Zanzibar kuanza kupiga kura kesho

Unguja. Ni dhahiri safari ya siku 46 za kampeni za kuusaka urais, ubunge, uwakilishi na udiwani kisiwani Zanzibar imekamilika baada ya kuhitimishwa leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025.

Kukamilika kwa kampeni hizo kunatoa nafasi kwa wananchi kupiga kura ya mapema kesho Jumanne, Oktoba 28, 2025, kabla ya kura kuu itakayojumuisha wapigakura wote keshokutwa, Oktoba 29.

Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), wapigakura 717,557 wanatarajiwa kupiga kura, kati ya hao wanawake ni 378,334 sawa na asilimia 53, na wanaume ni 339,223 sawa na asilimia 47

“Kati ya idadi hiyo, wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 ni 326,304 sawa na asilimia 45, wenye umri wa miaka 36 hadi 59 ni 300,986 sawa na asilimia 42, na wenye umri kuanzia miaka 59 na kuendelea ni 90,267 sawa na asilimia 13,” amesema Mkurugenzi wa Uchaguzi Zanzibar, Thabit Idarous Faina.

Kwa mujibu wa Sheria Namba Nne ya Uchaguzi ya mwaka 2018, imeelezwa kuwa kura ya mapema hufanyika kabla ya uchaguzi mkuu. Kura hiyo inawahusu watendaji wote wanaoshughulika na uchaguzi, walinzi na wasimamizi wa siku ya uchaguzi, ili waweze kutimiza majukumu yao bila changamoto zozote.

Safari ya kufikia hatua hiyo ya kupiga kura ilianza kwa mchakato wa kuwapata wagombea, kuteuliwa na kupitishwa na ZEC kuwania nafasi hizo.

Kwa mujibu wa Faina, tume imehidhinisha eneo moja la kupigia kura ya mapema kwa kila jimbo, hivyo kutakuwa na maeneo 50, Unguja ikiwa na vituo 32 na Pemba 18. Hata hivyo, katika maeneo hayo kutakuwa na vituo 407 kwa shehia zote 388, zikiwamo shehia za ziada.

Pia, imeidhinisha vituo vya kupigia kura 1,752; kati ya hivyo, Unguja ni 1,294 na Pemba ni 458, kwa ajili ya upigaji kura wa Oktoba 29.

Kwa mujibu wa ratiba ya ZEC, kampeni zilianza Septemba 11 na zinakamilika Oktoba 27 ili kupisha kura ya mapema.

Vyama vinavyoshiriki uchaguzi mkuu ni 18, ambavyo vimewasimamisha wagombea katika nafasi za ubunge, uwakilishi na udiwani. Hata hivyo, kwa nafasi ya urais ni vyama 11 pekee ambavyo wagombea wake waliteuliwa na ZEC kupeperusha bendera zao.

Miongoni mwa wagombea hao 11, wanaochuana zaidi ni Dk Hussein Mwinyi wa CCM anayetetea nafasi hiyo dhidi ya mshindani wake wa karibu, Othman Masoud Othman maarufu kama OMO wa ACT-Wazalendo, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais.

Wagombea wengine wa urais na vyama vyao katika mabano ni Said Soud Said (AAFP), Hussein Juma Salim (TLP), Khamis Faki Mgau (NRA), Laila Rajab Khamis (NCCR), Juma Ali Khatib (Ada-Tadea), Ameir Hassan Ameir (Makini), Hamad Rashid Mohamed (ADC) na Hamad Mohammed Ibrahim (UPDP).

Vyama vingine vitano vilishindwa kurejesha fomu zake, na chama kimoja cha CUF, licha ya kurejesha fomu, mgombea wake alishindwa kukidhi vigezo kwa kutowasilisha fomu ya wadhamini kwa mkoa mmoja kati ya mitano.

Wagombea wa vyama hivyo wamepita katika maeneo mbalimbali kujinadi na kuomba kura, huku kila mmoja akijinasibu kufanya kampeni za kisayansi na kukubalika na wananchi, hivyo kujihakikishia ushindi baada ya kupiga kura.

Zanzibar ina majimbo 50 ya uchaguzi, hivyo ina wagombea 50 wa uwakilishi na ubunge, na ina wadi 110, hivyo kufanya idadi ya wagombea wa udiwani kuwa idadi hiyohiyo.

Kwa nyakati tofauti, viongozi wa ZEC wameeleza namna watakavyoendesha uchaguzi wa haki, usawa na kuhakikisha kila mgombea anaridhika na matokeo ili kuepusha lawama na migogoro isiyokuwa na sababu.

Mwenyekiti wa ZEC, Jaji wa Mahakama Kuu Zanzibar, George Joseph Kazi, alisema tume inatarajia kuendesha uchaguzi kwa haki na uwazi kwa kila mmoja.

Katika kulitekeleza hilo, ZEC ilikutana na wadau wa uchaguzi kwa nyakati tofauti kuwapa mafunzo na miongozo kuhakikisha upigaji kura unakuwa wa amani na bila upendeleo.

Imeanza kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa uchaguzi, vyama vya siasa, waandishi wa habari, vyombo vya ulinzi na usalama, waangalizi wa uchaguzi, na makundi maalumu ya watu wenye ulemavu.

ZEC ilisisitiza kuwa kura ya mapema haipo kwa ajili ya wizi, kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa, bali ipo kwa ajili ya kumsaidia kila mwananchi kupiga kura. Mfumo huo umetokana na ripoti za uangalizi za mwaka 2010, na ukabainika kuwa mwarobaini wake ni kuweka kura ya mapema ambayo ni haki muhimu kikatiba.