MGOMBEA UBUNGE CHATO KUSINI APATA CHAKULA KWA MAMA NITILIE AKIOMBA KURA

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato kusini, Paschal Lutandula(Kushoto) akipata chakula kwa mama lishe

………………..

 CHATO 

MGOMBEA Ubunge wa Jimbo la Chato kusini kupitia tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Paschal Lutandula, ameshiriki chakula cha mchana kwa mama lishe (mama nitilie) kisha kuwaomba kura za Rais, Mbunge na diwani.

Mgombea huyo ambaye amekuwa akijinasibisha kuwa mtoto wa mama lishe, amewaomba wamiliki wa migahawa hiyo pamoja na wateja waliokuwa wakipata chakula eneo hilo kutofanya makosa ifikapo Oktoba 29, mwaka huu.

Alikuwa kwa mama lishe wanaofanya biashara ya chakula eneo la Ofisi za CCM Buseresere kisha kuwaahidi wafanyabiashara wa matunda kuboresha soko lao iwapo watamchagua kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.

Amesema mpango mkakati alionao ni kuupima mji wa Buseresere ili ukae katika ramani nzuri na kuboresha miundombinu ya mama lishe pamoja na wauza matunda waliopo mjini hapo.

Katika ziara hiyo ya nyumba kwa nyumba mlango kwa mlango imelenga kuomba kura kwa wananchi wa makundi yote ili kukipatia ushindi wa kishindo CCM ifikapo Oktoba 29,2025.

“Ndugu zangu nimefika hapa ili kumwombea kura Mgombea Urais wa CCM mama yetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, mimi mwenyewe kama mgombea Ubunge na Mange Samwel kuwa diwani wa kata yenu ya Buseresere”,

“Muhimu mtambue kuwa kukipigia kura za ndiyo CCM ni kuchagua maendeleo, amani, umoja, mshikamano na utulivu wa kitaifa”amesema Lutandula.

Kwa upande wake Katibu wa Umoja wa wauza matunda soko la CCM Buseresere, amemuahidi mgombea huyo kuwa atarajie kuona kura zake, Rais pamoja na diwani zinajaa kwenye sanduku la kupigia kura siku ya Uchaguzi mkuu.

Hata hivyo amemwomba kusaidia ujenzi wa miundombinu ya soko la matunda ili kuondoa adha iliyopo hivi sasa kwa wananchi hao.

                          Mwisho.