakini hawakuweza kuzipata taarifa zake.
Miezi iliendelea kukatika na hakuna aliyekuwa na taarifa za Muddy, mtu pekee aliyekuwa na taarifa hizo ambaye angeweza kuwahakikishia kwamba Muddy alikuwa hai ni Hamisi ambaye naye aliamua kulowea Nairobi.
Tangu Hamisi alipoingia katika nchi hiyo hakutaka kurudi Tanzania na alikuwa ameanza maisha mapya kwa kushirikiana na Fashanu na jamaa zake.
Watu waliowafahamu Muddy na Hamisi waliamini kwamba walikuwa pamoja, lakini kilichokuwa kinawapa wasiwasi ni kwamba Hamisi alionekana siku chache baada ya Muddy kutoweka.
Akili za kuamini kwamba Muddy alikuwa ametoroka nje ya nchi ni kama ilikuwa ikiwaingia na kutoka.
Katika kutaka kujiridhisha kama Muddy bado yuko hai, familia ikawatuma ndugu zake wawili, Meja na Kizanda kwenda Kimanzichana, mkoani Pwani kwa mganga wa kienyeji mzee Matobo ambaye aliaminika kwamba alikuwa na ujuzi mkubwa wa kuweza kutambua mambo mengi.
Mara baada ya Meja na Kizanda kufika, mzee Matobo aliwaambia asingeweza kufanya chochote bila ya kupata nguo ya mhusika na kondoo mmoja.
Ilibidi ndugu hao warudi tena Dar es Salaam kuchukua nguo ya Muddy na pesa ya kondoo kisha kumpelekea mtaalamu huyo wa tiba asilia.
Waliporudi kwa mara ya pili, mzee  Matobo aliwataka kujiandaa kwa safari ya kwenda kwenye mzimu wake. Ilikuwa ni mbali na pale walipofikia na aliwataka safari hiyo ifanyike usiku wa manane.
Iliwabidi Meja na Kizanda kukubaliana na masharti ya mganga kwa sababu walitakiwa kwenda huko wakiwa wamevaa kaniki tu huku wakiwa matumbo wazi.
Ilikuwa ni safari ya kutisha na kuogofya sana kwa kupandisha mabonde na milima hadi kufika katika mizimu ya mzee Matobo.
Mara baada ya kufika mzee Matobo kwa kusaidiana na kina Meja na Kizanda alimchinja kondooo chini ya mti mkubwa uliokuwa ukiamimika kwamba ndipo ilipokuwa mizimu yake kisha aliichukua nguo ya Muddy na kuiweka chini ya mti huo na kuanza kuzungumza na mizimu yake kwa lugha asiyoeleweka na wengi.
Kabla ya kuanza kuzungumza na mizimu yake, mzee Matobo alimwaga dawa na damu ya mbuzi chini ya mti ule huku kile kisu kilichochinjiwa kondoo kikiwa juu ya vitu hivyo, kisha kwa dakika kama kumi hivi upepo mkali ulivuma kiasi cha kuwatisha wateja wake.
Mara upepo alipotulia ndipo mzee Matobo alipoanza kuzungumza na mizimu yake katika lugha ambayo hakuna kati ya Meja na Kizanda aliyekuwa akiijua.
Kulikuwa na sauti iliyokuwa ikitoka kwenye mti ule mkubwa, lakini ilikuwa kama inanguruma hivi na kutoa mitetemo ni mzee Matobo pekee ndiye aliyekuwa akiilewa kilichokuwa kikizungumzwa na aliendelea kujibu kwa lugha hiyo isiyoeleweka.
Baada ya kumaliza kazi yake aliwaageukia wateja wake na kuwaambia kwamba ndugu yao bado alikuwa hai na alikuwa katika maisha mazuri.
“Yuko mbali sana na maisha yake ni mazuri…” alisema mzee Matobo kuwaambia Meja na Kizanda ambao nao hawakuwa na maswali zaidi kutokana na furaha ya kuamini kwamba ndugu yao alikuwa hai.
Hata waliporudi nyumbani na kutoa taarifa hiyo, waliulizwa maswali mengi ambayo hawakuwa na majibu nayo.
Baba yao mzee Manyara alikuwa mkali na kuwaambia makosa ambayo waliyafanya kwa kushindwa kumuuliza mzee Matobo maswali.
“Ilitakiwa mumuulize yuko mbali ya wapi? Tanzania hii hii au nje ya nchi…
“Pia, mlitakuwa kuuliza kama atarudi salama au ndio hatarudi tena?” Mzee Manyara aliendelea kuwaambia wanawe kwamba walitakiwa kumwambia mzee Matobo amfanye Muddy arudi nyumbani.
***
Usifanye mchezo na damu ya mswahili, baada ya miezi mitano ya kuwa na uhusiano kati yake na Muddy, Linnie alipatwa na mabadiliko makubwa ya mwili.
Hali yake ilibadilika na kuonekana kunawiri na kuwa mrembo zaidi ya alivyokuwa awali. 
Hatimaye akakosa kuziona ada zake za mwezi na ilikuja kubaini alikuwa ni mjamzito.
