Musoma. Watu sita wamefariki dunia na wengine wanane kujeruhiwa mkoani Mara katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita baada ya kutokea matukio 16 ya moto na maokozi.
Taarifa hiyo imetolewa mjini Musoma leo Oktoba 27,2025 na Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Mara, Augustine Magere alipokuwa akipokea magari manne kwa ajili ya jeshi hilo mkoani Mara.
Amefafanua kuwa matukio hayo yaliyotokea katika kipindi hicho, matukio tisa yalikuwa ni ya moto na saba yakikuwa ni ya maokozi.
Magere amesema katika kutimiza wajibu na majukumu yao jeshi hilo limekuwa likikumbana na changamoto kadhaa ikiwemo ujenzi holela wa makazi, ambapo wakazi wengi wa mkoa huo hujenga nyumba zao bila ramani zao kupitishwa na jeshi hilo kama inavyotakiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi akikata utepe wakati wa kukabidhi magari manne kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani humo. Picha na Beldina Nyakeke
“Kwa kipindi cha Julai hadi Septemba 2025 kulikuwa na matukio 16 ya moto na uokozi na katika matukio hayo kulikuwa na vifo sita na majeruhi wanane, pia changamoto nyingine ni wizi wa mifuniko ya visima vya kuchota maji ambavyo wezi hao wanakwenda kuuza kama chuma chakavu,” amesema.
Ameongeza kuwa matumizi mabaya ya namba ya dharura ya 114 ni changamoto nyingine wanayokumbana nayo ambapo wapo baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kupiga simu na kuanza kuongea vitu ambavyo havihusiani na madhumuni ya namba hiyo, au wengine kutoa taarifa za uongo kuhusu matukio ya moto au maokozi.
Akikabidhi magari hayohilo, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi amesema lengo la Serikali kununua magari hayo ni kutaka kuhakikisha huduma zinazotolewa na jeshi hilo zinakidhi viwango na zinapatikana kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (mwenye suti ya bluu) akipata ufafanuzi kutoka kwa Ofisa wa jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara Dikson Madale . Picha na Beldina Nyakeke
Amesema hatarajii kusikia malalamiko ya wananchi kuhusu huduma za jeshi hilo ikiwepo kuchelewa kufika kwenye tukio au kufika huku gari la zimamoto likiwa halina maji kwa maelezo kuwa changamoto hizo zimetatuliwa kwa ununuzi wa magari hayo
“Kwa magari haya natarajia kuona utendaji kazi wenu ukiboreshwa zaidi na kuwa wa viwango vya juu, muwe tayari muda wowote na vifaa viwe tayari muda wote kwa sababu majanga ya moto ama maokozi ni matukio yanayotokea muda wowote na wakati wowote, na huduma yenu inatakiwa kuwafikia wananchi ndani ya muda mfupi,” amesema.
Ameliagiza jeshi hilo kufanya ukaguzi kwenye majengo yote ya Serikali ili kuona kama miundombinu yake inakidhi vigezo na matakwa ya zimamoto na kwa yale yatakayopatikana na mapungufu yafanyiwe kazi mara moja, ili kuepuka athari zinazoweza kutokea ikiwepo vikwazo vya kuzima moto endapo kutatokea moto kwenye majengo hayo.
Kuhusu matumizi mabaya ya namba za dharura, Kanali Mtambi ameagiza kuchukuliwa hatua kwa wale wote watakaobainika kufanya hivyo kwa maelezo kuwa mbali na kuwa ni kinyume cha sheria, lakini pia vitendo hivyo wakati mwingine vinasababisha wananchi wengine kushindwa kutoa taarifa kwa wakati kwani kila wakipiga simu wanakuta inatumika.
