Safari ya uchaguzi kutoka Mwalimu Nyerere hadi Samia

Safari ya uongozi wa Tanzania ni hadithi ya mabadiliko na maono ya kitaifa yaliyosukwa kwa vizazi. Tangu enzi za Mwalimu Julius Nyerere, Baba wa Taifa, hadi uongozi wa sasa wa Rais Samia Suluhu Hassan, nchi imepitia hatua mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Kila Rais ameacha alama yake katika kujenga taifa lenye amani, umoja, mshikamano na maendeleo endelevu, likibadilika kutoka misingi ya ujamaa hadi uchumi wa soko huria na sasa kuelekea katika zama za uwazi, ushirikiano na mageuzi ya kisasa.

Julius Kambarage Nyerere (1962–1985):

Mwalimu Julius Nyerere ndiye Baba wa Taifa na Rais wa kwanza wa Tanganyika, na baadaye Tanzania baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar wa Aprili 26, 1964.

Mwalimu aliongoza taifa akiwa rais kuanzia mwaka 1962 hadi alipong’atuka mwaka 1985.

Alitambulika kwa sera yake ya Ujamaa na Kujitegemea, iliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kijamii, kupunguza pengo la kiuchumi kati ya matajiri na maskini na kujenga jamii yenye usawa.

Aliongoza chini ya mfumo wa chama kimoja, awali TANU (Tanganyika African National Union) na baadaye CCM (Chama Cha Mapinduzi) baada ya muungano wa vyama vya TANU na ASP (Afro Shiraz Party) Februari 5, 1977.

Ingawa sera zake za ujamaa zilipata changamoto za kiuchumi katika miaka ya 1970, mchango wake katika ujenzi wa taifa, umoja wa kitaifa na misingi ya amani uliweka Tanzania katika dira ya kipekee barani Afrika.

Mwalimu Nyerere alipitia katika vipindi mbalimbali vya uchaguzi mkuu tangu 1962 ambapo alichaguliwa kuwa rais wa nchi.

Uchaguzi wa kwanza wa kumpata Rais ulifanyika Alhamisi ya Novemba 1, 1962 ukihusisha vyama vingi vya siasa.

Waliojiandikisha katika uchaguzi huo ni 1,800,000. Kura halali zilizopigwa ni 1,149,254. Julius Nyerere (TANU) alipata kura 1,127,978 (98.15%) na Zuberi Mtemvu (ANC) kura 21,276 (1.85%).

Uchaguzi mwingine ulifanyika Alhamisi ya Septemba 30, 1965, Mwalimu Nyerere alichaguliwa bila kupingwa. Waliojiandikisha kupiga kura ni 3,373,089. Waliojitokeza kupiga kura ni 2,600,040 (77.1%). Kura zilizoharibika ni 100,537. Kura halali zilikuwa ni 2,499,503. Hata hivyo, kura za NDIYO zilikuwa ni 2,410,903 (96.46%) na kura za HAPANA zilikuwa 88,600 (3.54%).

Katika uchaguzi wa Ijumaa ya Oktoba 30, 1970, ambapo waliojiandikisha ni 5,051,938, kura halali zilikuwa 3,575,401. Katika hizo, kura za NDIYO ni 3,465,573 (96.93%) na HAPANA ni 109,828 (3.07%).

Katika uchaguzi wa Oktoba 26, 1975 ambao waliojiandikisha walikuwa 5,577,566, kura halali zilikuwa 4,474,272. Matokeo ni kwamba kura za NDIYO zilikuwa 4,172,267 (93.25%) na za HAPANA: 302,005 (6.75%).

Uchaguzi wa mwisho kwa Mwalimu Nyerere ulifanyika Oktoba 26, 1980 ambapo waliojiandikisha walikuwa 6,969,803. Katika kupiga kura, kura halali zilikuwa 5,829,923, Kura za NDIYO zilikuwa 5,570,883 (95.56%) na za HAPANA 259,040 (4.44%).

Baada ya kuongoza kwa zaidi ya miongo miwili, Nyerere aling’atuka mwaka 1985, na kukabidhi madaraka kwa Rais Ali Hassan Mwinyi.

Ali Hassan Mwinyi (1985–1995):

Ali Hassan Mwinyi alichukua madaraka mwaka 1985, akijulikana kama Rais wa Mageuzi au Mzee Ruksa. Uongozi wake uliashiria mwanzo wa mageuzi makubwa ya kiuchumi na kisiasa nchini Tanzania.

Mwinyi alilegeza sera za kijamaa, akaruhusu sera za soko huria, na kufungua milango ya uwekezaji wa binafsi.

Katika kipindi chake, Tanzania ilianzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1992, hatua iliyokuwa ya kihistoria katika kuimarisha demokrasia ya kisiasa.

Aliingia madarakani kupitia uchaguzi uliofanyika Oktoba 27, 1985 ambapo Waliojiandikisha ni 6,910,555, kura halali zikiwa ni 4,993,740. Katika hizo, kura za NDIYO: 4,778,114 (95.68%) na HAPANA ni 215,626 (4.32%).

Katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, 1990 walijiandikisha wapiga kura 7,296,553 lakini kura halali zilikuwa ni 5,315,486. Katika hizo kura za NDIYO ni 5,198,120 (97.79%) na HAPANA ni 117,366 (2.21%),

Uchaguzi wa mwaka 1990 ulikuwa wa mwisho kufanyika chini ya mfumo wa chama kimoja kabla ya kuanzishwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.