Ilikuwa ni furaha kwa Linnie kwa sababu ulikuwa ni ujauzito wake wa kwanza katika maisha yake. Alipokuwa na uhusiano na mwanamume wake wa kwanza wa Kizungu aliyekuwa akiishi naye awali hawakufikia katika hatua hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alizidi kumpenda Muddy kwa kuamini alikuwa mwanamume rijali na sahihi kwake, kitendo cha kupata mtoto kilikuwa katika akili yake na alikuwa akihisi kama alikuwa amechelewa kukifia.
Mbali na mapenzi Linnie aliongeza uaminifu kwa Muddy, akamfanyia kila jambo zuri alilokuwa akilitaka, ulikuwa humwambii kitu kuhusu mwanaume huyo. 
Pia, kwa upande wa pili ilikuwa furaha kubwa sana kwa Muddy, kupata mtoto na mwanamke wa Kizungu. Aliamini ni kitendo cha ushujaa wa hali juu kwake.
Kitendo ambacho hakijawahi kufanywa na mtu yeyoye katika ukoo wao kwa mwanamke wa Kizungu. Mababu na mababu walikuwa wamepita hakuna kati yao aliyewahi kuchanganya rangi na mzungu.
Pia, alifurahi kwa sababu sehemu ya ndoto yake ilikuwa inaenda kutimia, alikumbuka maneno waliyokuwa wakihadithiana katika kijiwe chao pale Gerezani na kina Ally Baga na Hamisi Sungajao kuhusu wanawake wa Kizungu. 
Aidha, alikumbuka ndoto yake ya kurudi Tanzania akiwa na mwanamke wa Kizungu sambamba na mtoto wao na kuwafunga midomo watu wote waliokuwa wakimbeza na kumdharau.
Hapo aliwakumbuka wanawake wote waliokuwa wamemkataa. Wamo wale aliokuwa akiishi nao jirani pale Kariakoo, pia akawakumbuka wanawake aliokuwa akisoma nao ambao walikuwa wakimkataa kwa kuwa hakuwa na kitu.
“Nitawafunga midomo…” aliwaza huku akijisifu kwa hatua aliyokuwa ameifikia hadi wakati huo. Hiyo ilikuwa ni moja tu ya sehemu ya ndoto zake, bado kulikuwa na kitu kimoja tu kilichokuwa hajakikamilisha, ndoto zake. Ndoto ya kumiliki gari ya kifahari…fikra zake zilikuwa ni kumiliki gari aina ya BMW…
“Nikiwa na mke wangu na mwanangu ndani ya BMW… tunavinjari mitaa ya Kariakoo….hata wazee watanipa shikamooo…” aliwaza Muddy huku akipiga hesabu za kufanya kazi kwa bidii ili siku akirudi nyumbani aweze kununua nyumba maeneo ya Kariakoo au Ilala kama sio Magomeni Mapipa.
“Ndio, mtoto wa mjini hawezi kuishi mbali na maeneo hayo,” aliwaza na kuamini kama atapambana ataweza kununua gari ya ndoto zake.
Mbali na ndoto hizo za Muddy, maisha ndani ya nyumba yao kati yake na Linnie yalikuwa na upendo sana, naye katika kipindi hiki alizidisha mapenzi sana kwa mpenzi wake, alikuwa akimdekeza kwa kumzuia kufanya kazi nzito… kila kitu alikuwa akitaka kukifanya yeye.
Mbali na hivyo, alikuwa akijitahidi kurudi nyumbani mapema na kumnunulia Linnie zawadi mbalimbali ambazo alikuwa akizipenda na kuzidisha upendo.
***
Kuna msemo maarufu unaosema ‘kunguru hafugiki hata umpe nini’… Kuna kitu kilikuwa kinamsumbua Muddy, hakuyapenda kabisa maisha ya Sigtuna.
Pamoja na jitihada zote zilizokuwa zikifanywa na Linnie, lakini bado maisha katika kitongoji hicho yalikuwa yakimshinda. 
Muddy hakupenda kabisa kuishi katika kitongoji hicho kidogo, mara kadhaa alikuwa akimsumbua Linnie kumtaka wahamie katika Jiji la Stockholm.
“Mtoto wa Mjini hawezi kuishi Sigtuna… anaishi Stockhom…,” maneno hayo alikuwa yakipita katika fikra za Muddy mara kwa mara.
Kilichokuwa kikimsumbua alikuwa akifikiria kuishi katika kitongoji hicho kutamfanya akose mambo ya kwenda kuhadithia kwa wenzake siku atakaporudi nyumbani, Tanzania.
Fikra zilimwambia Tanzania ni Dar es Salaam, Kenya ni Nairobi na Sweden ni Stockholm. Ndio sehemu ambazo Mtoto wa Mjini anapaswa kuishi…  
Hata hivyo, mpango wake wa kumshawishi Linnie kuhama katika mji huo ulishindikana kutokana na kukutana na vipingamizi vingi kutoka kwa mwanamke huyo.
Linnie alikuwa na msimamo mkali kuhusu maisha yake, hakutaka kupangiwa pa kuishi na alimwambia Muddy asingeweza kuhamia Stockholm kwa sababu sehemu aliyokuwa akiishi alikuwa ameachiwa na wazazi wake ambao wametangulia mbele ya haki.