Bilioni 120 zawekezwa upanuzi wa Muhas- Mloganzila, wafikia asilimia 50

Dar es Salaam. Ujenzi katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Kampas ya Mloganzila umefikia asilimia 50 ya utekelezaji, ukielezwa kukamilika kwake kutaongeza idadi ya udahili na kupunguza changamoto za upungufu wa miundombinu.

Ujenzi huo unafadhiliwa kwa dola milioni 45.5 za Marekani (Sawa na Sh120 bilioni) kupitia mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) wenye lengo la kupanua miundombinu na kuboresha mazingira ya mafunzo kwa wataalamu wa afya nchini.

Akizungumza leo Jumatatu, Oktoba 27, 2025 Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema uwekezaji huo unaofadhiliwa na Benki ya Dunia ni mkubwa zaidi kuwahi kupokelewa na chuo tangu kuanzishwa kwake.

“Huu ndio uwekezaji mkubwa zaidi katika historia ya chuo tangu kuanzishwa kwake kama shule ya tiba mwaka 1963,” amesema Profesa Kamuhabwa.

Amesema kati ya fedha hizo, dola milioni 30.5 zimeelekezwa katika ujenzi wa miundombinu, katika kampasi ya Mloganzila na kampasi mpya ya Kigoma.

“Kupitia mradi wa HEET, Muhas imepokea dola milioni 45.5, ambazo ni mkopo nafuu wa Benki ya Dunia kwa Serikali ya Tanzania,” amesema.

Akizungumzia ujenzi wa Chuo Kikuu cha Tiba katika eneo la Mloganzila ulioanza Desemba 2024 amesema kwa sasa umefikia asilimia 50 ya utekelezaji.

Kati ya majengo yanayojengwa ni pamoja na ukumbi wa mihadhara wenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,400, jengo la utawala lenye ofisi 450, maabara 21 za kufundishia, jengo la anatomia linaloweza kutumika na watu 300 kwa wakati mmoja, hosteli yenye vitanda 320 kwa wanafunzi na ukumbi wa chakula wenye uwezo wa kuhudumia watu 550 kwa wakati mmoja.

“Pia mradi huo unahusisha maktaba na kituo cha Tehama, barabara za ndani zilizoboreshwa, na uwanja wa mpira wa miguu,” amesema akifafanua kwamba ujenzi unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2026.

Kwa upande wa kampasi ya Kigoma, amesema ujenzi wake umefikia asilimia 35, majengo ya utawala na masomo yanaendelea kujengwa pamoja na maabara sita, jengo la anatomia na hosteli ya wanafunzi yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 110.

Amesema eneo hilo limechaguliwa kimkakati kuhudumia Kanda ya Magharibi, ambayo mara nyingi hukumbwa na changamoto za kijiografia na magonjwa ya milipuko.

“Fedha hizi zitasaidia kuanzishwa kwa kampasi ya afya katika kanda ya magharibi, eneo lenye changamoto kubwa za kiafya,” amesema.

Amesema upanuzi huo utaongeza idadi ya wanafunzi na kupunguza changamoto za upungufu wa miundombinu.

“Kwa kila waombaji 31, huwa tunamchukua mwanafunzi mmoja tu kwa sababu ya upungufu wa miundombinu,”amesema, akitolea mfano mwaka uliopita ambapo waombaji 31,026 waligombea nafasi 986 pekee za shahada ya kwanza Muhas.

Amesema kupitia mradi wa HEET, chuo kimefanya maboresho makubwa katika programu 83 za masomo na kuanzisha programu 23 mpya, huku ajira zaidi ya 300 zikiwa zimeshatolewa katika kipindi cha ujenzi.

Profesa Kamuhabwa amefafanua kwamba mazingira mapya ya kujifunzia yatavutia wanafunzi wa kimataifa na kuimarisha nafasi ya Muhas kama kituo bora cha mafunzo ya afya katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Mazingira bora ya kujifunzia vilevile yataongeza udahili wa wanafunzi wa kimataifa na kuimarisha hadhi ya Muhas,” amesema.

Aidha profesa huyo aliishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kipaumbele inachotoa katika uwekezaji wa sekta ya elimu ya juu na afya.

“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kuendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika kuboresha miundombinu ya elimu ya juu, hususan hapa Muhas,” amesema Kamuhabwa.

Mratibu wa HEET na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Erasto Mbugi amesema mradi huo unaendelea kwa kasi na kwa ufanisi mkubwa.

“Ujenzi unaendelea haraka na kwa namna ilivyopangwa, utakapokamilika mradi huu utaleta mageuzi makubwa katika mafunzo ya afya na kusaidia kuziba pengo lililopo la wataalamu wa afya nchini,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Mloganzila, Ahmad Ladack amesema mradi huo umekuwa baraka kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na fursa za ajira na biashara ulizozalisha.

“Mradi huu umekuwa neema kubwa kwa vijana wa mtaa wetu kwani wengi wamepata ajira. Ukikamilika, utakuwa umewanufaisha wananchi wetu kwa namna kubwa,” amesema.

Amesema pia ujenzi huo umeongeza mahitaji ya huduma na bidhaa za ndani, hivyo kuchochea uchumi wa jamii ya Mloganzila.