Zanzibar. Katika kuunga mkono juhudi za kuwaletea maendeleo wananchi, Benki ya CRDB, kwa kushirikiana na taasisi ya fedha ya Ufaransa ya BPIFrance, imesaini mkataba wa kuikopesha Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Sh115 bilioni kwa ajili ya kufunga Mfumo wa Usimamizi na Usajili wa Taarifa za Ardhi (LARIS).
Mkopo wa mfumo huo, unaotarajia kuondoa changamoto katika sekta ya ardhi, hasa migogoro ya makundi tofauti, umetolewa kwa ushirikiano wa CRDB, itakayotoa Euro milioni 7.949, na taasisi ya fedha ya Ufaransa ya BPIFrance, itakayotoa Euro milioni 29.55.
Akizungumza kwenye hafla ya kusaini mkataba huo iliyofanyika Ikulu visiwani Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amesema ardhi ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya wananchi, hivyo Serikali imeona ni vyema kuipa thamani inayostahili kwa kuimarisha usimamizi wake.
“Nawashukuru CRDB kwa kutuunga mkono katika wazo letu hili. Inachokifanya Serikali ni kuweka mazingira rafiki kwa kila mwananchi kunufaika na ardhi anayoimiliki.
“Tuna hakika baada ya kufunga mfumo huu wa LARIS, taarifa zote za umiliki na usimamizi wa ardhi hapa Zanzibar zitapatikana kirahisi, hivyo kuondoa migogoro ya mipaka na matumizi mengine ya ardhi,” amesema Dk Mwinyi.
Kumalizwa kwa migogoro ya ardhi kwa kutumia mifumo ya kidijitali, Dk Mwinyi amesema kutawapa nafasi wananchi kuitumia ardhi kuomba mikopo benki na taasisi nyingine za fedha ili kutekeleza miradi na biashara walizonayo, hivyo kuharakisha kasi ya kujiletea maendeleo.
“Mfumo huu utaongeza kasi ya kutoa leseni kwa wananchi na kumaliza changamoto ya uvamizi wa maeneo ya wazi au yale ya serikali na wawekezaji. Nawasihi Wazanzibari wote kutambua fursa njema zitakazoletwa na mfumo huu na kujiandaa kwa manufaa ya kiuchumi yanayotokana na ardhi iliyorasmishwa,” amesisitiza Dk Mwinyi.
Kwa upande wake, Waziri wa Ardhi Zanzibar, Rahma Kassim Ali, amebainisha kuwa mfumo huu pia utainufaisha Serikali kwani utarahisisha utambuzi wa wamiliki wote wa ardhi visiwani humo, jambo litakalowapa nafasi nzuri wasimamizi katika ngazi zote kukusanya kodi ya ardhi.
“Ninaamini pindi mfumo huu utakapoanza kufanya kazi, makusanyo ya kodi ya ardhi yataongezeka kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka taifa,” amesema.
Akisaini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema mfumo huo utazalisha mageuzi makubwa katika sekta ya ardhi visiwani Zanzibar kwa kuweka misingi imara ya usimamizi na umilikishaji wa ardhi kwa njia ya kidijitali.
Amesema utekelezaji wa mradi huo utafungua fursa mpya za kifedha na kiuchumi, kwani urasimishaji wa ardhi utajenga imani kwa taasisi za fedha, zikiwemo benki, katika kutoa mikopo na huduma nyingine za kifedha kwa wananchi.
Aidha, amebainisha hatua hii itachochea ustawi wa wananchi kupitia uboreshaji wa huduma, ukuaji wa uwekezaji, na ujenzi wa uchumi shirikishi unaowanufaisha Wazanzibari wote.
Akizungumza kuhusu utayari wa taasisi za nje ya nchi kushirikiana na benki ya ndani na Serikali katika mradi huo, Nsekela amesema hiyo inaonesha imani ya wadau wa kimataifa kwa Serikali na CRDB katika kuusimamia miradi mikubwa ya kimkakati.
Kwenye mkakati wake wa biashara wa muda wa kati wa 2023/27, CRDB imeweka kipaumbele kikubwa katika ushirikiano wa kimkakati na wadau wa kimataifa ili kurahisisha ufanikishaji wa ufadhili wa miradi mikubwa ya maendeleo nchini na katika mataifa ambako benki inatoa huduma zake.
Nsekela amebainisha kuwa kutokana na ushirikiano huo, tayari CRDB imeshiriki na kufanikisha ujenzi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), na kwa upande wa Zanzibar, Benki ya CRDB imewekeza zaidi ya Sh484 bilioni kusaidia ufadhili ujenzi wa miundombinu ya barabara, shule za kisasa, na Uwanja wa Ndege wa Pemba.
Katika kuchochea maendeleo nchini, Nsekela amesema pia benki hiyo imewekea katika ubunifu wa huduma na bidhaa, akitolea mfano utoaji wa hatifungani za kijani na hatifungani ya miundombinu ya ‘Samia Infrastructure Bond’, ambazo kwa pamoja zilikusanya jumla ya zaidi ya Sh494 bilioni kwa ajili ya kusaidia miradi ya kijani pamoja na ujenzi wa miundombinu kwa kushirikiana na TARURA.
“Hivi karibuni pia tumetoa hatifungani inayofuata misingi ya sharia ya dini ya Kiislamu ‘CRDB Al Barakah Sukuk’ iliyotuwezesha kukusanya Sh125.4 bilioni na dola milioni 32.3 za Marekani.
“Fedha hizi zote zinalenga kuchochea kasi ya maendeleo katika sekta mbalimbali ikiwamo ujasiriamali na biashara, kilimo na uvuvi, elimu, afya, utalii, pamoja na utekeleza miradi ya kimkakati kwa maendeleo ya taifa letu,” amesema Nsekela.
Akieleza namna BPIFrance ilivyojipanga kushirikiana na Afrika, Makamu wa Rais anayesimamia Mikopo ya Nje wa benki hiyo, yenye makao makuu yake jijini Paris, Ufaransa, Alienor Daugreilh, amesema wana uzoefu wa kutosha, na walipopokea ombi kutoka SMZ walilitekeleza kwa haraka kwani wanafahamu jinsi uchumi wa visiwa hivyo ulivyo imara na unaokua kwa kasi nzuri.