Benjamin Mkapa (1995–2005):

Benjamin Mkapa alichaguliwa kuwa Rais wa tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 1995, katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi.

Uongozi wake ulijikita katika mageuzi ya kiuchumi, uwazi na uwajibikaji wa serikali. Mkapa alifanikiwa kupunguza deni la taifa kupitia sera za urekebishaji wa uchumi, kuimarisha sekta ya elimu, afya na mawasiliano, na kuongeza uwekezaji wa kigeni.

Alisisitiza utawala wa sheria na uadilifu katika utumishi wa umma, akiweka msingi wa maendeleo endelevu.

Mkapa aliingia madarakani kupitia uchaguzi wa Oktoba 29, 1995 ambao waliojiandikisha ni 8,929,969 lakini kura halali zilizopigwa ni 6,512,745. Mkapa (CCM) kura 4,026,422 (61.82%), Augustine Mrema (NCCR-Mageuzi) kura 1,808,616 (27.77%), Ibrahim Lipumba (CUF) 418,973 (6.43%) na John Cheyo (UDP) 258,734 (3.97%).

Mkapa alishinda tena uchaguzi uliofanyika Oktoba 29, 2000. Waliojiandikisha ni 10,088,484 na kura halali zilikuwa 8,172,284. Mkapa alipata kura 5,863,201 (71.74%), Lipumba (CUF) 1,329,077 (16.26%), Mrema (TLP) 637,115 (7.80%) na Cheyo (UDP) 342,891 (4.20%).

Jakaya Kikwete (2005–2015):

Jakaya Kikwete alichaguliwa kuwa Rais wa nne mwaka 2005. Uongozi wake ulilenga kuendeleza uchumi, kuboresha huduma za kijamii na kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa.

Kikwete alitekeleza miradi mikubwa ya barabara, elimu, nishati na afya. Serikali yake ilihamasisha usawa wa kijinsia na ushirikiano wa kikanda, hasa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).Alijulikana kwa uongozi wa kidiplomasia na sera za uwiano wa kisiasa.

Aliigia madarakani katika uchaguzi wa Desemba 14, 2005. Kati ya wapiga kura 16,401,694 waliojiandikisha, kura halali zilikuwa 11,365,477. Kikwete (CCM) kura 9,123,952 (80.28%), Lipumba (CUF) kura 1,327,125 (11.68%), Freeman Mbowe (CHADEMA) kura 668,756 (5.88%).

Katika uchaguzi wa Oktoba 31, 2010 ambao waliojiandikisha ni 20,137,303, kura halali zilikuwa 8,398,394. Kikwete (CCM) alipata kura 5,276,827 (62.83%), Willibrod Slaa (CHADEMA) kura 2,271,941 (27.05%) na Lipumba (CUF) kura 695,667 (8.28%).

John Pombe Magufuli (2015–2021):

Dk. John Magufuli alichaguliwa kuwa Rais wa tano mwaka 2015. Uongozi wake ulijulikana kwa nidhamu ya kazi, kupambana na ufisadi, na utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati kama Bwawa la Nyerere, SGR na upanuzi wa barabara na viwanja vya ndege.

Alisisitiza matumizi bora ya rasilimali za taifa na uwajibikaji wa watumishi wa umma. Hata hivyo, utawala wake ulikumbwa na ukosoaji kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na upinzani wa kisiasa.

Dk Magufuli alifariki dunia Machi 17, 2021 akiwa madarakani.

Matokeo ya Uchaguzi wa 2015 ni kwamba Dk Magufuli (CCM) alipata kura 8,882,935, Edward Lowassa (CHADEMA) kura 6,072,848 huku wengine kwa pamoja wakipata chini ya asilimia moja ya kura halali.

Katika uchaguzi wa 2020 Dk Magufuli (CCM) alipata kura 12,516,252 (84%), Tundu Lissu (CHADEMA) kura 1,933,271 kura (13%) huku wagombea wengine 13 wakigawana kura zilizobaki chini ya asilimia 3.

Samia Suluhu Hassan (2021–Sasa):

Baada ya kifo cha Rais Magufuli, Samia Suluhu Hassan alichukua madaraka Machi 2021, na kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika historia ya Tanzania.

Rais Samia ameongoza kipindi cha maridhiano, diplomasia, na mageuzi ya kiuchumi. Ameimarisha uwazi wa serikali, kujenga mahusiano mazuri na jumuiya ya kimataifa, na kuhimiza ushirikiano kati ya serikali na sekta binafsi kupitia sera ya “Kazi Iendelee.”

Ameendelea kusukuma ajenda ya maendeleo endelevu, uwezeshaji wa wanawake na upatikanaji wa haki kwa wote.

Historia ya urais nchini Tanzania inaonyesha mabadiliko ya hatua kwa hatua kutoka kwenye sera za kijamaa za Mwalimu Nyerere, kupitia mageuzi ya kisiasa na kiuchumi ya Mwinyi, Mkapa na Kikwete, hadi siasa za uwajibikaji na miradi mikubwa chini ya Magufuli, na sasa diplomasia ya maridhiano na uwazi chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Kila rais amechangia kwa namna yake katika kujenga taifa lenye amani, umoja, na maendeleo endelevu, jambo linaloendelea kuwa nguzo kuu ya utambulisho wa Tanzania katika bara la Afrika.